Jumla ya waombaji 734 wamefanikiwa kujaza na kuzirudisha fomu za maombi ya ruzuku ya mradi wa VIUNGO ambao umelenga kutoa rukuzu kwa wanufaika wake waliosajiliwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Utoaji wa ruzuku hiyo ni moja ya malengo ya mradi wa VIUNGO kwa ajili ya kuwawezesha wanufaika wa mradi huo katika kukuza kilimo cha mboga, matunda na viungo na kuongeza thamani ya mazao hayo ili kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla .
Kufuatia kupokelewa kwa maombi hayo kutoka kwa wakulima, wachakataji na wadau wa mnyororo wa thamani kwa mazao ya kilimo kutoka Unguja na Pemba, ambapo mradi wa VIUNGO umeunda kamati ya wajumbe nane (8) yenye jukumu la kupitia ,na kuhakiki maombi ya ruzuku za wanufaika hao ili kupewa ruzuku hiyo.
Kamati hiyo imeundwa na wajumbe kutoka Wizara ya kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo na Wizara ya fedha na Mpango Zanzibar Pamoja na watendaji wa mradi huo.
Katika kuhakikisha maombi hayo yanakidhi vigezo vilivyowekwa na mradi ,kamati hiyo itakaa kwa muda wa wiki moja kwa lengo la kuzipitia na kuhakiki maombi yote.
Jumla ya wanufaika wa mradi wa VIUNGO 70 kati ya 734 waliiomba watapata ruzuku ambayo itachochea ufikiaji wa malengo ya kukuza mnyororo wa thamani kwa mazao ya viungo, mboga na matunda na kuinua kilimo cha wakulima wadogo wadogo Zanzibar.
Value Web Horticulture and Income Growth Project unajulikana kama mradi wa VIUNGO, ni mradi wa miaka minne umeanza Juni 2020 hadi Juni 2024, upo chini ya program ya AGRI-CONNECT na unatekelezwa Unguja na Pemba na Jumuiya ya PDF wakishirikiana na Community Forest Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Imetolewa na Kitengo cha Habari na mawasiliano
TAMWA, Zanzibar