Sunday, November 24

Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kujenga ukuta Kuunusuru mji wa karne ya 11 kuvamiwa na maji ya bahari

NA ABDI SULEIMAN.

MRATIBU wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba Khamis Ali Juma, amesema mikakati mbali mbali inaendelea kuchukuliwa na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, kuhakikisha eneo la Mkumbuu haliendelei  kuvamiwa na maji ya chumvi, kwa kujengwa ukuta wenye urefu wa mita 500.

Alisema ukuta huo utaweza kuzuwia mawimbi ya maji ya bahari kutokuendelea kuumega mji wa karne ya 11, ambao kwa sasa ndio uliobakia baada ya mji wa karne ya Kwanza (1) kuwa katikati ya maji ya chumvi na mji wa karne ya tisa (9) nao kuliwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko katika majengo ya kihistria Mkumbuu Wilaya ya Chake Chake, alisema ujenzi wa ukuta huo utaambatana na ukarabatari wa maeneo ya kihistoria na sehemu za huduma,  mradi wote ukigharimu Bilioni 2, 2,407,316,675.

“Wizara tayari imeshachukua hatua ya kuliboresha eneo la Mkumbuu, ambalo linaonekana lipo hatarini kutowekwa, kwanza kujenga ukuta mkubwa usio Pungua mita mia tano 500, wa kuzuwia mawimbi ya bahari yasiendelee kumega eneo la mkumbuu,”alisema.

Alisema kwa sasa mskiti wa karne 11 upo mbioni kutoweka, ambapo lengo ni kuuhuisha mji wa asili na ukawa katika haiba yake, ambao ni kidhibiti kikubwa kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba na ndio penye chimbuko la historia ya Pemba.

“Ni muda mrefu sana tokea mji wa karne ya kwanza ambao sasa upo chini ya bahari, kumegwa na maji ya bahari, sasa haipendezi na mji huu uliobakia kumengwa histora yetu tutakua tumeiweka wapi,”alisema.

“Kwa sasa mtu akifika ataona mji wa karibu karne ya 9 umebakia ufukweni, ukifika utaona hodhi la kuhifadhia maji tu ndio kwa sasa lipo kwenye mchanga wa bahari, ukuta huo utazuwa maji kuendelea kuathiri mji uliopo,”alisema.

Akizungumzia athari zake watakazipata, alisema ni kukosekana kwa maeneo ya kihistoriya na yatapotea kabisa, watalii watashindwa kufika kufahamu historia ya wapemba na serikali kukosa mapato yake kupitia maeneo hayo.

Mkuu huyo wa idara alisema lengo lao ni kuhifadhi, kulinda kwa ajili ya vizazi vinavyokuja kujua historia, pamoja na kufahamika kwa historia ya washiradhi, iwapo mabaki ya mji wa karne ya 11 utaendelea kubakia.

Kwa upande wake Afisa Utalii Kutoka Wizara hiyo Khalidi Kombo Khamis, alisema athari za mabadiliko ya Tabia nchi yanaendelea kuathiri baadhi ya vitu vya kale, ikiwemo historia ya majengo ya Mkumbuu.

Alisema kupotea kwa historia hiyo ni pigo kubwa kwa Wizara katika kutunza kwani ndio yenye jukumu la kutunza majengo hayo, ambayo kwa sasa yamekua ni kivutio kikubwa cha watalii.

Alisema tayari Wizara imeshamkabidhi mkandarasi ujenzi wa ukuta huo, huku pamoja na kurudisha haiba ya mji wa mkumbuu ambao umekua kivutia cha watalii.

MWISHO