NA MOZA SHAABAN, ZU
WAKULIMA katika Shehia ya Kojani Wilaya ndogo ya Kojani mkoa wa Kaskazini Pemba, wamewalalamikia wafugaji kutodhibiti mifugo yao, jambo ambalo hupelekea uharibifu wa mazao yao.
Akizungumza na Zanzibar leo, mkulima wa Viazi vitamu Saada Ali Faki kijijini hapo, alisema wamekua wakijishughulisha na kilimo ili kujikwamua kiuchumi, ingawa wafugaji hurejesha nyuma jitihada zao.
Alisema wamekuwa wakitumia nguvu na gharama kubwa, kupanda mazao ili yawasaidie kiuchumi, ingawa malengo yao hayafikiwi kwani wafugaji hushindwa kudhibiti mifugo yao na kufanya uharibifu mkubwa.
“Sisi tunatumia nguvu kupanda mazao, ili yatusaidie na familia zetu, ingawa wafugaji wanaturejesha nyuma kwa kuachia huru mifugo yao na kutuharibia mazao yetu,”alisema.
Nae mkulima wa zao la Mtama Bikombo Said Hamad alisema, wamekua wakichukua hatua kadhaa, ili kudhibiti suala hilo ikiwemo kuripoti matukio hayo kwa uongozi wa shehia na hatua stahiki kuchukuliwa, ingawa bado suala hilo linaendelea kijijini kwao.
Akizungumzia kadhia hiyo, mfugaji wa Ng’ombe na Mbuzi, Hassan Hussein Makame alisema, kuna haja kubwa kwao kudhibiti mifugo yao ili kuzuia uharibifu unaotokezea.
Alisema, iwapo watadhibiti mifugo yao, watatoa fursa kwa wakulima, kuendeleza kilimo chao, ili wapate tija kama wanavyo tarajia wenyewe.
Katika hatua nyingine amewaaasa wakulima, kutolinyamazia suala hilo, na ni muhimu kuliripoti katika vyombo vya sheria, ili wafugaji wasiodhiti mifugo yao kuchukuliwa hatua.
Nae mfugaji wa Mbuzi Issa Mohamed Yakoub, alisema wamekuwa wakiidhibiti, ingawa uharibifu mwengine unatokea, pale wanapokata kamba.
‘’Wakati mwengine mifugo hukata na kupelekea uharibifu wa mazao, lakini sio kama tunawaharibia kwa maksudi wakulima, kwani hao ni ndugu zetu,’’alifafanua.
Naibu Sheha wa shehia hiyo Ali Hamad Ali, alisema amekua akipokea malalamiko mara kwa mara kutoka kwa wakulima, juu ya wafugaji kutodhibiti mifugo yao, na tayari wameshachukua hatua kadhaa, kama kuzungumza na wafugaji.
“Hatua nyingine tunazozichukuwa ni kulipisha faini kwa mfugaji, ingawa bado suala hilo ni sugu kijijini hapa, na naendelea kutoa wito kwa wafugaji, kudhibiti mifugo yao ili, kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima,”alifafanua.
Hata hivyo amewataka wakulima kufanya mazungumzo ya utatuzi wa migogoro baina yao na wafugaji na wajiepushe na kujichukulia sheria mikononi.
Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari, alieleza kuwa wilaya itaendelea kuwatuma wataalamu na kutoa elimu ya kukinga na migogoro inayoepukia.
Mwisho