Na Kassim Nyaki, Ngorongoro.
Watalii wanaotembelea vivutio vya Utalii nchini hususan eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wameendelea kuvutiwa na aina mbalimbali za shughuli za utalii zilizoko katika Hifadhi hiyo.
Shughuli za utalii ambazo zinafanyika katika hifadhi ya Ngorongoro ni pamoja na utalii wa picha (Photographic tourism), utalii wa kutembea (walking safaris), Utalii wa akiolojia (archeological tourism) katika Bonde la Olduvai na Laetoli, utalii wa kupanda maputo angani (hot air balloon) na utalii wa kupanda milima (Mountain hiking) ambayo vyote vinapatikana katika hifadhi ya Ngorongoro.
Bw. Remen Rudolff kutoka Marekani ameelezea kufurahishwa na utalii wa picha katika bonde la Ngorongoro lenye umbo la kipekee la mandhari asilia yaliyopambwa na mtawanyiko wa wanyama na ndege mbalimbali.
“Niko katika eneo zuri na la kipekee duniani ambalo kila mtu anapaswa kuwa na ndoto ya kufika hapa, tumekuwa na muda mzuri wa kutalii, waongoza utalii wetu ni wakarimu sana na wajuzi wa hadithi za porini na tabia za wanyamapori, tumeona vivutio vingi; wanyama, mimea, ndege na maeneo ya malikale ambavyo kwa ujumla vinaipa Ngorongoro uzuri wa kipekee kwa Afrika na duniani kwa ujumla”
Sarah Tery kutoka Canada anabainisha kuwa yeye kama mpenda utalii wa kutembea amefurahi utalii wa matembezi (walking safari) akiwa Ngorongoro hasa katika eneo la Endoro ambapo wakiwa matembezi na wenzake katika eneo la Endoro ameona tembo na nyati na kuona msitu uliotunzwa vizuri, maporomoko ya maji ya endoro, kusikika kwa sauti za ndege wazuri wakiwa katika mazingira asilia na kushuhudia mapango ya tembo (Elephant caves) ambayo tembo huchimba kama sehemu ya kuja kupumzika na kulamba udongo ambao ni sehemu ya virutubisho katika miili yao.
Baadhi ya watalii hupendelea utalii wa kutembea kwa miguu katika vivutio vilivyopo upande wa Kaskazini mashariki mwa hifadhi Ngorongoro ambavyo ni Kreta ya Empakai, Kreta ya Olmoti na Mlima Lolmalasin ambao ndio mlima wa tatu kwa urefu nchini Tanzania ukiwa na urefu wa Mita 3,666.
Watalii wanaopenda utalii wa akiolojia na mambo kale wamekuwa wakitembelea eneo la Bonde la Olduvai lenye utajiri wa gunduzi mbalimbali ikiwemo fuvu la binadamu wa kale Zinjanthropus, Makumbusho Hai ya Dkt. Mary Leakey, mchanga unaohama pamoja na Nyayo za Laetoli zenye umri wa miaka takriban Milioni 3.6 iliyopita.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt. Freddy Manongi kati ya mwezi Julai 2022 hadi Juni 2023 jumla ya watalii 752,232 walitembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, hii ni tofauti na mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo jumla ya watalii walikuwa 425,386.