Wednesday, January 8

Juhudi za pamoja zinahitajika kuzuwia uharibifu wa mtambwe Kusini.

SUALA la ukataji wa miti na utiaji moto kwa ajili ya kutayarisha mashamba ya kilimo, limekua likifanyika kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbali mbali ya Mtambwe kusini, Pichani wananchi wakitia moto miti waliokata ili waweze kuendelea na shuhuli za kilimo, kitu ambacho kinapelekea uharibifu wa mazingira.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA ABDI SULEIMAN,PEMBA.

MITI ni uhai na inapaswa kulindwa, kuthaminiwa na kutunzwa, kutokana na mchango mkubwa kwenye maisha ya bianaadamu, wanyama na ndege.

Katika miaka ya hivi karibuni, misitu imekua ikiteketea kwa kiasi kikubwa, kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo kilimo, uvuvi, uvunaji wa asali na matumizi ya majumbani na shuhuli za kibinaadamu zisizozingatia suala zima la uhifadhi wa mazingira.

Ukijani wa Kisiwa cha Pemba uliokua ukitambulika, kujulikana sasa unapotea siku hadi siku, kutokana na uharibifu wa mazingira.

Siku za hivi karibuni misitu ya asili na iliyohifadhiwa, imekua ikipotea kutoka na ukataji wakuni, uchukuaji wa mchanga katika fukwe kwa shuhuli za kijamii na kibiashara.

Shehia ya Mtambwe kusini ni miongozi wa maeneo yalioathirika na ukataji wa miti, uchukuaji wa mchanga katika fukwe kwenye visiwa vidogo vidogo.

WANANCHI WANAWASEMAJE WAO

Salum Hamid Kombo mkaazi wa Mtambwe Kusini, anasema uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti katika misitu ya juu, baharini na uchukuaji wa mchanga kwenye visiwa upo kwa asilimia kubwa .

Anasema miti imekua ikitwa kwa matumizi mbali mbali, ikiwemo upigaji wa mkaa, majenzi, kuni za kupikia na kuni za kuuzwa, watumiaji wa bekari za mikate ya kizamani na Vikosi vya SMZ.

Hassan Salum Ali, anasema wanaoharibu mazingira ni watu kutoka ndani ya shehia husika, wakishirikiana na wanaotaka nje na kupeleka kuathiri mazingira yao.

“Kuna watu wanakata miti mikubwa kwa ajili ya kuni au vidogo, kuwauzia watu wa vikosi kwa ajili ya kuni, wapo wanaokata kwa ajili ya shuhuli za bekari za mikate, kama hali haijadhibitiwa tutabakia kuwa jangwa,”amesema.

Nae Fatma Khamis Silima, anasema tayari kuna maeneo yamechimbwa mchanga na kupelekea kuwatia hofu, kutokana na kuhatarisha maisha ya wananchi wa shehia husika, ikiwemo kunusuru visiwa vidogo vidogo na mabadiliko ya tabianchi.

Amewaomba wananchi wenzake wa mtambwe Kusini, kujitahidi kulinda maliasili ambazo zimekua zikipotea kila siku kutokana na tamaa na umaskini.

Kwa upande wake Zuhura Omar Mattar, anasema iwapo kamati ya hifadhi ya Mazingira Mtambwe na Serikali zitaweka mikakati madubuti ya ulinzi suala la uharibifu wa mazingira utapungua na kuondoka kabisa.

“Leo hapa Kamati inakamata watu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, lakini siku ya tatu unawakuta nje, serikali ikiweka nguvu basi itakua funzo kwa wengine watakaoharibu mazingira,”alisema.

KAMATI YA HIFADHI YA MAZINGIRA MTAMBWE KUSINI

Khamis Ali Said mjumbe wa kamati ya hifadhi ya mazingira, anasema uharibifu wa mazingira unatokana na ukataji wa miti upo kwa asilimia 70 hadi 80.

“Watu wanakata miti mpaka sehemu inakua nyeupe, tena bila ya kuwa na taarifa yoyote, wala kibali kutoka sehemu husika, mwisho inabakia jangwa”amesema.

