NA KHADIJA KOMBO-PEMBA.
Waumini waliorudi kwenye ibada ya hijja wametakiwa kuendeleza mema waliyoyachuma katika Hijja hiyo ili kuwa mfano bora kwa wengine kwa kuzingatia kwamba wema ndio msingi imara unaotakiwa kufanywa katika maisha ya kila siku .
Akizungumza na Mahujjaj waliosafiri kupitia taasisi ya Tattauwe pamoja na waumini wengine wa dini ya Kiislam katika kikao cha Tathmini juu ya safari ya Hijja mwaka huu huko katika ukumbi wa Skuli ya Madungu Sekondari Chake Chake Sheikh Abdalla Hamad Salim kutoka Ofisi ya Mufti Pemba amesema daima Mahujjaj wanatakiwa kuwa kioo ndani ya jamii kwa kuongoza kufanya mambo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya TATTAUWE ambayo ni miongoni mwa taasisi zinazosafirisha Mahujjaj hao Sheikh Rashid Habib Ali Kombo amewaomba waumini wa dini ya Kiislam kushajihishana kwenda kufanya Ibada ya Hijja kwani kufanya hivyo ni kutekeleza nguzo ya dini na ujira mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Nao Mahujjaj waliohudhuria katika kikao hicho wameiomba taasisi hiyo kutoa elimu ya vitendo zaidi kwa mahujjaj watarajiwa ili watakapofika huko waweze kutekeleza ibada zao kwa ufanisi .
MWISHO.
KUANGALIA VIDEO HII BOFYA HAPO CHINI.