Saturday, December 28

RAIS Dk.Miwnyi ameahidi kusaidia vifaa vya usafiri kwa watoa msaada wa kisheria

NA ABDI SULEIMAN.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuwasaidia vifaa mbali watoa msaada wa kisheria  ili wawe na mazingira mazuri wanapokwenda kuwasaidia wananchi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema watoa msada wa kisheria  wamekua wakifanya kazi kubwa ya kuwasaidia wananchi katika mazingira magumu, huku wakizungukwa na changamoto  mbali mbai ikiwemo usafiri na ofisi za kudumu.

Alieleza kuwa amevutiwa mno na kazi yao hiyo na ndio maana ameahidi kuangalia kila aina ya mazingira ya kuwasaidia vifaa, ikiwemo vyombo vya usafri, ofisi zenye hadhi na mazingira wezeshi ili wafanyw kazi zao ka ufanisi zaidi.

“ Nimevutiwa mno na kazi yao hiyo wanayoifanya licha ya changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo na ndio maana nimeahidi kuangalia kila aina ya mazingira ya kuwasaidia vifaa ikiwemo vyombo vya usafri,ofisi zenye hadhi na mazingira wezeshi ili wafanye kazi zao ka ufanisi zaidi,”alisema

Alisema watoa msada wa kisheria  wamekua wakijitolea na kuwapatia wananchi huduma stahiki kwani  suala hilo sio la Zanzibar peke yake bali la kimataifa na lina historia kubwa

Alisema  kwa upande wa Zanzibar ipo haja ya kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kwa vitendo kama ilivyoelezwa katika katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alifahamisha kwamba licha ya mafanikio yaliopatikana bado lipo jukumu la kuhakikisha wanasimamiwa vizuri watoa msaada wa kisheria ili waweze kutoa huduma kwa mujibu wa sheria na viwango vilivyowekwa

Aidha alisema  watoa msaada wa kisheria wanahitaji kuungwa mkono na kupata ushirikiano wa kutosha kwa watendaji mbali mbali wa Serikali katika kufanikisha kazi zao

Dk. Mwinyi alisema Serikali kupitia Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora itaendelea kushirikiana bega kwa bega na watoa msaada wa kisheria kwa kuhakikisha tuzo zinazotolewa zinakua endelevu katika kupatikana mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao.

Pia alisema SMZ itahakikisha marekebisho  ya msaada wa kisheria yanafanyika kwa haraka na ufanisi ili kukidhi matakwa yanayotakiwa.

“Napenda kuzipongeza taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kwa juhudi wanazozichukua katika kuwafikia wananchi na kuwafahamisha juu ya upatikanaji wa msaada wa kisheria,”alisema.

Sambamba na hayo Dk.Mwinyi alitoa wito kwa kila mtu kutumiza wajibu wake ili kuwepo kwa mazingira bora ya upatikanaji wa msada ili kuzidi kuimarisha kiwango cha utawala bora na misingi ya haki za binaadamu nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, Hanifa Ramadhan Said alisema watoa msaada wa kisheria wanafanya kazi kwa kujitolea na kwa uzalendo kwa huhakikisha wananchi wasio na uwezo wanapatiwa msaada huo kwa kufika kila sehemu.

Mapema akitoa salamu za LSF, Mjumbe wa Bodi ya LSF Jaji Mstaafu Robert Makaramba, alisema uwepo wamazingira wezeshi kwa watoa huduma za msaada wa kisheria  ni pamoja na kuwepo sheria na sera zinazotambua na kuunga mkono usaidia wa kisheria, kutenga rasilimali za kutosha za kifedha za kiufundi kwa ajili ya mafunzo, vifaa, ofisi na huduma nyengine zinazohitajika katika kutoa huduma endelevu kwa jamii.

Alisema takriban miaka 12 sasa LSF imekua ikitekeleza program ya upatikanaji wa haki Tanzania bara na Zanzibar, ambapo wananchi mbali mbali wameweza kupatiwa elimu na huduma ya msaada wakisheria bure, kwa mujibu wa ripoti ya LSF 2022 inaonyesha Upande wa Zanzibar wananchi laki 165,264 wamefikiwa na elimu na elimu ya kisheria, ambapo Wanawake ni 100,,722 wanaume 88,242.

“Huduma za usaidizi wa kisheria zaidi zimewasaidia wanawake kutokana na kuathiriwa na vitendo mbali mbali vya ukiukwaji wa haki zao ikiwemo ukatili kijinsia,”alisema.

Alisema Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria inahitaji nguvu za pamoja kutoka kila sehemu kwa wahusika mbali mbali na kuona haraka zote za msaada wa sheria zinaratibiwa vizuri.

Akisoma risala kwa watoa maaada wa kisheria, Saleh Mussa Alawi alisema mafanikio mengi yamepatikana tangu kuanzishwa kwa mpango huo.

Aliyataja mafanikio hayo ni pamoja na kushirikishwa katika nyanja mbali mbali kwenye taasisi za Serikali na binafsi,jumuiya hizo kupata ruzuku kutoka shirika la LSF, ambazo husaidia kuendesha shughuli za taasisi.

“Mafanikio mengine ni kupunguza migogoro kwa jamii ikiwemo kwa njia ya usuluhishi ikiwemo ardhi,ndoa na talaka,malezi,matunzo ya watoto,madai ya kukopeshana na malalamiko ya kifedha,”alisema.

Mbali na mafanikio hayo watoa msaada hao walisema wamekua wakikabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo kukosa ofisi za kudumu,kupata vitisho,muhali kwa jamii,kukosa usafiri na nauli za kuwasaidia wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Katika risala yake hiyo alisema watoa msaada hao waliomba kuimarisha mashirikiano kwa wahusika wote wa masuala hayo ikiwemo Jeshi la Polisi,Mahakama,DPP pamoja na taasisi binafsi

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “mazingira wezeshi kwa watoa msaada wa kisheria ni daraja la upatikanaji haki”