Anasema uharibifu upo katika shehia yao, hata katika maeneo ya visiwa vidogo vidogo, wamechimba mchanga katika mafungu baharini hali inayoanza kutishia usalama wa visiwa hivyo.

Khamis anasema hifadhi ya msitu inaukubwa wa hekta 2977 kwa msitu wa juu na baharini, asilimia 70 wanaokata ni wakaazi wa Mtambwe na asilimia 30 kutoka shehia jirani, ikiwemo ndagoni, Mchanga mdogo, Jojo na Micheweni.

Aidha anasema katika kisiwa cha Pemba, ukiondosha msitu wangezi msitu uliobakia ni Mtambwe Kusini, kitu ambacho vikosi vya SMZ na wananchi wa shehia mbali mbali wanautegemea kwa kupata kuni za kupikia.

“Msitu huu wa jamii umeingia mpaka katika visiwa vidogo vidogo kama vile Kokota, Funzi, Maangwi, Pembe, Kashani, Mapanya na Kikunyuu, kuna misitu ya asili na imekua ikikatwa na wavuvi,”alisema.

Nae katibu wa kamati hiyo Said Hamad Omar, anasema mtambwe ilikua na mstu mkubwa, ambao sasa umeshatoweka na kubakia janga, hali iliyopelekea kutokea kwa mvua, upepo na kupeleka joto kali.

Anasema kwa sasa bahari imekua ikipanda juu kwa kasi, kutokana na kuchimbwa kwa mchanga pembeni mwa fukwe na kukatwa kwa miti kwa kisi kikubwa.

“Kutokana na hali ya uharibifu wa mazingira inayotokana na ukataji wa miti, uchukuaji wa mchanga katika fukwe na visiwa vidogo vidogo ni wazi kisiwa cha Pemba, hakiko salama tena na kipo hatarini kutoweka iwapo hali hiyo haitodhibitiwa na mamlaka husika,”amesema.

UKATAJI wa Kuni kwa ajili ya kupikia umekua ukifanywa kwa kiasi kikubwa katika shehia ya mtambwe kusini, picha baadhi ya kuni ambazo hutumika kwa kupikia zikiwa zimekusanywa na kusubiri kusafirishwa.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

MIKAKATI GANI WALIONAYO

Afisa elimu ya mazingira kutoka kamati ya hifadhi ya Mazingira Mtambwe Kusini Zuwena Omar Ali, amesema mikakati ni kuendelea kushajihisha jamii na wadau mbali mbali, kupanda miti kwa wingi katika maeneo ya baharini na juu, ili kurudisha haiba ya kijani ya kisiwa cha Pemba.

“Sisi kama kamati tumeshapanda miti zaidi ya 40000 katika maeneo mbali mbali, ikiwemo miti ya juu kama vile miembe, mikungu, minazi, mifenesi na miti mengine pamoja na miti ya Pwani mikandaa (mikoko),”mefahamisha.

Aidha anasema ni wakati sasa wa kutumia majiko sanifu ya kuni moja, umeme na Gesi katika kupikia, ili kupunguza matumizi mabaya ya miti kukatwa kupigwa tanu za mkaa.

Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba Mwalim Khamis Mwalim, anasema mikakati mbali mbali inachukuliwa ikiwemo kufanywa ufutaliaji kwa kushirikiana na kamati ya hifadhi ya msitu, kwa kuyanya doria za mara kwa mara.

Anasema watu wanaowakamata huwapiga faini au kufilisi mali zao zinazotumika, ili kutoa fundisho kwa watu wengine wanaoharibu mazingira.

MKUU IDARA YA MISITU PEMBA

Mkuu wa Idara ya Misitu Pemba Massoud Bakar Massoud, amesema suala la uharibifu wa mazingira lipo, katika kisiwa cha Pemba msitu uliobakia ni Mtambwe Kusini pekee.

Uharibifu huo umechangiwa kutokana na kuongezeka kwa shuhuli za mahitaji ya wananchi, kutoka Chake Chake na Wete kuhitaji kuni, mkaa, miti kwa ajili ya majengo.

“Wakataji wakubwa wa miti hii ni wenyeji wenyewe, kutokana na tamaa za kifedha, kutokana na kulazimishwa na mahitaji yaliyopo mjini,”amesema.

