NA FATMA HAMAD PEMBA,
Ukosefu wa huduma za maji safi na salama, bado ni kilio kikubwa kwa wananchi wa kijiji cha Mjini kiuyu Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazi Pemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kijijini kwao, mwananchi Bikame Bakar Darusi, alisema huu ni mwaka wa tano sasa wamekua wakikosa huduma hiyo ya maji safi na salama.
Alisema wamekuwa wakipata tabu kwani wanashindwa kupata maji ya kutosha ya kufanyia shughuli zao za nyumbani.
‘’Tunashindwa kupata maji hata ya kuwakoshea watoto wetu’’alieleza mwanachi Bikamae.
Aliendelea kusema kuwa watoto wao wanakwenda skuli na uchafu kutokana na kadhya hiyo.
Kwa upande wake Bakar Hamad alisema suala la maji limekua ni tatizo sugu, ambalo linawatesa wanawake wa kijiji hicho.
Alisema siku yanayotoka maji kwa baadhi ya mabomba hutoka kuanzia sa tano hadi tisa za usiku, hali ambayo inapelekea wamama kukesha kwenye foleni ya maji.
‘’Hakuna hata mwanamme mmoja anaelala na mke wake wakati wa usiku, kwani wanawake hulala kwenye foleni za maji’’ alieleza mwananchi Bakar.
Mapema Fatma Khalfan Suleiman alisema kuwa ukosefu wa maji unaweza ukapelekea wananchi wa kijiji hicho kupata maradhi hatarishi yatokanayo na uchafu.
‘’Hatupati maji tukaweza kusafishia vyoo pamoja na nyumba zetu’’
Nae Ali Masoud alisema wananchi wa kijiji hicho wameanguka kiuchumi kwani, hawapati maji ya kumwagilia mazao yao.
‘’Kazi yetu kubwa sisi ni kilimo cha mboga mboga ila kwa sasa kimetushinda, tunateseka na watoto,’’ alisema Ali Masoud.
Hivyo wameitaka wizara husika kukiona kilio chao ili waweze kuondokana na kadhya hiyo.
Fatma Ali na Asha Juma wanafunzi wa darasa la tano walisema wanakosa kusoma masomo ya vipindi vya mwanzo darasani kutokana na kuchelewa kwenye kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Afisa uhusiano wa mamlaka ya maji [Zawa] Pemba Suleiman Anas Masoud, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kijiji hapo.
Alisema tatizo hilo linasababishwa na kukosekana kwa matangi pamoja na uchakavu wa miundombinu ya kusambazia maji.
Hivyo amewataka wanachi hao kuwa na subra, kwani tayari wameshaingizwa kwenye mradi mpya ambao, unamaliziwa kufanyiwa upembuzi yakinifu, unaofadhiliwa na Bank ya watu wa ujerumani, ambao utajenga matangi kwenye vijiji vilivyo na shida ya maji.
MWISHO.