Friday, March 14

WEMA: ‘CHANGAMOTO ZA MAISHA MICHEWENI ZISIWE CHAKA LA UTORO WANAFUNZI’

NA ABUU BAKAR, ZU

WANAFUNZI wa skuli za Micheweni kisiwani Pemba, wametakiwa kuacha utoro na kuhudhuria masomoni kikamilifu, na hali ngumu ya maisha inowakabili, isiwe chanzo cha katitisha masomo.

Kauli imetolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilayani humo, Rishad Kombo Faki, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii, ofisini kwake Micheweni, juu ya utoro kwa baadhi ya wanafunzi, kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha.

Alisema hali ya kimazingira iliyopo Micheweni, isiwe chanzo kwa wanafunzi hao kukatisha masomo yao, kwani elimu ni haki yao ya msingi.

Alieleza kuwa, wazazi wamekuwa wakipambana, ili kuhakikisha wanawapatia watoto wao huduma za kila siku na za lazima, hivyo ni wajibu kwa wanafunzi hao kuthamini jambo hilo.

“Ni kweli mazingira yaliyopo Micheweni yana vivutizi vingi vinavyo sababisha wanafunzi kuwa watoro, na hii inatokana na wanafunzi kupata marafiki wasio kuwa wazuri kitabia,”alifafanua.

Akizungumzia athari ya wanafunzi kuwa watoro masomoni, alisema mojawapo ni kudumaa kiakili, kuongengezeka kwawasiojua kusoma na kuandika na kujirahisishia kuingia katika vitendo viovu.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa skuli ya sekondari ya Tumbe Nassor Rashid Said alisema, muamko mdogo kwa baadhi ya wazazi na walezi juu ya elimu, unasababisha kwa wanafunzi kua watoro masomoni.

Mwalimu mkuu huyo aliwataka wazazi na walezi, kuwa na ushirikiano katika kuwalea vijana wao na asiachiwe mzazi wa wakike pekee, kwani kufanya hivyo, kutaporomosha maendeleo ya elimu ya mtoto.

“Ulezi ameachiwa mzazi wa kike tu, na ndio maana hata tukiwaita kwenye vikao vya skuli, inakuwa vigumu kuwapa wazazi wanaume, jambo ambalo wakati mwengine, huzorotesha maendeleo ya elimu kwa mtoto,”alifafanua.

Mzazi Bimzungu Ali Rashid alisema kuwa, changamoto za kimaisha za majumbani, wakati mwengine ni tatizo linalowapelekea wanafunzi kuwa watoro masomoni.



“Ugumu wa maisha unaotukabili sisi wazazi huko majumbani kwetu na wanaume kutuachia majukumu peke yetu, nikichocheo kikubwa kwa watoto wetu kutohudhuria masomoni, kikamilifu,”alieleza.

Naye, mzazi Sabrina Haroun Hamad, alieleza kuwa ni vyema kwa wazazi na walezi wenzake, kuwasaidia vijana wao, ili kukamilisha ndoto zao za kielimu.

Wanafunzi Sada Ali Hamad na Kombo Mohamed Said wa kidato cha pili skuli ya Tumbe, wamewawataka wanafunzi wenzao, kutojihusisha na utoro, kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha, kwani kufanya hivyo kutapoteza ndoto zao za maisha.

Afisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, alizitaka kamati za wazazi za skuli, kusimamia utoro kwa wanafunzi ili kuhudhuria masomoni.

              MWISHO.