NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM kuendelea kufanya kazi ya kukijenga chama, ili kuendelea kushika dola.
Alisema kuwa, chama chochote cha siasa kina jukumu la kushika dola, hivyo kuna haja ya kujipanga kikamilifu kuanzia sasa ili kuhakikisha chama cha Mapinduzi CCM kinaendelea kushika dola siku zote.
Akizungumza na wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba, Makamo huyo alisema kuwa, ni vyema kwa wanachama wakafanya kazi ya kukiimarisha chama cha CCM ili kuendelea kushinda katika chaguzi zote zinazofanyika kila baada ya miaka mitano.
“Baada ya kumaliza uchaguzi kwenye chama chetu maana yake sasa, tunatakiwa tufanye kazi ya kujenga chama chetu, nimekua nikihimiza tu kwani natambua kuwa kazi hiyo inafanyika lakini nasisitiza tujipange kuhakikisha tunakiimarisha chama chetu, jambo ambalo litasaidia kushika dola kila siku”, alisema Makamo huyo.
Aidha Dk. Mwinyi aliwataka wanachama hao kuondosha mpasuko na changamoto ndogo ndogo kwenye chama na waendelelee kushikamana ili kuleta ushindi katika chama chao.
Dk. Mwinyi aliwashukuru wanachama hao kwa kumchagua kuwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na kuitaka Ofisi Kuu ya CCM kupanga utaratibu wa kutoa mafunzo ili kila mtendaji ajue majukumu yake katika chama.
“Tuhimize kufanyika vikao vya kikatiba, hatuwezi kufanya kazi bila kukutana, lazima tukutane na taarifa zitolewe na waliohidhuria tuwajue, ili tuone kwamba kama kuna changamoto ziweze kutatuliwa mapema”, alisema Dk Mwinyi.
Aliupongeza Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kupata wanachama wengi wapya, kwani mtaji wa chama chochote ni wanachama wake, hivyo wamefanya kazi kwa vitendo na kwa ufanisi.
Makamo huyo alieleza kuwa, hakuna maendeleo bila ya kuwepo amani, hivyo wailinde amani iliyopo sambamba na kufanya kazi vizuri ili kukijenga chama hicho.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Mohamed Said Mohamed alisema kuwa, wataendelea kuitunza amani iliyopo pamoja na kuongeza wanachama wapya, ili waendelelee kushinda kila ifikapo kipindi cha uchaguzi.
“Tutaendelea kukijenga chama chetu kwa kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza wanachama wapya, ili kuimarisha chama”, alisema.
Aidha alisema kuwa, maagizo yote yaliyotolewa na Makamo Mwenyekiti huyo tayari wanayafanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kuwapa wanachama mafunzo, vitambulisho na kadi.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM alisema kuwa, hali ya siasa katika Mkoa huo ipo vizuri na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kimaendeleo bila ya kujali itikadi zao za vyama.
Alimshukuru Dk Mwinyi kwa kutekeleza vyema Ilani hiyo ya chama kwa kujenga majengo mawili ya vituo vya ujasiriamali, hospitali mbili za Wilaya, ujenzi wa barabara kubwa na barabara za ndani, huduma ya maji safi na salama mjini na vijijini kupitia miradi mbali mbali pamoja na huduma ya umeme, ambazo zimeimarika katika Mkoa wao.
“Kwa kweli Ilani ya chama chetu tumeitekeleza kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wetu, tunampongeza sana Makamo Mwenyekiti wetu Dk. Hussein Mwinyi kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji huu, tunajivunia sana”, alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkuu huyo alieleza kuwa, katika kutekeleza Ilani hiyo, pia Serikali imewawezesha wajasiriamali kwa kuwapa mikopo kwa ajili ya kujiendesha kiuchumi pamoja na kujenga viwanda vitatu vinavyosaidia kuzalisha ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini, jambo ambalo linaleta faraja kutokana na kuimarika kiuchumi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa alisema kuwa, baada ya kupita uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kulikuwa na changamoto zilizokuwa zikiwakwamisha, ingawa kutokana na umoja wao walionao wamezikabili kasoro hizo na kwa sasa hali inakwenda vzuri.
Alisema kuwa, lengo la nchi na chama cha Mapinduzi ni kujenga amani, hivyo aliwaomba wanaCCM kuendelea kudumisha amani na utulivu ili kupata maendeleo endelevu katika nchi.
“Tunakuuomba Makamo Mwenyekiti wetu utujengee Bandari yetu ya Wete ili usafiri uimarike zaidi kwani Mkoa wa Kaskazini Pemba una wasafiri wengi pamoja na wafanyabiashara, hivyo itakapojengwa tunaamini kuwa na uchumi utaimarika zaidi”, alisema Mwenyekiti huyo.
Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto Khamis amewashukuru wanaCCM kwa kumuunga mkono Makamo Mwenyekiti Dk. Hussein katika kutekeleza majukumu yake ya kulitumikia taifa.
“Dk. Hussein Mwinyi amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo ndani ya kipindi kifupi alichokiongoza, hivyo tutaendelea kumuunga mkono ili kuhakikisha anafanikiwa katika shughuli zote za kimaendeleo alizozipanga”, alisema Katibu huyo.
Makamo Mwenyekiti Dk. Hussein Mwinyi katika ziara yake hiyo pia alikagua eneo la Mkoa litakalojengwa kitega uchumi Wete, kukagua maskani ya Mtemani, kukagua eneo la chama lililopo mkabala na hospitali ya Wete, kukagua eneo la chama mkabala na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni pamoja na kukagua eneo lililokusudiwa kujengwa hospitali ya jumuiya ya Wazazi.
MWISHO