IDARA YA MAZINGIRA INASEMAJE

Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba Mwalimu Khamis Mwalimu, amesema suala la ukataji wa miti na uchukuaji wa mchanga, linapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote, ili mazingira ya Mtambwe yasiendelee kuharibiwa.

“Kwa sasa kuna eneo kubwa limekua jangwa hili, limetokana na suala zima la uharibifu wa mazingira, tumeruhusu watu kutoka nje ya shehia kuindia na kuharibu na sasa imekua kilio wetu,”amesema.

Aidha amesema kama hali ya uharibifu litaendelea suala la ukosefu wa mvua, joto kali na maradhi yanaweza kujitokeza kutokana na ukataji wamiti.

SUALA la ukataji wa miti na utiaji moto kwa ajili ya kutayarisha mashamba ya kilimo, limekua likifanyika kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbali mbali ya Mtambwe kusini, Pichani wananchi wakitia moto miti waliokata ili waweze kuendelea na shuhuli za kilimo, kitu ambacho kinapelekea uharibifu wa mazingir.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

WIZARA YA KILIMO UMWAGILIAJI MALIASILI NA MIFUGO ZANZIBAR

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar 2023/2024, Waziri wa Wizara hiyo Shamata Shaame Khamis, amesema mazao ya misiti takwimu zinaonyesha mwaka 2022 matiumizi ya kuni yameongezaka kutoka mita za ujazo 25,813 mwaka 2021 hadi kufikia mita za ujazo 26,236.

Matumizi ya boriti (majengo) yameongezeka kutoka mita za ujazo 1,422 mwaka 2021 hadi 1,741 mwaka 2022, uzalishaji wa mapau ya kuezekea umeongezeka kutoka mita za ujazo 2,956 mwaka 2021 hadi kufikia mita 2,970 mwaka 2022.

Nao uzalishaji wa nguzo kubwa umepungua kutoka mita za ujazo 3,098 mwaka 2021 hadi kufikia 2,948 mwaka 2022, kwani ongezeko la matumizi ya mazao ya misitu limetokana na matumizi makubwa ya shughuli za kimaendeleo ikiwemo ujenzi, upishi wa dagaa, bekari za mikate na kambi za vikosi vya Ulinzi, ambao bado unaendelea kutumia kuni kwa kiwango kikubwa.

“Kwa wananchi wa mijini matumizi ya kuni yamepungua, kwa vile wamejielekeza kutumia nishati mbadala ya kupikia ikiwemo gesi na umeme,”alisema.

Nae Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, akiwasilisha bungeni bajeti ya 2023/2024 Mohamed Omary Mchengerwa, anasema jukumu la wakala wa huduma za misitu Tanzania –TFS ni kusimamia, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali zamisitu na nyuki zilizochini ya serikali kuu.

Anasema jumla ya hifadhi za misitu 463 inayojumuisha misitu ya asili 416, misitu ya mazingira asilia 23, mashamba ya miti 24 na hekta 158,100 za mikoko.

Aidha Tanzania ina misitu yenye hekta milioni 48.1 ambapo asilimia 93 ni misitu ya mataji wazi (woodland), na asilimia saba (7) ni misitu iliyofunga,

SUALA la ukataji wa miti na utiaji moto kwa ajili ya kutayarisha mashamba ya kilimo, limekua likifanyika kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbali mbali ya Mtambwe kusini, Pichani wananchi wakitia moto miti waliokata ili waweze kuendelea na shuhuli za kilimo, kitu ambacho kinapelekea uharibifu wa mazingir.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

ATHARI ZAKE NI NINI

Said Hamad Omar, anasema wananchi Mtambwe kwa sasa mvua imekua ikikata tafauti na miaka ya nyuma mvua za mara kwa mara kutokana na msitu kuwa imara.

“Maji ya bahari yamekua yakiingia katika mashamba ya wa kulima, mbao sasa hawalimi kutokana na athari za ukataji wa miti na jua kuwa kali kupitia kiasi,”amesema.

Mkuu wa Idara ya Misitu Pemba Massoud Bakar Massoud, amesema maji ya chumvi kupanda juu na kuvamia mashamba ya wakulima, mabadiliko ya hali ya hewa, joto kuwa kali, miongo ya mvua kubadilika na ardhi ya mtambwe kupungua ukubwa siku hadi siku.

