Monday, December 30

UNDP itaendelea kufanya kazi na asasi za kiraia Kisiwani Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Matifa (UNDP), limesema litaendelea kufanya kazi na asasi za kiraia Kisiwani Pemba, katika kuhakikisha amani na utulivu inaendelea kudumu ndani ya kisiwa hicho.

Hayo yameelezwa na mwakilishi kutoka UNDP Zanzibar Gamaliel Sunu, wakati akizungumza na vijana wa Wilaya ya Micheweni, katika utekelezaji wa mradi wa Dumisha Amani unaotekelezwa na CYD kwa Ufadhili wa UNDP.

Alisema kituo cha Majadiliano kwa Vijana Zanzibar (CYD) imekua ni taasisi ya mfano, katika kuhakikisha vijana wanakua mstari wambele katika kudumisha amani na utulivu nchini.

Alisema UNDP itaweza kufikia malengo endelevu iliyojiwekea katika mradi huu, iwapo vijana wataweza kuifikisha elimu ya umuhimu wa amani kwa vijana wenzao mitaani na kuona Pemba inaendelea kua kisiwa cha amani muda wote.

“kila kitu kinataratibu, miongozo, mikakati na malengo yake iliyojiwekea, hata sisi pia tuna malengo yetu na katika mradi huu wa Dumisha Amani, ilimu ikifika kwa wengi basi malengo yatafikiwa,”alisema.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, amesema taasisi ya CYD imefanya mambo makubwa katika Wilaya ya Micheweni kupitia miradi yake mbali mbali inayotekeleza hasa katika kuwaweka vijana pamoja.

Alisema mradi wa kwanza wa Amani Mipakani umeweza kusaidia vijana kuwa walinzi wa zuri wa mipaka yao, kwa kuhakikisha wageni hawing ovyo ovyo ndani ya Wilaya hiyo.

Alisema mradi wa Dumisha Amani ambao pia unatekelezwa na CYD, tayari imeshawakutanisha vijana mbali mbali, ili kuweza kuhubiri suala la amani ndani ya jamii zao, kwa lengo la kuona Wilaya ya Micheweni inaendelea kubakia salama muda wote.

“Vijana ndio kundi kubwa ambalo linatakia kudumisha amani muda wote, sasa ni wakati wa kwenda shumba mjini kuwapatia elimu vijana wenzenu wa kule, ili kuondokana na mihemko yao kwani sote tunatambua bila ya amani hakuna lolote la maendeleo litakalofanyika,”alisema.

Hata hivyo aliwataka vijana hao kuhakikisha elimu waliopatiwa wanaifikisha kwa vijana wenzao, ili jamii iliyokubwa iweze kunafaika.

Mwakilishi wa UNDP kutoka Dodoma Veronica Fubile, alipongeza Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba, kwa kuona bado mvijana wanaendelea kuishi katika maisha ya amani na utulivu.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Micheweni Sheha Mpemba Faki, aliwataka vijana kutokukubali kushawishiwa na wanasiasa, kwani wao ndio kundi kubwa linalopaswa kusimama kitedete kuhakikisha amani inadumu.

Nae mwakilishi Kutoka Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Zadida Abdalla Rashidi, alipongeza CYD kwa kuendelea kushirikiana na vijana, kwani vijana wanafursa nyingi katika jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa CYD Hashim Pondeza, aliwataka vijana kushirikiana katika suala zima la maendeleo, kwa kuweka pembeni tafauti zao za kisiasa, katika kuhakikisha amani na utulivu inaendelea kuwepo zanzibar.

MWISHO