Saturday, December 28

Barabara Mleteni bado changamoto.

NA ABDI SULEIMAN

WANANCHI wa Kijiji cha Mleteni shehia ya Kisiwani kwa binti Abeid Wilaya ya Wete, wamesema bado suala la barabara ya kijijini kwao linaendelea kuwamuzia kichwa hususana kipindi cha mvua inaponyesha.

Wamesema kipindi hiki hakuna usafiri wa aina yoyote unaofika kijijini kwao, hali inayopelekea huduma muhimu za kijamii kusikoza kwa kipindi hicho.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wamesema tayari walifikisha kiliochao hicho kwa viongozi mbali mbali wa serikali bado hadi sasa hakuna juhudi iliyofanyika.

Mohamed Said Mkaazi wa Mleteni, alisema ufumbuzi wa maendeleo sehemu yoyote duniania inatokana na uwepo wa barabara ya kisasa, jambo ambalo mleteni halipo na itendelea kuwa mwisho kufikiwa na maendeleo hayo.

Alisema hakuna kipindi hata kimoja ikiwa jua au mvua, gari kufika kijijini kwao kutokana na barabara yao kuwa mbovu kupitia kiasi, licha ya kilio chao kukifikisha kwa viongozi wa juu.

“Mimi binafsi tayari nimeshamueleza Rais Mwenyewe na kutoa agizo kwa wasaidizi wake, lakini mpaka leo hakuna barabara iliojengwa wala kuona hatua zilizochukuliwa,”alisema.

Nae Bimariyam Hassan Bakar (56) alisema kipindi cha mvua hulazimika kuwaondosha watoto wao wajawazito kijiji hapo na kwenda kuwaweka sehemu nyengine mpaka watakapojifungua kutokana na shida ya barabara inavokuwa.

Alisema ubovu wa barabara inapelekea walimu kuchelewa kufika skuli, pamoja na kukosa mahitaji yao muhimu ya kijamii ya siku, sambamba na kwenda hospitali kufuata matibabu.

“Tayari tunakesi kadhaa zimeshatokea hapa kijijini, wazazi kujifungulia njiani, gari kufika kumchukua mzazi shilingi 40,000, ukitizama hali za maisha ni masikini, barabara ikitengenezwa basi ghamara,”alisema.

Kwa upande wake Nunu Shaibu Suleiman, alisema kilio chao kikubwa wananchi wa mleteni ni suala la barabara, kipindi cha mvua hakuna kinachoingia wala kutoka kujijini kwao.

Alisema wafanyabiashara hulazimika kusitisha biashara zao na kwenda kupata hasara, kipindi ambacho mvua inanyesha kwa kushindwa kwenda sokoni.

Nae mwalimu wa skuli ya Maandalizi na Msingi Mleteni Hadija Hamad Ali, alisema kipindi chamvua ni shida kufika skuli kufundisha watoto, hata bodaboda hazifiki na nauli shilingi elfu 2,000 kwenda na kurudi 4,000.

Alisema muda wakusafirisha vifaa ni shida kubwa kufikisha kutokana na changamoto hiyo, huku akiiyomba taasisi husika kuhakikisha wanaifanyia matengenezo barabara hiyo.

Naibu sheha wa shehia ya Kisiwani kwa Binti Abeid Bahati Juma Mtwana, alisema juhudi zinachukuliwa kuhakikisha barabara hiyo inatengenezwa na kupitika.

Alisema barabara hiyo ni moja ya barabara za ndani ambazo zinajengwa na serikali, huku akiwataka wananchi kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki serikali inafuatilia ujenzi wake.

Mkuu wa Wilaya ya Wete Dkt.Hamad Bakar Omar, alisema wananchi wasiwe na wasiwasi kwani serikali inafahamu changamoto hiyo ya barabara.

Alisema wananchi walikua na vipaombele vyao na tayari vya kwanza vimeshatekelezeka, ikiwemo umeme, skuli na maji, hivyo barabra nayo iko katika kipambole kinachofuata.

Afisa mdhamini Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema barabara ya Mleteni tayari iko katika mradi wa ujenzi wa barabara za ndani, ambapo mkandarasi tayari yupo ndani ya kisiwa cha Pemba.

Alisema kwa sasa tayari kampuni ya IRIS imeshaanza kusafisha barabara mbali mbali za ndani, ikiwemo Mchangamdogo-Mazambarau Takao KM6, Mapofu-Tumbe bandarini KM12, Finya- Kicha KM8.6, Micheweni-kiuyu Maziwangombe KM7.5, Konde Makangale KM12, Micheweni-Shumbamjini Bandarini KM2, Penjewani Mjini kiuyu KM2.2 na Pembeni Pandani KM3.2.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa wastahamilivu, kwani serikali inatambua kila kitu kwao na barabara itajengwa kwa kiwango cha lami.

MWISHO