NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amesema, ujumbe wa siku ya vijana duninia mwaka huu, umeonyesha umuhimu wa elimu na utunzaji wa mazingira kwa vijana, hivyo ni wajibu wao kuufanyia kazi kwa vitendo.
Alisema, iwapo vijana watapatiwa elimu na ujuzi wa mazingira kwa ajili ya kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wataweza kusaidia sana kutunza mazingira yaliyowazunguka na kuwanufaisha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni Mkuu huyo alisema fursa zinazotokana na mazingira ni nyingi, hivyo kuna haja kwa vijana kuhakikisha wanazitumia ipasavyo ili kujikomboa.
Alisema kuwa, kaulimbiu ya siku hiyo ambayo ni ‘Elimu na Ujuzi wa kijani kwa vijana kwa maendeleo endelevu’ inahimiza vijana kuzitumia fursa za kimazingira, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa chakula, upandaji wa miti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Sote ni mashahidi ujumbe wa mwaka huu unatusisitiza sisi vijana, kutumia fursa ambazo tayari wameshaziandaa na zile ambazo wanazozihitaji na kuhakikisha Srikali inawasaidia,” alisema.
Aidha aliwasisitiza vijana hao kuchangamkia fursa mbali mbali zinazopatikana nchini, ili kuweza kujipatia ajira zinazotokana na uchumi wa kijani kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia suala la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika Mkoa wake, alisema miti 1,573,669 ya aina mbali mbali ikiwemo ya matunda na viungo imepandwa kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023.
Alisema, lengo la kupandwa miti hiyo ni kukabiliana na athari za ambazo zimekua zikiendelea kutokea siku hadi siku, hivyo suala la upandaji wa miti linapaswa kuwa endelevu, ili kurudisha uwoto wa asili uliopotea.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Pemba Mhandisi Idris Hassan Abdalla alisema, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, suala la upandaji wa miti ni jambo endelevu ndani ya kisiwa cha Pemba.
Nae Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba Mwalimu Khamis Mwalimu alisema, ukataji wa miti unapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote, ili kukabiliana na athari za kimazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba Mwalim Khamis Mwalimu, alisema hadi sasa Zanzibar kuna maeneo 148 ambayo yaningia maji chumvi na 123 yapo katika kisiwa cha Pemba na 25 yako Kisiwa cha Unguja.
Alisema wananchi walijisahau kipindi cha nyuma kuwa ukataji wamiti unapelekea uharibifu wa mazingira na maeneo kubakia wazi hali ambayo kwa sasa maji yamepata mwanya.
“Kama tungekua na utamaduni baada ya kukata miti tunairudisha kwa kuipanda mengine, basi ingesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuwia maji ya bahari kuingia katika maeneo ya wananchi ikiwemo sehemu za kilimo,”alisema.
Nae mkurugenzi wa chama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania (JET) John Chikomo, alisema jukumu la uhifadhi wa mazingira ni wananchi wote, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mstari wambele katika suala zima la utunzaji wamazingira kwa kuachana na ukataji wamiti.
MWISHO.