Aidha Waziri Mohamed Mchengerwa anasema ongezeko la shughuli za kibinadamu, ikiwemo usafishaji wa mashamba kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji, makazi, umekuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa miti hasa uchomaji wa moto ndani ya hifadhi za misitu.

“Uchomaji moto holela umekuwa na athari kubwa katika maeneo ya hifadhi ikiwemo kupoteza bioanuai, kuathiri ubora wa miti na upotevu wa mapato ya Serikali, mfano katika kipindi cha mwaka 2021/2022 takriban hekta 3,172 ziliungua moto katika mashamba ya miti ya Sao hill, Wino na Buhigwe,”amesema.

MITANDAO YA KIJAMII INASEMAJE JUU YA MISITU

Zaidi ya viongozi 100 wa dunia wa meahidi kukomesha na kubadili athari za ukataji miti ifikapo mwaka 2030, katika mkataba wa kwanza mkuu wa mkutano wa kilele wa COP26.

 

Mkutano wa COP26 kilele wa wiki mbili huko Glasgow, unaonekana kuwa muhimu, ikiwa mabadiliko ya hali ya hewa yatadhibitiwa, ambapo nchi nyengine zitakazotia saidi ni Canada, Brazili, Urusi na Indonesia, zinasheni karibu asilimia 85 ya misitu duniani.

 

Aidha karibu hekta milioni 12 ya misitu katika dunia ya kitropiki ilipotea mwaka 2018, ambapo ni sawa na kupoteza viwanja 30 vya mpira wa miguu kwa dakika.

Wakati ripoti ya ‘Global Forest watch’ ikiwasilisha kupungua kwa misitu kwa mwaka 2016 na 2017, ingawa bado upoteaji wa misitu ulikuwa umeanza tangu mwaka 2001.

 

NINI KIFANYIKE

Mkuu wa Wilaya ya Wete Dkt. Hamad Omar Bakari, anasema nguvu za pamoja kwa wananchi wa Mtambwe Kusini, zinahitajika ili kuwatia mikononi waharibifu wa mazingira.

“Suala la muhali tunapaswa kuliweka pembeni katika ulinzi na uhifadhi wa mazingira, tusipofanya hivyo tutaweka mazingira yetu hatarini,”amesema.

Mkuu wa Idara ya Misitu Pemba Massoud Bakar Massoud, amesema nguvu za pamoja zinahitajika katika kuendeleza na kulinda msitu huo wa asili, na kuachana na muhali kwani wanaofanya matukio hayo wengi wao ni vijana kutoka shehia hiyo.

Afisa elimu ya mazingira kutoka kamati ya hifadhi ya Mazingira Mtambwe Kusini Zuwena Omar Ali, amesema watahakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Mtambwe juu ya suala zima la ulinzi na upagaji vita ukataji wamiti.

Haji Suleiman Mzee mjumbe wa kamati hiyo, amesema serikali inapaswa kushirikiana kwa dhati katika kusimamia tatizo hilo, kwa kuwapatia chombo cha kufanya ufatiliaji bahari juu ya uchotaji wa mchanga katika fukwe na ukataji wa miti kwenye visiwa vidogo vidogo.

“Kwa sasa kwetu sisi ni ngumu kufika baharini kwenye visiwa saba (7) vidogo vidogo kuzunguka kama hatuna chombo maalumu, na wale wanaowakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kuhakikisha inatia nguvu,”amesema.

Aidha kwa mujibu wa Ripoti ya The State of the World’s Forests”,inasema hatua za dharura zinahitajika, ili kutunza bayoanuai ya misitu wakati ambapo ukataji wa miti na kudidimia kwa misitu vinaendelea kwa kiwango cha kutisha duniani.

Iadha ripoti hiyo inaonyesha hekta milioni 420 za misitu imeangamia kupitia kutumia ardhi kufanya shughuli zingine tangu mwaka wa 1990, ambapo misitu ina spishi 60,000 za miti mbalimbali, asilimia 80 ya spishi za amfibia, asilimia 75 ya spishi za ndege, na asilimia 68 ya spishi za mamalia duniani.

MWISHO