Thursday, January 30

Shirika la ZSTC linampango wa kununua unga wa karafuu

NA ABDI SULEIMAN,PEMBA

MDHAMINI wa ZSTC Abdalla Ali Ussi, amesema shirika lipo kwenye mpango wakununua unga wa karafuu, kutoka kwa wakulima na kuwataka kuuhifadhi unga huo.

Alisema kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na moja ya kampuni, ambayo imeonyesha nia ya kuuhitaji unga huo, kwa matumizi mbali mbali.

Mdhamini huyo aliyaeleza hayo, wakati alipokua akizungumza na wakulima wa karafuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, kikao kilichoandaliwa na kampuni ya simu za mkononi Tigo Zantel na kufanyika mjini Chake Chake.

Aidha aliwataka wakulima kuhakikisha wanazisafisha karafuu zao vizuri, kabla ya kwenda kuziuza ZSTC na baadea kuuhifadhi unga unabakia baada ya karafuu kuchungwa.

“Mazungumzo ikiwa yataenda vizuri basi mti wa mkarafuu utakua ni mali, majani, makonyo, karafuu, unga wenyewe vyote vinanunuliwa, kilichobakia wakulima kuendelea kuuza karafuu zenu ZSTC,”alisema.

Akizungumzia suala la mezani za kietroniki, alisema tayari shirika limeshafunga mezani 10 katika vituo vyate vikubwa na litaendelea kufunga kwenye vituo vilivyobakia, ili kuondosha changamoto za wakulima juu ya kilio hicho.

Kwa upande wa karafuu alisema asilimia 65 ya karafuu zinazalishwa mkoa wa kusini Pemba ikiongzwa na Wilaya ya Mkoani, ambapo watu 37,000 walitembelea kwenye vituo vya ZSTC kwa msimu uliopita.

Hata hivyo alisema wakulima wengi wa karafuu wamekua na imani na ZSTC, hivyo aliitaka kampuni ya Tigo Zantel kufanya kazi kwa uaminifu, ili wakulima kuwaamini kama walivyofanya kwa ZSTC.

mapema afisa mdhamini Wizara ya Biashara na maendeleo ya Viwanda Pemba Ali Suleiman Abeid, aliwashauri wakulima hao kuendelea kupokea fedha zao kwa kutumia mitandao ya simu na benk.

“Tokea Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Miwnyi, kuruhusu wakulima wenye pishi moja hadi gunia moja kulipwa pesa mkononi, kumeibuka mtindo kwa wakulima, hata kama anagunia 10 atauza mojamoja ili kupata fedha mkononi jambo ambalo sio sahihi, ”alisema.

“Tulishafanya mazungumzo na wenzetu tigo Zantel na tayari wameshakubali kufanya miamala yote, pamoja na kuhakikisha watu wanalipa kwa wakati na sio kuchelewesha,”alisema.

Aidha aliwasihi wakulima, kuitumia huduma hiyo ya tigo Pesa kwa ajili ya kuingiziwa malipo ya karafuu, huku akiwataka watendaji wa kampuni hiyo kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwa wateja.

Hata hivyo mdhamini huyo, aliitaka kampuni ya tigo Zantel kuboresha mifumo yao ya mawasiliano ya mtandao, kwani mkulima anapotoka kituoni tayari fedha zake anapatiwa hapo hapo.

Nae Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Zanzibar Ali Suleiman Mussa, alisema huduma za kifedha duniani sasa zinapitia kwenye mitandao ya simu, kwa ajili ya usalama wa fedha wenyewe kuwa sehemu salama.

“Katika msimu wa mavuno ya karafuu kuna na watu wengi hujuwi yupi mwema au mbaya, wengine wanakazi ya kuangalia mkulima amepata kiasi gani ili wamuibie, lakini unapoweka kwenye simu zinakua salama,”alisema.

Kwa upande wake meneja TigoPesa Zanzibar Salum Nassor Mohamed, alisema lengo la mkutano ni kukutana na wakulima kusikiliza changamoto zao, ili kuweza kuzitatua na wakulima waweze kupata fedha zao kwa wakati muwafaka.

Alisema kampuni ya tigo Zantel inaimani kubwa na ZSTC na wamejipanga, kuhakikisha kufanya vizuri katika suala zima la malipo ya karafuu kwa kutumia mtandao.

Nae meneja wa TogoPesa Pemba Farouk Ahmed, alisema misimu miwili walikua katika changamoto ya mfumo wa mawasiliano, ila kwa wasasa wameboresha kupitia minara yote.

Nao baadhi ya wakulima, wameukubali mfumo huo wa malipo kupitia mitandao ya simu, lakini wameitaka kampuni hiyo ya simu kuhakikisha changamoto za ujeleweshaji wa kupokea fedha, unaondoka kwani mkulima baada ya kuuza hutaka kupata pesa zake pale pale.

Kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 Shirika lilipanga kununua tani 4,940 za karafuu kavu kwa gharama ya shilingi bilioni 69.1, ambapo bei ya kununulia karafuu iliyokadiriwa kuwa ni wastani wa Shilingi 14,000 kwa kilo moja.

Aidha hadi kufikia Machi 2023, tayari shirika limenunua jumla ya tani 3,917.28 za karafuu kwa thamani ya shilingi bilioni 52.1, sawa na asilimia 75 ya makadirio kwa miezi tisa

MWISHO