NA FATMA HAMAD PEMBA
Wanakikundi cha Mapambano Cooperative kinachojishuhulisha na ufugaji wa Samaki, Kaa na Kamba kilichopo Sizini wilaya ya Michewemi mkoa wa Kaskazini Pemba wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, pamoja na asasi nyengine kuviangalia na kuviunga mkono vikundi vya ushirika, ili viweze kwenda samba mba na Sera ya Serikali ya Uchumi wa Buluu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kwenye Kikundi chao Sizini Wilaya ya Micheweni walisema sera ya Serikali ya Uchumi wa Buluu ni kuhakikisha wanaviinuwa vikundi vya ushirika ili viweze kutoa tija na kuondokana na umasikini.
Alisema wamekuwa wakipata faida kubwa kwani tayari wameshapata pesa za kuendeshea maisha yao kupitia mavuno waliovuna msimu uliopita.
‘’ Tumeamua kufuga, Kamba na Samaki jambo ambalo litatuwezesha kujingizia kipato, hivyo twaiomba Serikali ituunge mkono kihali na mali ili kutimiza malengo ya Serikali juu ya uchumi wa buluu,’’ walieleza wanakikundi.
Mapema Naibu katibu wa kikundi hicho Thamrat Suleiman Said aliwataka wanakikundi wenzake wasikatishwe tamaa na maneno ya watu bali waendelee kupambana wakiendeleze kikundi chao.
“ Sisi kama vijana wa kike ni lazima tujiamini, tupambane ili tuweze kukiendeleza kikundi chetu jambo ambalo litatusaidia kupata kipato cha halali, “ alifahamisha.
Akitoa nasaha kwa wanakikundi hao Meneja wa mipango ya Bahari na Pwani kutoka Shirika la International Union for Conservation of Nature ( IUCN ) Elinasi Monga, alisema ni vyema kwa wanakikundi hao kuendeleza mradi wao huo wa ufugaji wa Samaki na Kamba kwani sasa hivi Duniani kote wamelekeza nguvu zao kwenye bahari.
“ Mukiitumia bahari vizuri mtaweza kuondokana na Umasikini, mtakuza uchumi wa nchi pamoja na kuondokana na mabadiliko ya tabia ya nchi’’, alifahamisha Meneja.
Alisema endapo watajipanga na kuachana na migogoro wataweza kujipatia kipato ambacho kitaweza kuendesha maisha yao sambamba na kujipatia ajira.
Nae Ofisa mdhamini wizara ya Uchumi wa Buluu Dk, Salim Moh’d Hamza aliwataka kuendeleza ushirika wao kwani kutawawezesha kupata fursa mbali mbali za kimaendeleo zilizopo Nchini kupitia sekta ya Uvuvi.
“Serikali ya Zanzibar inalengo la kuekeza zaidi kwenye sekta ya bahari, hivyo ni vyema mjitoe ili kuendana na soko la dunia,’’ alisema Ofisa mdhamini.
Alisema wizara itaendelea kuwasaidia wanakikundi wanaojishuhulisha na masuala ya baharini ili waweze kuenda na Sera ya Serikali ya Uchumi wa buluu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho Khalfan Hamad Khalfan alisema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2013, kilianza na wanachama 10 wanawake 5 na wanaume 5, na sasa kinawanachama 17 wanaume 8, wanawake 9 tayari walishawahi kuvuna mara tatu.
Hata hivyo alieleza kwa msimu huu wameingiza vifaranga vya Kaa kilo 150, wenye thamani ya shilingi Laki tisa (900,000) Samaki vifaranga Elfu kumi na moja mia tano na nne (11,504) wenye thamani shilingi milioni Nne Elfu ishirini na Sita na mia nne (4,026,400) na Kamba ndoo mia tisa wenye thamani ya shilling Milioni Saba (7,000,000).
MWISHO.