Sunday, November 24

Vijana watakiwa kuzichangamkia fursa zinazotolewa serikalini

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, akizungumza na vijana wa mikoa miwili ya Pemba kwenye maadhimisho ya siku ya siku ya vijana duniani Kisiwani Pemba yaliofanyika katika viwanja vya shamemata Wilaya ya Micheweni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

NA ABUU BAKAR, ZU

VIJANA nchini, wametakiwa wajikombowe kimaisha, kwa kuzichangamkia fursa mbali mbali zilizopo katika taasisi mbali ikiwemo zile za serikali kuu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana kimataifa, katika uwanja wa mpira wa Shamemata wilaya ya Micheweni.

Alisema, ni jukumu la vijana ni kuzitumia fursa zinazotolewa na serikali yao, ili kujikwamua na hali ngumu za kimaisha inayowakabili.

Aidha mkuu huyo, aliwasihi vijana kuwa wabunifu kwa kuzitumia fursa za mazingira, uzalishaji wa chakula, upandaji wa miti, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kujipatia ajira, ili kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo aliwataka vijana, wenye mikopo ya UVIKO 19 kuweza kuirejesha, ili wengine waweze kupatiwa mikopo hiyo, kufanya hivyo kutaifanya serikali kuweza kutimiza malengo yake kwa vijana katika kuwainuwa kiuchumi,

“Nawasihi ndugu zanguni vijana munapaswa kujitambuwa, musije mukatumika vibaya, mukaharibu malengo yenu, serikali yenu inafanya kila njia ili kuona inawasaidia vijana wake katika kuwainua kiuchumi,” alisema.

Alisema uwepo wa kituo vya wajasiriamali mjini Ole na Pujini vimejengwa kwa lengo kuwakomboa vijana, ili kuwafanya wawe wajisiriamali watakao piga hatua kimaendeleo.

Akizungumzia program ya vijana ya Mkoa wa kaskazini Pemba ya ‘zinduka’ alisema program hiyo itawasaidia vijana wa mkoa huo, kufanya kazi kwa pamoja, bila ya ubaguzi wa aina yoyote, kwa kuyaondosha makundi ya vijana wanaojishughulisha na ulevi, wizi na vitendo vya udhalilishaji.

Nae kaimu mkuu wa wilaya ya Micheweni, ambae ni mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Bakar Omar, aliwataka vijana kuyazingatia maadili ya kizanzibari, ili kujiepusha na vitendo vinavyoweza  kuwapelekea kuingia matatani.

MKUU wa Wilaya ya Wete Dr.Hamad Bakari Omar, ambaye ni kaimu mkuu wa Wilaya ya Micheweni, akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya siku ya vijana duniani Kisiwani Pemba yamefanyika katika viwanja vya shamemata Wilaya ya Micheweni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

Hata hivyo aliwasihi vijana, kurejesha maadili ya kizanzibari, kwa kufuata  mila na silka na tamaduni ambazo zitawaepusha kuingia katika matatizo, yatakayo pelekea kutokufikia ndoto zao za kimaisha.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini wizara ya Habari, Vjana, Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau, alisema ujumbe wa siku ya vijana 2023 “elimu na ujuzi wa kijani kwa vijana kwa maendeleo endelevu ya taifa”  kauli hiyo inalenga  kuwamairisha vijana kitaaluma.

AFISA Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani Kisiwani Pemba yamefanyika katika viwanja vya shamemata Wilaya ya Micheweni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

Hata hivyo aliwataka vijana kuhakikisha wanakua makini, kwani tayari kuna baadhi ya watu wamekuwa wanachafua umoja wa vijana kwa kuwadanganya wananchi kuna ajira, jambo ambalo sio sahihi.

Mapema akisoma risala ya Vijana Omar Dawa Juma, aliishukuru serikali ya, kwa kuwapatia mikopo nafuu, ambayo imewapatia maendeleo makubwa na kuwasaidia kuwainua kiuchumi.

VIJANA wa Sarakasi kutoka kiuyu mbuyuni Micheweni, wakionyesha moja ya fani za uchezaji wa sarakasi kwa kupita katikati ya ringi lenye moto, wakati wa maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani, Kisiwani Pemba maadhimisho hayo yamefanyika Viwanja vya Shaame Mata Wilaya ya Micheweni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
WASANII wa kikundi cha mziki cha maswaga Fress kutoka Wilaya Wilaya ya Chake Chake, wakiimba wimbo maalumu wa vijana kuelekea maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani, Kisiwani Pemba maadhimisho hayo yamefanyika Viwanja vya Shaame Mata Wilaya ya Micheweni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 MWISHO