Sunday, November 24

Vijana wa kijiwe cha Africana wataka Sheria iwe kwa wote

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

VIJANA wanaokaa katika kijiwe cha vijana Afrikana Chake Chake wamesema, wanasikitishwa na kitendo cha kinachofanywa kwenye vyombo vya sheria cha kuwachiwa huru watuhumiwa wanaokamatwa na dawa za kulevya, huku wakiendelea kuwaathiri vijana mitaani.

Wamesema, wanashangaa sana kuwaona wakizurura mitaani watu wanaokamatwa na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya, ambapo wanaokamatwa na dawa kiwango cha chini wanaendelea kusota rumande na wengine wanatumikia chuo cha mafunzo.

Waliyaeleza hayo walipokuwa wakizungumza na wadau wa msaada wa kisheria kutoka taasisi mbali mbali, wakati walipofika kijiweni hapo kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Mmoja wa Vijana hao Mohamed Kassim alisema, changamoto kubwa inayowakabili ni kuachiwa kwa wanaokamatwa na dawa nyingi za kulevya, wakati wanaokamatwa na dawa kidogo wanaendelea kushikiliwa.

‘’Hii Sheria ni ya watu wote lakini kinachotushangaza ni pale tunapowaona vijana waliokamatwa na dawa za kulevya wapo mtaani wanadunda hasa wale waliokamatwa na kiwango kikubwa cha dawa hizo’’, alisema kijana huyo.

Alisema, Sheria inapaswa kutekelezwa kwa watu wote na sio baadhi kama vile haiwahusu, jambo ambalo linaonekana kuelemea upande mmoja kwa wasiokuwa na uwezo.

Nae Khamis Haji Ali (mandonga) alisema, vijana wameamua kujiajiri wenyewe kupitia bajaji na bodaboda, ili kuondokana na tabia ya kukaa maskani, ingawa kinachowakwaza ni askari wa usalama wa barabarani kuwabugudhi na kuwakosesha kufanya kazi zao vizuri.

“Sisi tunapozidisha abira mmoja, kwenye kibajaji askari wanatulazimisha kulipa pesa hapo hapo, kama huna wanaipandisha bajaji juu jambo ambalo sio sahihi, au wanataka tukae vijiweni tufanye uhalifu”, alisema.

Aidha alisema, posi zinazotolewa na Jeshi la Polisi lazima waweke siku angalau tatu ndipo imalize muda wake, kwani wakati mwengine hawana pesa ya kulipa pale pale.

Kwa upande wake dereva wa bajaji Mohamed Kassim Iddi alisema, wanasikitishwa na faini wanayotakiwa kulipa baada ya kuzidisha abiria, jambo hilo linawakwamisha sana katika biashara yao hiyo kwani hakuna abiria wengi.

‘’Ukikamatwa umezidisha abiria mmoja tu tunatozwa faini ya shilingi 80,000, tunawaomba waweke kiwango kidogo kwa sababu na sisi tunafanya biashara na abiria wenyewe hawapo’’, alisema.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria wilaya ya Chake Chake Nassor Bilali Ali alisema, vijana wanalipa fedha nyingi kutokana na kutokujua Sheria, hivyo ni vyema wakapewa elimu ya sheria ili kujua haki zao.

Nae mwanasheria kutoka Shirikisho la Msaada wa kisheria na Haki za binaadamu Zanzibar(ZLHO)Khalfan Amour Mohamed alishauri kufanyika kwa mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa kijiwe, uongozi wa bodaboda na bajaji, mawasiliano, polisi na wadau wa Sheria kujadili juu ya suala la kontroo namba na muda wake wa kumaliza ili kuondosha mzozo uliopo.

 

“Hipendezi kuona vijana hao wanapokamatwa wanatakiwa walipe fedha hapo hapo wakati vyombo vyenyewe wamekopa na wanatakiwa kurudisha mkopo, hali hii inarudisha nyuma maendeleo ya vijana”, alisema.

Nae Hakimu wa mahakama ya mwanzo Chake Chake Adamu Abdallah aliwataka vijana hao wanapokamatwa wajiue makosa yao, sababu za kukamatwa kwao na sio kuogopa kuuliza.

Kwa upande wake Afisa Opereshi Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba ASP Hassan Khamis alisema, dereva wa bajaji anapozidisha abiria mmoja, Jeshi hilo huwatoza faini ya shilingi 23,000 na sio shilingi 80,000 wala kuchukuliwa chombo kama wanavyodai.

Mapema Afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali alisema, katika wiki hiyo wamepanga kupita katika vijiwe mbali mbali vya vijana, ili kujua changamoto za kisheria wanazokumbana nazo.

                 MWISHO