Sunday, November 24

Wakulima wa karafuu Kaskazini Pemba washauriwa kutumia tigo pesa kupokea malipo yao.

wakulima wa zao la karafuu mkoa wakaskazini Pemba, wakishajihishwa malipo yao ya zao hilo kupitia kwenye mitandao ya simu badala ya pesa mkononi

   NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MKURUGENZI  wa Mfuko wa maendeleo ya Karafuu Zanzibar Ali Suleiman Mussa, amesema dunia sasa imebadilika katika kutafuta pesa, utapeli umeongezeka na njia rahisi ya kubaki na pesa salama ni kutumia huduma ya tigopesa .

Alisema njia hiyo itaweza kuwasaidia wakulima wa zao la karafuu, fedha zao kuendelea kuwa salama muda wote na sio kuchukua mkononi hali inayohatarisha hata maisha yao.

Mkurugenzi huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mkutano wa wakulima wa karafuu Mkoa wa Kaskazini Pemba, juu ya kuhamasisha kutumia mitandao ya simu ya Tigo Zantel katika malipo ya zao hilo.

Aliwataka wakulima katika msimu wa karaufuu ulioanza Agosti 3, kuhakikisha wanatumia mitandao ya simu katika kuweka fedha zao, huku wakiendelea na mchakato wa kusajiliwa wakulima wote.

“Kutumia mitandao katika kuhifadhi fedha ni sehemu salama, kuliko kuondoka na fedha mkononi wengi wanakumbana na changamoto za kuungua, kuliwa na mchwa au panya pale fedha wanapozihifadhi majumbani,”alisema.

Alisema mkulima anaposajiliwa anapopata tatizo anashuhulikiwa mwanzo, kuliko asiyesajiliwa kwa sababu itakua hatambuliwi na shirika la ZSTC.

Nae Mdhamini wa shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Pemba Abdalla Ali Ussi, aliwataka wakulima kukubali kulipwa fedha zao kupitia huduma ya Tigo pesa au benk na kama kuna matatizo wasisite kutoa taarifa kwa wahusika.

Alisema ulipaji wa fedha kwa kutumia mitandao ya simu ni rahisi, kwani mtu anapata fedha zake kwa wakati na kiwango kikubwa, kuliko fedha kuchukuliwa mikononi jambo ambalo hupelekea pesa kupotea.

Aidha aliwafahamisha wakulima hao kuwa ZSTC tayari, imeshafungua vituo vyake vya ununuzi wa karafuu kwa Unguja na Pemba, tokea Agositi 3 na tayari tani mbili za karafuu zimeshanunuliwa.

Aidha alisema lengo ni wakulima kupata malipo yao ya karafuu baada ya kuziuza katika shirika la ZSTC, kupitia kwenye mitandao ya simu na sio mkononi .

Kwa upande wake Meneja wa tigo Zantel Zanzibar Salum Nassor Mohamed, alisema tokea kuanza kwa malipo ya wakulima wa karafuu Unguja na Pemba, mwaka 2021 hadi 2023, zaidi ya wakulima 10,000 wameshapokea malipo kupitia tigoPesa na EzyPesa na zaidi ya bilini 40 zimepelekwa kwa wakulima hao kupitia mitandao ya simu.

Alisema faida ya kutumia tigopesa ni njia salama ya kuweka fedha kuliko kuchukua fedha mkononi, ikitokea bahati mbaya na  kupotea simu, bado fedha zako zitaendelea kuwa na usalama.

Nae meneja wa tigoZantel kanda ya Pemba Farouk Ahmed, alisema mawakala wa kampuni hiyo watahakikisha wanakuwepo katika vituo vyote vinavyohusika na mauzo ya zao la karafuu.

Aidha aliahidi hakutokuwepo na changamoto yoyote ya kukosekana kwa mawasiliano ya mtandao, kwani wamejipanga kuendelea kuboresha huduma hizo.

Kamanda wa ZAECA Mkoa wa Kaskazini Pemba Nassir Hassan Nassir, aliwapongeza wakulima wa karafuu kwa mashirikiano makubwa walioyatoa katika msimu uliopita huku akiwataka kuendelea na msimu huu.

Mkulima wa karafuu kutoka kisiwani kwa binti Abeid, Mohamed Salum Ali, aliwapongeza Tigo Zantel kwa mikakati yao mizuri mwaka jana, kwani fedha aliweza kupokea kwa wakati muwafaka bila ya usumbufu wowote.

Aidha alisema changamoto kubwa ilikuwa kwenye viwango vya mikato ilikuwa mikubwa na wao, hivyo na kuwaomba kuweka wazi suala zima la makato kwa wakulima.

Nae mkulima Mohamed Ali Mmaka kutoka Mtambwe, aliitaka tigoZantel kuhakikisha wanawafutilia matapeli wanaotumia mitandao ya simu ili kujuwa wanaovujisha siri za wateja wao.

MWISHO