Monday, November 25

WANANCHI MLETENI: ‘MARUFUKU MGENI KUINGIA PASI NA TAARIFA’

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI wa kijiji cha Mleteni, shehia ya Kisiwani wilaya ya Wete Pemba, katika kukabiliana na dawa za kulevy na wizi, wameendelea kupiga marufuku kwa mgeni yeyote, kuingia kijijini hapo, pasi na taarifa kwa uongozi wa kijiji.

Walisema, hawatomvumilia mgeni wala mwenyeji aliyefuatana naye, ikiwa watabainika ameingia kinyemela kijijini hapo na hakuna taarifa rasmi.

Walieleza kuwa, kwa sasa kijiji chao cha Mleteni, kiko salama kiasi, kwa dawa za kulevya na hata wizi, ndio maana wanawasisitiza wenyeji wanaotembelewa na jamaa zao, kutoa taarifa rasmi, kwa uongozi wa kijiji.

Mmoja kati ya wananchi hao Salim Mussa Ali, alisema ingawa utumiaji wa dawa za kulevya bado uko chini, lakini wanaendelea kuwataka wenyeji, wanaoingia na wageni wao, kutoa taarifa rasmi.

‘’Tumeshagundua kuwa, wapo wageni wengine wanakuja na nia mbaya katika kijiji chetu, sasa tukigundua na ikawa ana mwenyeji wake wa kijiji cha Mleteni, tutamfikisha mbele ya vyombo vya sheria,’’alieleza.

Nae Yassir Said, alisema bado kijiji chao kiko salama na utumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, na ndio maana kila mgeni anayeingia, wamependekeza, kuwepo kwa taarifa zake kamili.

‘’Inawezekana ile mikakati yetu ya kila wakati, ikawa inasaidia kupunguza wimbi la vijana kuzurura ovyo, na baadhi ya wakati ndio wanaojihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya,’’alieleza.

Akizungumzia juu ya wizi wa mazao kijijini hapo, mwananchi Alawi Said Yussuf, alisema wizi ni mkubwa kiasi, ingawa kwa sasa wanajiandaa kuanzisha kamati maalum.

Alisema, mifugo kama kuku na mazao kama ndizi, mihogo imekuwa ikiibiwa hasa nyakati za usiku, ingawa wamebaini ni watoto wao na sio wageni.

Kwa upande wao Asha Ali Sharif na mwenzake Aisha Nassib Shehe, walisema bado mkakati wa kweli na endelevu haujakuwepo wa kudhibiti vitendo vya wizi.

‘’Ni kweli utumiaji, usambaazaji na uuzaji wa dawa za kulevya kwenye kijiji chetu cha Mleteni haupo, lakini kama tukishindwa kudhibiti wizi, kisha dawa za kulevya zitafika,’’walisema.

Kaimu sheha wa shehi ya Kisiwani wilaya ya Wete, Bahati Juma Mtwana, aliwataka wananchi hao wa kijiji cha Mleteni, kuanzisha haraka ulinzi shirikishi kijijini hapo.

Alisema, kwa sasa karibu kila kijiji kwa Unguja na Pemba, kimeshaathirika kwa wizi, dawa za kulevya, vitendo vya udhalilishaji, hivyo kama kijiji chao cha Mleteni kiko salama na dawa za kulevya, waendelee kudhibiti.

Kaimu sheha huyo alisema, ingawa kwa sasa wamo katika kuufufua ulinzi shirikishi, lakini sio vibaya kijijini hapo wanao watakuwa na kamati yao.

Katika hatua nyingine, Kaimu sheha huyo wa shehia ya Kisiwani, amewakumbusha wananchi kuendelea kutoa taarifa Polisi, pindi wakibaini kuwepo kwa vitendo vya kihalifu.

‘’Kwa mfano kuna ubakaji, wizi, dawa za kulevya au jambo jingine lolote linaloashiria uvujivu wa amani, wasijaribu kuchukua hatua mikononi na badala yake, wawasiliane na mamlaka husika,’’alisisitiza.

Hata hivyo, amewataka wananchi hao kuwashajiisha watoto kuhudhuria masomoni, kwani serikali imesikia kilio chao cha ujenzi wa skuli ya maandalizi.

Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, alisema wakati umefika sasa wa kuendelezwa kwa kamati za ulinzi shirikishi katika shehia.

                                  Mwisho