Sunday, December 29

Kisiwani kwa binti Abeid walia na huduma ya kina mama wanapotaka kujifungua.

NA ABDI SULEIMAN.

WANANCHI wa shehia ya Kisiwani kwa Binti Abeid Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamesema umefika wakati kwa Serikali kukiongezea ukubwa kituo chao cha afya, ili huduma zote muhimu ziweze kupatikana kituoni hapo.

Wamesema kwa sasa akina mama wajawazito wanalazimika kujifungulia katika hospitali ya Wete au Chake Chake, kutokana na kituo cha afya chao kutokuwa na uwezo huo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafauti, wakati wa ziara ya kutembelea vijijini, wamesema wanapohitaji kujifungulia hulazimika kwenda huko, lakini huduma nyengine zote za mama na mtoto zinapatikana kituoni hapo.

Mmoja ya wananchi hao Time Ali Sultani mkaazi wa Shangafu, alisema watoto wao wanapokaribia kujifungua huwa na gamu la kuwapeleka Chake Chake au Wete, kupata huduma kwa ajili ya kupata huduma hizo.

“Serikali kutuangalia na sisi huduma nyingi tunapatiwa katika kituo chetu, ila hii ya kujifungulia ndio shuhuli lazima tugharamike, gari ni shilingi elfu 40,000/=,”alisema.

Nae Siti Abdalla Said mkaazi wa kijiji cha Mashuga, alisema umbali wa kituo cha afya unapelekea baadhi ya huduma kupelekea huko huko kijiji kwao, zikiwemo huduma za chanjo kwa watoto na wamama wajawazito.

“Tunakotoka na kukifuata kituo cha afya ni mbali sana kwa bodaboda ni shilingi elfu 2,000 kwenda na kurudi 2,000, pesa wenyewe mtihani kuipata, vizuri serikali kutufikiria na sisi tena,”alisema.

Hata hivyo aliyomba serikali kuhakikisha madaktari wa kituo cha afya Kisiwani kwa Binti Abeid, wanapatiwa nyumba ya kuishi karibu na kituo hicho ili waweze kutoa huduma muda wote.

“Kipindi cha mvua kinapofika tunaanza kuwa na gamu juu ya upatikanaji wa huduma, ingekua madaktari wapo hapa hapa afadhali sana, huduma tuzifuate Chake Chake au Wete,”alisema.

Kwa upande wake Masunde Malik Seif mkaazi wa kijiji cha Mashuga, alipongeza Serikali katika utoaji wa huduma za afya, kwani baadhi ya huduma ikiwemo za chanjo wanafikishiwa majumbani muda wa watoto kupata chanjo unapofika.

Naibu sheha wa shehia ya Kisiwani kwa Binti Abeid Bahati Juma Mtwana, alisema huduma za mama na mtoto zinapatikana vizuri katika shehia yao, huku wananchi wa vijiji vya Tondooni, Mleteni  na Mashuga huduma hupelekewa huko huko.

Alisema changamoto iliyopo ni huduma za kujifungulia akinamama hulazimika kuzifuata Chake Chake au Wete, hususan muda wa usiku unapofika na kipindi cha mvua kutokana na kukosekana kwa nyumba ya madaktari kituoni hapo.

Kwa upande wake Daktari wa kituo cha afya Kisiwani kwa Binti Abeid Dk.Aminia Hamad Khamis, alisema huduma ziko vizuri na wananchi wameitikia wito vizuri kuwafikisha watoto wao kupata huduma za chanjo pamoja na akinamama.

Alisema chanjo za aina zote zinatolewa kituoni hapo, ikiwemo za watoto, Uviko 19, akinama wajawazito, akinamama wanaotaka kupanga uzazi, na hata wamama wanaokwenda kujua afya zao.

“Kwa siku huduma wamama wajawazito wanafika 15, wanaopeleka watoto kupimwa ikiwa wameshamaliza chanjo wanafikia 15, wamama wanaokwenda kwa ajili ya chanjo wanafikia 20, huduma mbali mbali zinatolewa na sio chanjo tu,”alisema.

Hata hivyo alisema kwa kuwatumia CHV hulazimika kufika katika vijiji vilivyoko mbali na kituo cha afya, lengo ni kuwapatia watoto chanjo zote zinazotolewa na Wizara ya Afya kwa watoto, huku akiwataka wananchi kuendelea kutumia vituo vya afya kwa kuwapatia huduma mbali mbali.

MWISHO