Saturday, December 28

 Fedha za mfuko wa jimbo  kuweka uwazi wa matumizi yake  ili kuondosha migogoro 

NA ABDI SULEIMAN.

WAJUMBE wa Kamati ya Maendeleo ya skuli ya Maandalizi na Msingi Tundauwa Wilaya ya Chake Chake, wamewataka wahasibu wanaosimamia fedha za mfuko wa jimbo za Mwakilishi na Mbunge, kuweka uwazi wa matumizi ya fedha hizo wakati wanapozipeleka katika miradi ya jamii.

Wamesema uwazi huo utasaidia kujulikana na matumizi halisi ya fedha hizo, na kuondosha migogoro na mabishano pale matumizi yanapokua sio sahihi.

Wajumbe wa kamati hiyo waliyaeleza hayo, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayojengwa kupitia fedha za mfuko wa jimbo na mwakilishi wa jimbo la Chonga Wilaya ya Chake Chake.

Mwalimu Juma Maalim Khatib, alisema wakati wautekelezaji wa miradi, vizuri mambo ya fedha za mfuko huo zinapopelekwa katika miradi kuwekwa wazi juu ya matumizi yake na sio kupelekea vutu na ujenzi kuanza.

“Sisi hapa Tundauwa tunajenga jengo la vyumba vitano, wananchi na kamati tumenga fondesheni ya vyumba viwili, fedha za mfuko wa jimbo zikashindwa kumaliza ujenzi wa fondeshieni iliyobakia na hatujuwi kilichotumika,”alisema.

Alisema hadi sasa wameshindwa kujua kiasi gani cha fedha kilichotumika, kwani wanapoulizia wanapigwa dandana mara Milioni tano, wakati mwengine Milioni saba na kushindwa kujuwa uwazi wa matumizi ya fedha.

Nae mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Mwalimu Suleiman Said Salum, alisema lengo la wananchi kuamua kujenga vyumba hivyo vitano vya nyongeza ni kutaka watoto wanapomaliza maandalizi na msingi kuingia darasa la pili hapo hapo na sio kutembea masafa marefu.

Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma hadi darasa la saba skulini hapo, hivyo viongozi wanaosimamia fedha mifuko ya jimbo, wanapaswa kuwa waminifu ili miradi inayojengwa iweze kuwanufaisha wananchi ipasavyo.

“Vizuri ujenzi huu wafondesheni wangeachiwa wananchi wenyewe wangeimaliza, kuliko hivi walivyokwenda kujenga sisi tumejenga tulivyokua tunataka wao wamekuja kutuharibia na fedha hatukuweza kujuwa matumizi yake,”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Chonga Suleiman Abrahman Kombo, alitawaka wananchi wa kijiji cha Tundauwa kuridhika na maendeleo wanayopatiwa kupitia mwakilishi wao.

Aidha nae Mwkailishi wa jimbo hilo Suleiman Massoud Makame, alisema wananchi wamepiga hatua kuhakikisha changamoto za watoto kwenda skuli kilindi na kurudi zinaondoka kabisa.

Alisema atajitahidi skuli hiyo inamalizika kwa wakati muwafaka na watoto wanasoma hapo hapo, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na kuwa wamoja katika masuala ya maendeleo.

MWISHO