Thursday, November 14

Wawi wanatakiwa kuwa kitu kimoja katika suala la kulinda amani na kuibua miradi ya maendeleo.

 

 

NA ABDI SULEIMAN.

WANANCHI wa Shehia ya Wara jimbo la Wawi Wilaya ya Chake Chake, wametakiwa kuutumia vyema mfumo wa pima kadi ya jamii, kwa kuhakikisha wanakua kitu kimoja katika suala zima la kulinda, kuibua na kuisimamia miradi ya maendeleo iliyopo kwenye shehia yao.

Hayo yameelezwa na msaidizi mratib wa mradi wa Ujenzi wa Amani na Maendeleo kwa Vijana na wanawake, Hidaya Maulidi Dude, mradi unaotekelezwa na NCA,ZANZIC,ELETR-ND na kufadhiliwa na Ubalozi wa Norway, huko katika skuli ya maandalizi machomanne.

Alisema lengo la pima kadi ya jamii ni kujenga jamii kuwa kitu kimoja, kufanya kazi zao kwa umoja bila ya kujali rangi kabila wala dini.

Hidaya alisema wananchi wa shehia ya Wara, wanapaswa kufuatilia na kuibua, kuwa walinzi wa miradi ya maendeleo inayofikishwa katika shehia yao, ili iweze kudumu kwa muda mrefu na sio kuwa chanzo cha kuharibu.

“Wara imekua shehia ya kwanza katika suala la Pima kadi ya Jamii, itakayoweza kuwasaidia katika kuwawezesha watu katika shuhuli zao za kiuchumi, ufugaji na wa kuku wa kisasa na kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi,”alisema.

Nae Mkufunzi wa walimu wa walimu kwenye shehia, Piusi William Ngirwa kutoka NCA Morogoro, alisema wananchi ndio wanaopaswa kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo kwenye shehia kwani ndio wanufaika wa kubwa wa miradi hiyo.

Akizungumzia suala la amani, alisema NCA imekua mstari wa mbele kushajihisha amani nchini, kwani inapopotea waathirika wakubwa ni wanawake na watoto, hivyo akinamama kutokukubali kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.

“Dunia imebadilika na mambo mengi yanatokea tu hivi sasa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, umasikini unaongezeka mikakati mbali mbali inapaswa kuchukuliwa kuhakikisha jamii inakua imara,”alisema.

Nae TOT Mwadini Juma Ali, alisema pima kadi ya jamii ni nyezo madhubuti ya upimaji wa maendeleo katika jamii, ikizingatiwa lengo lake ni kuchachua maendeleo katika jamii.

Kwa upande wake TOT Seifa Khamis Salim kutoka Tumbe, alisema vijana wanawajibu mkubwa wakulinda jamii yao, pia ndio walinzi na watunzaji wa kubwa miundombinu ya shehia yao.

“Pima Kadi inaonyesha umuhimu wa vijana katika jamii, pamoja na ushiriki wao katika shuhuli za miradi ya maendeleo iliyomo katika shehia zao,”alisema.

Mmoja ya wananchi wa shehia ya Wara Abdi Ali Mussa, aliwataka wazazi wenzake kuhakikisha wanakuwa waangalifu na wafuatiliaji wakubwa wa watoto wao, kwani watoto wadogo wamekuwa wakijiingiza kwa kiasi kikubwa katika suala la uvutaji wa sigara.

MWISHO