Saturday, December 28

Suala la uharibifu wa mazingira Mtambwe Kusini bado changamoto.

NA ABDI SULEIMAN.

WANANCHI wa Shehia ya Mtambwe Kusini Wilaya ya Wete, wamesema suala la uharibifu wa mazingira juu ya ukataji wa miti katika shehia yao, limekua likiwaumiza kichwa licha juhudi mbali mbali wanazozichukua.

Walisema hali hiyo imepelekea maji ya bahari kuingia katika mashamba ya kilimo, jua kua kali, kukosekana kwa mvua katika shehia yao kitu ambacho hawajakizowea.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa shehia hiyo, walisema wanaofanya uharibifu huo ni vijana kutoka ndani ya shehia kwa kushirikiana na wageni, kutoka shehia za jiran zikiwemo ndagoni, Mchanga mdogo, Jojo na Micheweni.

Salum Hamid Kombo mkaazi wa Mtambwe Kusini, alisema uharibifu wa mazingira upo kwa kiasi kikubwa, kwani miti inakatwa kwa ajili upigaji wa mkaa, majenzi, kuni za kupikia majumbani na bekarini na Vikosi vya SMZ.

“Wengi wanaoharibu mazingira ni watu kutoka ndani ya shehia husika, wakishirikiana na wanaotaka nje na kupeleka kuathiri mazingira yao, yote yanatokana na tamaa za kifedha na kusahau wanawahatarisha ukame,”alisema.

Aidha aliwataka wananchi wenzake wa mtambwe Kusini, kujitahidi kulinda maliasili ambazo zimekua zikipotea kila siku kutokana na tamaa na umaskini.

Nae Zuhura Omar Mattar, alisema ni wakati sasa kwa kamati ya hifadhi ya Mazingira Mtambwe na Serikali zitaweka mikakati madubuti ya ulinzi suala la uharibifu wa mazingira utapungua na kuondoka kabisa.

“Leo hapa Kamati inakamata watu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, lakini siku ya tatu unawakuta nje, serikali ikiweka nguvu basi itakua funzo kwa wengine watakaoharibu mazingira,”alisema.

kwa upande wake Khamis Ali Said, alisema uharibifu wa mazingira unatokana na ukataji wa miti upo kwa asilimia 70 hadi 80,kitu ambacho kimeanza kuwatia hofu na tayari baadhi ya maeneo ya kilimo yameanza kuingia maji chumvi.

Aidha alisema katika kisiwa cha Pemba, ukiondosha msitu wangezi msitu uliobakia ni Mtambwe Kusini, kitu ambacho vikosi vya SMZ na wananchi wa shehia mbali mbali wanautegemea kwa kupata kuni za kupikia.

Katibu wa kamati ya hifadhi ya Mazingira Mtambwe Kusini, Said Hamad Omar alisema mtambwe ilikua na mstu mkubwa, ambao sasa umeshatoweka na kubakia janga, hali iliyopelekea kukosekana kwa mvua na kutokea kwa upepo na kupeleka joto kali.

Afisa elimu ya mazingira kutoka kamati ya hifadhi ya Mazingira Mtambwe Kusini Zuwena Omar Ali, alisema mikakati ni kuendelea kushajihisha jamii na wadau mbali mbali, kupanda miti kwa wingi katika maeneo ya baharini na juu, ili kurudisha haiba ya kijani ya kisiwa cha Pemba.

“Sisi kama kamati tumeshapanda miti zaidi ya 40000 katika maeneo mbali mbali, ikiwemo miti ya juu kama vile miembe, mikungu, minazi, mifenesi na miti mengine pamoja na miti ya Pwani mikandaa (mikoko),”alisema.

Aidha alisema wakati sasa wa kutumia majiko sanifu ya kuni moja, umeme na Gesi katika kupikia, ili kupunguza matumizi mabaya ya miti kukatwa kupigwa tanu za mkaa.

Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba Mwalim Khamis Mwalim, anasema mikakati mbali mbali inachukuliwa ikiwemo kufanywa ufutaliaji kwa kushirikiana na kamati ya hifadhi ya msitu, kwa kuyanya doria za mara kwa mara.

Mkuu wa Idara ya Misitu Pemba Massoud Bakar Massoud, alisema suala la uharibifu wa mazingira lipo, katika kisiwa cha Pemba msitu uliobakia ni Mtambwe Kusini pekee.

Uharibifu huo umechangiwa kutokana na kuongezeka kwa shuhuli za mahitaji ya wananchi, kutoka Chake Chake na Wete kuhitaji kuni, mkaa, miti kwa ajili ya majengo.

hifadhi ya msitu inaukubwa wa hekta 2977 kwa msitu wa juu na baharini, asilimia 70 wanaokata ni wakaazi wa Mtambwe na asilimia 30 kutoka shehia jirani, ikiwemo ndagoni, Mchanga mdogo, Jojo na Micheweni.

MWISHO