NA FATMA HAMAD-PEMBA.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud, amezitaka asasi za kiraia kushirikiana kwa Pamoja na kuwajengea uwezo Watoto wa kike walioacha Skuli ili waweze kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo katika mkutano wa kuutambulisha mradi wa Malala, utakaoendeshwa na Zafela visiwani Zanzibar kwa muda wa mwaka mmoja, kikao hicho kilichowajumuisha asasi mbali mbali za kiraia kisiwani Pemba.
Alisema katika utafiti wao walioufanya waligundua kuwa ,kuna wimbi kubwa la watoto wa kike wamekuwa wakikatisha masomo yao kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo kuolewa, kupata mimba za utotoni pamoja na kufanyishwa kazi za nyumbani.
Alisema wamekuwa wakipokea kesi nyingi za Watoto wa kike, kudai haki zao, aidha waliolewa au waliojihusisha na mahusiano, ambao ukiwangalia umri wao unapaswa wawe wako shuleni na wanaendelea na masomo yao.
‘’Tumeamua kuleta mradi huu wa Malala kwa ajili ya kumuezesha na kumsaidia mtoto wa kike ili aweze kurudi shule na kumaliza masomo yake angalau hadi darasa la kumi na mbili,’’alisema mkurugenzi.
Alifahamisha kuwa mrahidi huo umelenga kuwafikia jumla ya Watoto 3,000 kwa Unguja na Pemba, hiyo amezitaka asasi za kiraia kuweka mashirikiano makubwa na jumuia ya Zafela ili kuona mradi huo umefikia malengo.
Aidha kwa upande mwengine mkurugenzi aliwataka wanajamii kukaa karibu na watoto wao na kuwasikiliza matatizo yao, ili wawe na uthubutu wa kueleza changamoto zinazowatokezea katika harakati zao za kimasomo.
‘’Inawezekana mtoto anaacha Shule kutokana na vikwazo tu vinavyo mkwaza aidha njiani au shuleni, hiyo tujenge urafiki na Watoto wetu ili tuwanusuru na kadhia kama hizo,’’ alifahamisha mkurugenzi.
Mapema msimamizi wa mradi huo Hairun Abass Rajab kutoka Chama Cha Wanansheria wanawake Zanzibar [ZAFELA] Alieleza kuwa hadi sasa bado zipo familia ambazo hazimpi fursa mtoto wa kike kupata haki yake ya elimu kuanzia Msingi hadi Vyuo vikuu.
Alifahamisha kuwa lengo la mradi huo nikuwasaidia Watoto walioacha Shule, na waliokatika mazingira magumu, ili kuhakikisha wanapata elimu na kufikia ndoto zao.
Akichangia katika mkutano huo mwanaharakati wa kulinda na kutetea haki za wanawake na Watoto kutoka wilaya ya Mkoani Sada Moh’d Othman alisema ni vyema kuweko na mkakati Madhubuti ya kuwaekea usimamizi wa hali ya juu wanafunzi hao wakati watakapo rudi shuleni ili kunusuru vitendo viovu na waendelee na masomo yao.
‘’Kuna Watoto waliokaa nje kwa muda mrefu, na tayari walisha athirika na ulevi, ulawiti, ubakaji, hivyo ni vyema tuwe makini nao, wakati tunapowarejesha shuleni, ili wasije wakambukiza na wengine,’’alifahamisha mwanaharakati.
Nao washiriki Ali moh’d Ali na Salim Said walisema ili kumaliza vitendo viovu katika jamii, ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake kuchukua jitihada za makusudi, jambo ambalo litasaidia kupata kizazi chenye madili mema.
MWISHO.