Sunday, November 24

VIONGOZI VYAMA VYA SIASA PEMBA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU SERA YA JINSIA KATIKA VYAMA VYAO.

AMINA AHMED MOH’D, PEMBA. 

ZAIDI  ya Viongozi 15 kutoka vyama mbali mbali vya Siasa  kisiwani  Pemba wamepatiwa Mafunzo maalum   kujengewa uwezo juu ya Kuanzisha na kuifanyia  kazi Sera ya jinsia Katika Vyama Vyao.

Mafunzo hayo ya Siku moja yaliondaliwa na Chama  cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Jumuia ya Utetezi wa kijinsia  na Mazingira Pemba  PEGAO   yamefanyika Leo katika ukumbi wa Chama hicho Mkanjuni Chake Chake.
 Akizungumza katika Mafunzo hayo Mratibu wa chama hicho Pemba Fat-hiya Mussa Said Amesema lengo la Mafunzo hayo kwa Viongozi wa vyama vya Siasa ni  kusaidia Kuongeza  ushiriki wa  wanawake Katika Demokrasia kwa kufuata Utaratibu maalum utakaotambulika kisheria, kusimamiwa pamoja na kuweza kutekelezwa  kupitia  Sera ya Kijinsia  ndani ya Vyama.
” Baada ya kuona Changamoto kubwa ndani ya Vyama vya Siasa ni kukosekana kwa Sera ya kijinsia, na Vile ambavyo vimebahatika kuwa na Sera  basi haviitekelezi Tukaona ipo haja ya kuandaa Mafunzo haya ili kupeana miongozo jinsi gani tunaweza Kuandaa Sera ya jinsia ambazo zitasaidia  Kupatikana usawa  kwa Wanawake na wanaume katika Vyama”Alisema.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa  Jumuia ya Pegao  Hafidh Abdi Said  amewataka viongozi hao kuyafanyia kazi kwa vitendo Mafunzo hayo ili kuweza kuleta matokeo chanya katika vyama vya siasa ambayo yatatokana   na kuanzishwa kwa sera  ya jinsia ambayo imezingatia usawa wa Kijinsia  na ushiriki  na upatikanaji wa fursa sawa kwa vitendo.
 “Haya mafunzo malengo yake ni kupata Mabadiliko  ndani ya vyama tunahitaji zile changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wanawake zilizomo ndani ya vyama  vya siasa zinazowarudisha nyuma kugombea uongozi zisijitokeze tena”.
“Turudi katika jamii zetu  tukashauriane  tuwashirikishe ili kuona ni kwa namna gani vyama vyetu vinakuwa na sera ya  kijinsia , isiwe Maneno matupu tunataka mabadiliko kuona wanawake na wao  wanapata fursa ya kugombea uongozi kwa Miongozo ya kisera iliyomo ndani ya vyama”alisema Mkurugenzi Pegao.
Sabah Mussa Said  ni mkufunzi katika mafunzo hayo pamoja na mambo mengine  amesema Kupatikana kwa Sera ya kijinsia katika vyama vya siasa kutasaidia kuondosha ubaguzi na unyanyasaji wa aina zote ambao hujitokeza kutokana kukosekana au kushindwa kupewa vipaumbele  kwa sera hizo ndani ya yyama  .
Wakizungumza baadhi ya viongozi walioshiriki mafunzo hayo akiwemo  Muhammed Haji Kombo Mwenyekiti Wa chama cha wananchi CUF  Mkoa wa Kusini  Pamoja na Hamiar Ali Said  kutoka chama hicho Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema chama kitaendelea kulinda na kuendeleza haki na upatikanaji wa  fursa sawa  kwa Wanawake na  wanaume.
 Raya Juma Othman pamoja  na Rufea Muhammed Saleh  Viongozi kutoka chama cha wakulima AFP wamesema  katika kuona wanawake wanapata fursa sawa katika kushiriki michakato ya uongozi  wataendelea kuyafanyia kazi mafunzo hayo ya Sera ya kijinsia kwa kushirikiana na Viongozi wa juu zaidi  ndani ya chama chao kuanza mara moja mchakato wa kuanzisha Sera ya Kijinsia.
 Mafunzo hayo ya siku moja ya  kuwajengea uwezo viongozi wa vyama mbali mbali vya siasa  yalitoa fursa ya  kushiriki kwa Pamoja katika kuitolea Ufafanuzi    mada  ya Sera ya jinsia katika vyama vya Siasa.
Mwisho.