Thursday, November 14

WANAWAKE wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi wametakiwa kuelewa mbinu sahihi za kufanya ushawishi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar -SUZA, Dkt. Salum Suleiman Ali, akizungumza wakati wa mafunzo WASHIRIKI: Washiriki wa mafunzo maalum kwa wanawake kutoka vyamba mbalimbali vya siasa Pemba kuwajengea uwezo kutambua haki zao na kushiriki katika mchakato wa kugombea nafasi za uongozi kwenye vyombo vya maamuzi wakiendelea na mafunzo.

 

WANAWAKE wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi wametakiwa kuelewa mbinu sahihi za kufanya ushawishi katika siasa na uongozi ili kukabiliana na vikwazo vinavyoweza kuwakwaza kushika nafasi hizo katika ngazi mbalimbali.

Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar -SUZA, Dkt. Salum Suleiman Ali, wakati wa mafunzo maalum kwa wanawake kutoka vyamba mbalimbali vya siasa Pemba kuwajengea uwezo kutambua haki zao na kushiriki katika mchakato wa kugombea nafasi za uongozi kwenye vyombo vya maamuzi.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Tanzania, alieleza suala la kushiriki kugombea nafasi za uongozi ni mchakato endelevu unaohitaji maadalizi ya muda mrefu ili kujenga Imani kwa jamii juu ya uwezo wa kiongozi katika kutetea na kusimamia changamoto zao.

Alifahamisha ili wanawake waweze kufanikiwa kushika nafasi za kisiasa na uongozi katika ngazi mbalimbali uwezo wa kujenga hoja na kuibua changamoto zinazowakabili wananchi ni mbinu muhimu katika kuongeza ushawishi wao kwa jamii.

Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Dkt. Salum aliwahimiza wanawake kuanza kutumia fursa ya vyombo vya habari kuweka ajenda ya kuisemea jamii matatizo yao ili kusaidia kupata suluhisho.

“Lazima tuvitumie vyombo vya habari kwaajili ya kufanya ushawishi wa mabadiliko kwa kutengeneza ujumbe na maudhui yanayolenga kuwasemea wananchi matatizo yanayowakabili hii itatusaidia kujijenga kisiasa na kuaminika kwa umma kuliko kusubiri uchaguzi umefika ndipo tuanze kujitokeza kutaka kuwasemea wananchi,” alifahamisha mkufunzi huyo.

Aliongeza TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake katika masuala ya uongozi (SWIL) imechapisha muongozo maalum ambao unatoa mwelekeo kwa wanawake kutambua mbinu za kutumia kushinda nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali.

Alieleza, “TAMWA ZNZ imeandaa kitini maalum kwaajili ya kutoa muongozo kwa wanawake wagombea watarajiwa kujijengea uwezo wa kushiriki katika mchakato wa kugombea nafasi za kisiasa na uongozi pamoja na michakato yote ya kidemokrasia.”

Mapema mratibu wa TAMWA ZNZ, Fat-hiya Mussa Said alieleza mafunzo yamewashirikisha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa pamoja na viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati kwaajili ya kuwaunganisha na kubadilishana uzoefu kuelekea kugombea nafasi mabilmbali za uongozi.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa wanawake kwaajili ya kuwajengea ujasiri na uthubutu wa kuwa tayari kushiriki kugombea na kudai haki za wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Alieleza, “mafunzo haya yanalenga kuwawezesha wanawake kuwa na ujasiri na uwezo wa kusimama kutetea haki za msingi za wanawake kwenye masuala ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kugombea uongozi kwenye chaguzi mbalimbali za kidemokrasia.”

Kwa upande wake Saghira Moh’d Khalfan mmoja wa washiriki hao alishukuru TAMWA ZNZ kwa kuandaa muongozo huo maalum kwaajili ya kuwaonesha njia wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi kwani utawasaidia kwenye uchaguzi mkuu 2025 kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikiwakatisha kufikia malengo yao kwenye uongozi.

TAMWA Zanzibar kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi SWILPROJECT unaotekelezwa kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway inasaidia kufanikisha utekelezaji wa Lengo namba Tano la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohimiza kuwepo kwa Usawa wa Kijinsia kwa Wanawake na wasichana.

Imetolewa na 

Kitengo cha Habari na mawasiliano,

TAMWA Zanzibar

11, Julai 2023.