Thursday, November 14

Wadau ZEEA  watoa maoni juu ya rasimu ya muongozo wa kuwawezesha wananchi kupata mikopo

NA ABDI SULEIMAN.

WADAU wa mfuko wa 10%(4.4.2) unaotekelezwa na wakala wa uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), wamesema serikali inania nzuri ya kuwasaidia vijana, hivyo mfuko huo unapaswa kuangalia njia ya kusaidia mtu mmoja mmoja, ili kuweza kurudisha fedha wanazokopa kwa wakati muwafaka kuliko kikundi.

Wamesema baada ya fedha kuingia katika kikundi wajumbe wengi wanabadilika kimawazo, badala yake fedha hizo hutumiwa kwa shuhuli nyengine tafauti na mtu mmoja mmoja anapokopa.

Wadau hao waliyaeleza hayo, wakati wa kutoa maoni juu ya rasimu ya muongozo wa kuwawezesha wananchi kupata mikopo kupitia asilimia 10 ya Makusanyo ya mapato ya ndani ya serikali za Mitaa, chini ya mfuko wa ZEEA uliopo Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Pemba.

Mwakilishi kutoka Idara ya Maendeleo ya Vijana Pemba Hafidhi Rajab, rasimu hiyo inapaswa kufikiria upya suala la kumsaidia mtu mmoja mmoja, pamoja na kulengeza sifa za wakopajia kwa kikundi.

“Hebu angalia hapa vikundi vingi vinamikopo kutoka benk nyengine, sasa hapa ukisema mkopaji asiwe na mkopo kutoka benk nyengine itakua kikundi kinakosa haki zake, wakati wanarudisha fedha kwa wakati,”alisema.

Alisema kuna baadhi ya vikundi vimekopa fedha za UVIKO 19 na vinasuasua kurudisha fedha walizotakiwa, mpaka wamefika kufuatiliwa kutokana na fedha hizo kutumika vyengine na kukosa usimamizi mzuri.

Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Hamada Mbwana Shehe, alipendekeza eneo litakalotolewa fomu na malipo yanapaswa kulipwa hapo hapo, kwani fedha sio za Halmashauri au mabaraza ya miji wala serikali za mitaa.

Kwa upande wake Fatma Ali Kombo, kutoka baraza la mji Wete,  alisema upande wakikundi cha watu wenye ulemavu wanapaswa kuwa wote au japo mtu mmoja tu kuwa sio mwenye ulemavu ambaye atakua anasimamia kikundi kizima.

“Unajua unaweza kusema kikindi cha watu wenye ulemavu, ika kikundi kizima wote uwanaulemavu wa uwoni, sasa hapo tutafanya vipi, au kuwepo mtu mmoja anaeona vizuri ikawa msimamizi wao”alisema.

Kaimu afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji Hamad Rashid Khamis, aliwashukuru wadau hao kwa maoni yao walioyatoa, kwani wao ni muhimu katika kuhakikisha Rasimu hiyo inafanikiwa na kwendana na wakati.

Alisema hakuna sababu ya kuficha taarifa inayohitajika, kwani kila jambo linakwenda kulingana na mipango iliyopangwa na kukamilika, ikizingatiwa lengo la serikali ni kuwapatia mikopo vijana.

Alisema lengo la mfuko huo ni kuwapatia mikopo Vijana, wanawake, watu wenye ulemavu, ikizingatiwa Vijana na Wanawake ndio kundi kumba ambalo linahitaji kusaidiwa kwa asilimia kubwa.

Naye kaimu mtaribu ZEEA Pemba Haji Mohamed Haji, alisema lengo ni kujadili rasimu ya mfuko wa 4.4.2 kwa lengo la kuwasaidia vikundi vya vijana, wanawake na walemavu.

Akiwasilisha Rasmi huyi Kaimu Mkurugenzi idara ya mitaji na mikopo, wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar Kassim Haji Mrisho, alisema suala la kuwawezesha wananchi kiuchumi ni moja ya kipaombele cha serikali ya awamu ya nane katika kwuasaidia vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu.

MWISHO