Sunday, November 24

Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa kusini Pemba toweni Elimu kwa viongozi wa ngazi mbali mbali

 

HABIBA ZARALI, PEMBA
MAKAMO Mwenyekiti wa chama Cha Mapinduzi (CCM ) ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi amewataka wajumbe wa Halmashauri kuu ya Mkoa wa kusini Pemba kutowa elimu kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ili kila mmoja kuweza kujuwa na kutekeleza majukumu yake ipasavyo .
Alisema viongozi ndio wenye jukumu la kuhakikisha wanatowa elimu ya kukijenga chama na kuleta mafanikio yanayohitajika na sio vyenginevyo.
Kauli hiyo aliitowa katika ukumbi wa umoja ni nguvu Mkoani wakati akizungumza na viongozi wa chama cha Mapinduzi ikiwa ni siku yake ya mwanzo ya kichama  Mkoa wa Kusini Pemba.
Makamo Mwenyekiti alisisitiza viongozi hao kuacha makundi katika chama na badala yake waandikishe wanachama wapya kwani bado Chama cha Mapinduzi kinahitajika kupata wanachama wapya  hasa ukizingatia ndio mtajii wa chama hicho.
Alifahamishwa kuwa jambo jengine litakaloimarisha chama hicho ni kufanyika kwa vikao vya kikatiba kila mara na kujuwa taarifa na baadae ziende katika ngazi za juu ili maamuzi sahihi yaweze kutekelezwa.
“Niwahimize kuwa tunahitaji kupata takwimu sahihi ya idadi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi na ili tuweze kuwapata basi muhakikishe munahakiki daftari la wanachama na kujuwa walioongezeka pamoja na kutowa kadi mpya za kielektroniki ili wanachama wote wawemo kwenye mfumo maalum”,alisema.
Wakati huo huo Makamo Mwenyekiti aliwasisiza wanachama wa Chama cha Mapinduzi kulipa ada ya chama ili kiweze kupata uhai na kuwahimiza kukisimamia chama kwa nguvu zote na kukiwezesha kiuchumi.
“Wakati sasa umefika katika chama chetu kuweza kuwa na uchumi na vitendea kazi vyake vyote ili tuweze kufanya kazi vizuri na watendaji waweze kupata maslahi nitajitahidi kulisimamia hilo lifanikiwe”,alifahamisha.
Akizungumzia utekelezaji wa ilani ya chama Makamo Mwenyekiti huyo alisema kuwa hadi sasa unakwenda vizuri kwani mafanikio ni makubwa  katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya ,miundombinu ya Barabara na maji jambo ambalo ni faraja kubwa katika Serikali ya Chama cha mapinduzi.
Akizungumzia amani na utulivu ambayo ni miongoni mwa ilani ya chama hicho alisema imefanikiwa vyema na kuwataka viongozi wanaosimamia kwenye majukwaa waihubiri amani na umoja kwani ni la msingi wa mafanikio yote.
Mapema akitowa salamu za Mkoa wa kusini Pemba mkuu wa Mkoa huo ambae pia ni mjumbe wa kamati ya Siasa Mkoa huo Matar Zahor Masoud alimpongeza makamo Mwenyekiti huyo kwa hatuwa nzuri iliyofikia ya kukiimarisha kisiwa Cha Pemba.
Alisema kukamilika kwa majengo ya skuli za  ghorofa , maabara za kisasa ajira mbalimbali 971 zikiwemo za walimu zisizipunguwa 500 na huduma ya maji mijini na vijijini hadi kufikia asilimia 85 ni jambo la faraja si kwa wanachama pekee bali ni kwa wananchi wote kwa ujumla.
Alieleza katika sekta ya afya hospitali za Wilaya wakati wowote zitafunguliwa, bara barabara za ndani kuendelea kujengwa na muda wowote kuanza barabara kuu ikiwemo ya Chake Mkoani,ujenzi wa gati ya Mkoani na uwanja wa ndege ambao utajengwa kwa kilomita 2.5 yote yakiwa na lengo la kuimarisha kisiwa cha Pemba.
“Nimpongeze Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa dhamira yake ya kukiimarisha kisiwa cha Pemba inaendelea kwa kishindo kutokana na miradi mbali mbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya mkoa wa kusini Pemba”, alisema.
Hata hivyo nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa kusini Pemba Yussuf Ali Juma akitowa pongezi kwa makamo Mwenyekiti kwa kudumisha amani na utulivu na kuwaunganisha wazanzibari kuwa kitu kimoja bila ya kujali  vyama na itikadi zao.
                 MWISHO.