Sunday, December 29

Umbali mrefu wanaotembea wanafunzi wa skuli ya msingi Makongeni yatwajwa moja ya sababu ya utoro .

NA ABDI SULEIMAN.

IMEELEZWA kuwa suala la utoro kwa wanafunzi wa skuli ya msingi Makongeni Shehia ya Mtambwe Kusini Wilaya ya Wete, inatokana na umbali mrefu wanaotembea wanafunzi kufuata huduma ya elimu.

Hayo yameelezwa na wazazi, walezi, walimu na viongozi wa kamati ya skuli hiyo, wakati walipokua wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati Tofauti.

Walisema wapo watoto wanatembea zaidi ya kilomita sita (km6) kufuata huduma ya elimu kutoka kijijini kwao, hali inayoepelekea baadhi yao kukubwa na matendo mabovu wanapokuwa njiani

Omar Khamis Haji Mkaazi wa Kivumoni Mtembwe Kusini, alisema wanajitahidi kuhimiza watoto kwende kufuata elimu, lakini umbali wa kijiji chao na iliko skuli inachangia kwa akiasi kikubwa suala la utoro.

“Sisi huku Kivumoni na kufika skuli ni kilomita 6, wapo watoto wadogo wanafuatana na kaka zao, kwa kupitia barabarani wapo wengine wanapita porini mitihani mbali mbali inawakumba huko”alisema.

Alisema baadhi ya wakati watoto wanashindwa kwenda skuli husuna mvua inaponyesha, hulazimika kubakia nyumba kwa kuhofia kurowesha mabuku na wao wenywe.

Naye Mariyam Hassan Kai mkaazi wa Mtambwe Kinazini, alisema watoto wanatembea kilomita nne (km4) hadi kufika Makongeni, wakati mwengine wanashindwa kufika kutokana na kuumwa njiani ikizingatiwa baadhi yao ni wadarasa la kwanza.

“Kwa kweli huu ni mtihani kwetu ila tunajitahidi kuwahamasisha watoto wetu kufuata elimu, japo kua skuli iko mbali na watoto wetu,”alisema.

Kwa Upande wake Hajra Yussuf Ali, Mkaazi wa kijiji cha Mitambuuni Mtambwe Kuisini, alisema suala la umbali wa skuli iliko linawafanya watoto kushindwa kwenda kwani wanapita katika misitu ili kufika skuli.

Aidha aliiyomba serikali kuwajengea skuli nyengine ya msingi iliyo karibu na vijiji, ambavyo watoto wao hutembea masafa marefu kufuata huduma ya elimu.

Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Makongeni Shehia ya Mtambwe Kusini, Juma Said Salum alisema suala la utoro kwa wanafunzi lipo na linatokana na watoto kutembea masafa marefu kufuata huduma hiyo ya elimu.

Alisema wanafunzi wanaosoma skuli hiyo wapo naotoka makongeni wenye, wengine vijiji vya jirani ikiwemo Jirambe, Funika, Kinyuji, Mavuiko, Mitambuuni KM3, Kinazini KM 4 na Kivumoni KM6.

“Hapa matukio mabaya yalishawakumba watoto wanaotoka kijiji cha Mitambuuni tena darasa la kwanza, ili wafike kwa haraka wanalazimika kupita msituni, yote hii ni kutokana na skuli kuwa mbali na watoto wanataka kusoma,”alisema.

Hata hivyo aliyomba serikali kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa skuli ya madarasa sita, ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi na wahisani, ambayo itaweza kuwasaidia wanafunzi wanaotembea masafa marefu kufuata huduma hiyo ikiwemo kijiji cha kivumoni, Mitambuuni na Kinazini.

Mwenyekiti wa kamati ya skuli Mtambwe Kusini Said Nassor Hakim, alikiri kuwepo kwa utoro skulini hapo unaochangiwa na umbali wa skuli ilipo na wanafunzi wakotoka.

Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mwalimu Mohamed Nassor Salum, alisema Wizara itahakikisha inalimaliza jenge la skuli lililojengwa eneo la Kivumoni ili mwaka 2024 wanafunzi waweze kusoma skulini hapo.

Alisema kumalizika na kuzinduliwa kwa jengo hilo litaweza kuondosha tatizo la kufuata huduma ya elimu masafa marefu, kwa watoto wa darasa la kwanza, darasa la pili na tatu.

Mkuu wa Wilaya ya Wete Dk.Hamad Omar Bakar, alisema serikali ya Wilaya inatambua changamoto wanazozipata wanafunzi wa Mtambwe Kusini kufuata huduma ya elimu umbali wa Kilomita sita kutoka kijiji cha Kivumoni.

Hata hivyo alisema changamoto hiyo itamalizika baada ya wanafunzi kuanza kusoma katika mabanda mabya yanayojengwa katika eneo la kivumoni.

MWISHO