NA TATU NAHODA, ZU
WANAKIJIJI wa kisiwa cha Kojani shehia ya Mpambani wilaya ya Wete Pemba, wameishukuru polisi jamii yao, kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya kihalifu kijijini hapo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wananchi hao walisema, tokea kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi shehiani hapo, vitendo kadhaa vya kihalifu vimepungua.
Walisema kuwa, ulinzi shirikishi umekuwa muarubaini tosha katika kijiji chao, kwa kupunguza matendo maovu, jambo ambalo kabla ya hapo halikuwepo.
Wananchi hao walieleza kuwa, umoja na mshikamano uliopo, umesaidia kudhibiti vitendo viovu, kama vile wizi wa mazao na mifugo, na kupelekea kuishi kwa amani na utulivu.
Mmoja kati ya wananchi hao Said Haji Said alisema, kwa sasa mifugo na vipando vyao vinanawiri, kutokana na kuimarika kwa ulinzi shirikishi, kijijini kwao.
Alisema kwa sasa wafugaji, na wakulima wanavuna wanachokipanda kwa wakati, kutokana na kuimarika kwa ulinzi shirikishi, jambo ambalo halikuwepo kwa muda mrefu kijijini kwao.
“Sisi wananchi lazima tutoe shukrani zetu kwa vijana wetu wa ulinzi shirikishi, maana sasa ndizi inapea, mihogo, kuku na hata wizi wa kawaida wa majumbani umepungua, alisisitiza mwananchi huyo.
Na mwananchi Fatma Nassor Ali alieleza kuwa, kuimarika kwa ulinzi shirikishi kijijini kwao, imetoa fursa kwa wanawake na watoto, kutembea bila ya wasiwasi hasa nyakati za usiku wamapema wanapokuwa na shughuli zao.
Aidha Mwanakame Kombo Hassan, alisema kilichobakia kwao, ni kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kikundi cha ulinzi shirikishi, katika kuiweka shehia yao salama.
Mapema Mjumbe wa polisi jamii shehiani hapo, Othman Mwinyi Shezume alisema, polisi jamii imekuwa ikifanya kazi zake ipasavyo, ili kudhibiti vitendo vyote vya kihalifu, kijijini hapo, kama vile wizi, ubakaji uporaji na utoro wa watoto masomoni.
Alieleza kuwa, wamefanikisha majukumu yao hayo, na yameleta mafanikio makubwa, kutokana na kuwepo kwa ushirikiano mzuri, baina yao na wanakijiji wa shehia hiyo.
“Jukumu la kulinda na kudhibiti vitendo viovu, ni jukumu la kina wanakijiji pia, hivyo ushirikiano wao na sisi waliotukabidhi jukumu hili, utaweza kuleta matunda mazuri katika kijiji chetu,’’alifanunua.
Kwa upande wake Naibu Sheha wa shehia hiyo Hassan Iddi Othman, aliwaomba wanakijiji wa shehia ya Mpambani, kuzidi kuleta ushirikiano na polisi jamii, ili kuunga mkono juhudu zao kwa lengo la kufanikisha azma yao.
Hata hivyo aliiomba, serikali kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na polisi jamii hiyo, juu ya changamoto ambazo wanapitia wakati wa utendaji wa kazi zao, kwa kuwapa mafunzo maalum.
MWISHO