NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
AFIASA Mdhamini Wizara ya Maji, Nishati na Madini Pemba Injinia Suleiman Hamad Omar, amesema wakati umefika kwa shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuwa na sheria, kanuni na sera zinazoendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane katika kuwapatia maendeleo bora wananchi.
Alisema uwepo wa sheria, kanuni na sera zinawafanya wafanyakzi wa shirika hilo, kuzidisha kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mdhamini Injinia Suleiman aliyaeleza hayo wakati wa mkutano wa wadau, kupitia rasimu ya mabadiliko ya sheria ya ZECO namba 3/2006, mkutano uliofanyika mjini Chake Chake.
Alisema uwepo wa sheria hiyo itaweza kwenda sambamba na mabadiliko yaliyopo kwenye teknolojia, kiuchumi na kijamii, hivyo serikali imeona ipo haja ya kupitia baadhi ya sheria, sera na kanuni, ili ziweze kwenda na wakati.
“Hivi sasa mashirika mengi yameamua kubadilisha sheria zao, sera na kanuni, ndio maana na sisi ZECO tupo katika kukusanya maoni ya wadau juu ya mapendekezo ya rasimu ya sheria, ili kwenda na wakati huu wa sasa,”alisema.
“Niwakati wakufanyia mabadiliko ya sheria, kanuni na sera ili ziweze kwenda sambamba na kasi ya serikali ya awamu ya nane, maamuzi yanayofanyika lakini sheria zinapinga,”alisema.
Mapema mwenyekiti wa kamati ya mabadiliko ya sheria ya ZECO, Mwanasheria Hadia Abdulrahman Othman, aliwataka wadau na wafanyakazi wa shirika hilo, kuhakikisha wanatoa maoni yao ipasavyo katika rasimu hiyo, ili sheria itakayopatikana iweze kukidhi mahitaji ya wafanyakazi na wananchi.
“Rasimu hii imeangalia mazingira na mabadiliko ya sera yaliyopo hivi sasa, ikiwemo katika kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi,”alisema.
Naye katibu wa kamati ya mabadiliko ya sheria ya ZECO, Mwanasheria Suleiman Pandu Kweleza, wao wanawauzia wananchi Uniti shilingi 266 huduma ambayo ipo rafiki kwa wananchi.
Akijibu hoja za Wadau wa kutoka maoni juu ya Rasimu ya Mabadiliko ya sheria, meneja wa ZECO Pemba Mohamed Juma, amesema ZECO linakusudia kubadilisha mita zote za kizamani na kuweka za kisasa, ambazo mtu anaweza kuona umeme wake uliobakia akiwa ndani mwake na kuweka mwengine bila ya kutoka nje.
“Mita tuliziweka nje ili kuwapa urahisi wasomaji wa mita wanapokuja, baadhi ya nyumba zilizokua zinafungwa ila sasa kila kitu kinaenda kisasa zaidi,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa kikao Adi Juma Faki, alisema maoni ya wadau ni muhimu katika rasimu hii, kwani ZECO sasa wanataka kubadilika katika utendaji wao wa kazi hivyo wadau ni wakati wa kuifanya rasimu kuwa sheria kamili.
Nao baadhi ya wadau waliotoa maoni yao, wamesema vizuri kuweko na muda maalumu wa kumuungiza mteja huduma baada ya kulipa malipo yake na sio kama ilivyo sasa mtu anaweza kulipa na kuungiwa huduma baada ya miezi miwili au mitatu.
MWISHO