NA SAID ABDULRAHMAN, PEMBA
WANAFUNZI wa skuli ya msingi na sekondari Pandani pamoja na sekondari Wete ambao wanajitayarisha na mitihani yao ya taifa, wamepatiwa msaada wa tochi na balbu vyenye thamani ya shilingi 23,5000 kwa ajili ya kuwasaidia wakati umeme unapozimwa.
Msaada huo umetolewa na Mkaguzi wa Polisi Jamii shehia ya Pandani, Inspector Khalfan Ali Ussi baada kutembelea kambi ya wanafunzi hao na kuona hali halisi ilivyo wakati unapozima umeme, jambo ambalo linawapa usumbufu wakati wanapopitia masomo yao.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo alieleza kuwa, vitaweza kuwasaidia wanafunzi hao katika kujisomea wakati umeme unapokata kwenye mabweni yao.
Inspector Khalfan aliwataka wanafunzi hao kujitahidi katika masomo yao, ili waweze kufaulu vizuri na kuwa wakombozi katika familia zao na taifa kwa ujumla.
Aidha alieleza kuwa, wako tayari kufuatilia nyenendo za wanafunzi hao na yeyote ambae atapatikana na hatia ya kutohudhuria kwenye masomo, adhabu kali itatolewa dhidi yake.
“Kwa wanafunzi ambao mnakaa kambi katika skuli zetu hizi, ni vyema tukafuata muda ambao umepangwa ili kuondosha matatizo ambayo yanaweza kuepukika”, alieleza.
“Kwa wale ambao wamekimbia skuli, niwaombe wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto hao wanarudi skuli kuendelea na masomo yao na hili sio ombi ni lazima”, alifahamisha Khalfan.
Sambamba na hayo Inspekta huyo aliwasisitiza wanafunzi hao kuacha rushwa muhali kwani inarudisha nyuma maendeleo yao na jamii kwa ujumla.
“Pale ambapo kutatokezea tatizo lolote ambalo liko kinyume na maadili yetu, ni vyema tukatoa taarifa mapema ili jambo hilo liweze kuchukuliwa hatua na wala tusione aibu kusema ukweli”, alisema Inspekta Khalfan.
Mapema Mratibu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kaskazini Pemba Inspekta Makame Ali Makame alifahamisha kuwa, lengo la kuanzishwa Polisi jamii nchini, ni kuhakikisha wanaondosha vitendo vya uhalifu ambavyo vimekithiri katika jamii.
Inspekta Makame alieleza kuwa, katika jamii kumekuwa na matukio mbali mbali ya uvunjifu wa amani, hivyo aliwasisitiza wanafunzi hao kutoa taarifa kwa wakubwa wao pale ambao wataona kuna viashiria vibaya.
Sambamba na hayo Inspekta Makame aliwasisitiza wanafunzi hao kutumia muda wao mwingi katika kushughulikia masomo yao, kwani ndio msingi bora wa maisha yao ya baadae.
Nae Kaimu mwalimu Mkuu wa skuli ya msingi Pandani Halima Khalifan Said aliupongeza uongozi wa Polisi jamii hehia ya Pandani kwa kuwapatia wanafunzi hao msaada, ambapo umewapa faraja na furaha.
Aidha Halima aliahidi kushirikiana pamoja na uongozi wa Polisi Jamii shehia ya Pandani, ili kuona kero ambazo zipo katika skuli zao zinatatulia kwa mashirikiano ya wote.
“Tunamshukuru sana Inspekta Khalfan kwa msaada wake aliotupatia, hii inaonesha dhahiri kuwa ana upendo wa dhati kwetu”, alisema Halima,
Nae mwanafunzi Fatma Salim alitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake na kusema kuwa kutatuliwa changamoto hiyo iliyokuwa ikiwakabili, imewapa matumaini makubwa kuendelelea na masomo yao.
“Tulikuwa tunapata shida sana wakati unapozimwa umeme, hivyo kwa vifaa hivi ambavyo tumepatiwa , tutavitunza ili kuona kwamba vinadumu kwa maslahi yetu ote”, alisema mwanafunzi huyo.
MWISHO