Thursday, January 9

ZECO wapo mbioni kukiangaza kijiji cha kivumoni

 

NA HANIFA SALIM, PEMBA

WANANCHI wa kijiji cha Kivumoni shehia ya Mtambwe Kusini Wilaya ya Wete Pemba, wametakiwa kuwa na subira wakati mafundi kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) wakiendelea na harakati za kuwafikishia huduma hiyo katika kijiji chao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisa Uhusiano wa Shirika la ZECO Pemba Amour Salim Massoud, kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kivumoni juu ya kuona huduma hiyo kutokamilika, alisema mafundi wapo katika maeneo ya ujenzi wanaendelea na zoezi hilo, hivyo wawe wastahamilivu.

Alisema, laini ndogo tayari zimeshajengwa na hatua iliyobakia ni kujenga laini kubwa ambapo tayari nguzo zimeshafikishwa katika eneo husika, ili ziweze kufungwa na wananchi wapate huduma hiyo.

‘’Harakati za kupeleka umeme zinaendelea ndani ya kijiji cha Kivumoni na upimaji wa laini zote tayari umeshaanza, mafundi wetu wanaendelea na hatua ya laini kubwa pamoja na kufunga transfoma ambayo itakua ni hatua ya mwisho’’, alisema.

Aidha aliwataka wananchi hao, kutayarisha mifumo ya miondombinu ya umeme katika nyumba zao, ili mafundi watakapomaliza zoezi hilo la uungaji, waweze kupata huduma hiyo muhimu moja kwa moja bila ya usumbufu.

Hata hivyo alifafanua, kuhusu suala la ulipwaji wa fidia kwa wananchi ambao walikatiwa miti yao pamoja na vipando vyao, watalipwa kwani bado mchakato wa kupatiwa umeme unaendelea na suala hilo linafanyiwa kazi.

Awali mmoja wa wanakijiji cha Kivumoni Naima Khalid Ali alisema, wana shauku kubwa ya kuona huduma hiyo imewafikia ndani ya kijiji chao.

‘’Sisi jambo lolote ambalo ni la kimaendeleo linapokuja kwetu hatulidharau tuko pamoja na Serikali yetu, tunaiomba itufanyie haraka ili tuone umeme ukiwaka ndani ya nyumba zetu’’, alisema.

Nae mwananchi Amour Suleiman Mohamed alisema, huduma ya umeme itakapopatikana wataweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika masuala ya kiuchumi, kwani Mtambwe ni sehemu ya ukanda wa bahari hivyo wataweza kuutumia katika masuala yao ya uvuvi na mambo mengine.

Mwananchi Ali Said Khamis wa Kivumoni aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwajali wananchi wake na kusema kuwa, huduma hiyo ni hitaji la watu wote wa shehia hiyo kwa muda mrefu sasa, ingawa matumaini yao yao karibu.

Kwa upande wake Sheha wa shehia ya Mtambwe Kusini Othman Ali Khamis alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi  ina nia njema na wananchi wake, hivyo aliwataka wananchi wake kuwa na subira wakati mafundi wakiendelea na zoezi hilo.

                                         MWISHO.