Wednesday, January 15

Andikoni kijiji kilichohaulika chakosa huduma muhimu za kijamii

barabara ya kuingia katika kijiji cha andikoni kabla ya kutengenezwa

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WILAYA ya Mkoani ni moja kati ya Wilaya Mbili zilizomo ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba, iwemo Wilaya ya Chake Chake ambapo naweza kusema ndio mji mkuu ndani ya Kisiwa cha Pemba.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi Tanzania 2022, Mkoa wa kusini Pemba una idadi ya wananchi 271,350 Wilaya mbili Mkoani na Chakle Chake, ambapo shuhuli kuu za wananchi wa Wilaya hizo, Uvuvi, kilimo, biashara na ufugaji.

Wilaya ya Mkoani ina shehia 36, moja ya shehia zilizomo ndani ya ni Chumbageni Wambaa, yenye idadi ya wananchi 5220, Wanawake 2112 na wanaume 3108 huku vijiji tisa (9) vikunda shehia hiyo.

Miongoni mwa vijiji hivyo ni pamoja na Andikoni, Ndogoni, Kigongo, Maliamuke, Mpopooni, Chumbageni, Sinongone, Tumbi na Kidutani.

Kijiji cha Andikoni shehia ya Chumbageni kina wakaazi 477 na wastani wa nyumba 52 shughuli kuu za wananchi wa kijiji hicho uvuvi, kilimo na ufugaji.

Kwa muda mrefu kijiji hicho kilikosa huduma mbali mbali za kijamii na maendeleo, ambazo zingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kubadilisha maisha ya wananchi hao.

Mwandishi wa makala haya alilazimika kufunga safari hadi kijijini andikoni, kujionea uhalisia wa mambo ulivyo kijijini hapo na sio kusikia kwa wananchi.

WANANCHI WA ANDIKONI WANASEMAJE.

Mwanakijiji cha Andikoni Mohamed Juma, anasema wakati umefika umefika kwa kijiji chao, kuanza kunufaika na matunda ya serikali ya awamu ya nane Zanzibar, ikiwemo barabara ya kisasa.

Anasema tokea kijiji hicho kuasisiwa hadi hasasa, hakijawahi kuwa na huduma yoyote ya kijamii, ambayo wananchi wanaweza kuipata kama ilivyo kwa vijiji vyengine.

“Sisi hapa huduma zote unazozijua wewe, tunaposema barabara umeona hali ilivyo shuhuli kipindi cha mvua hata wanafunzi hawatakwenda skuli,”amesema.

Amezitaja baadhi ya huduma ambazo wamekua wakizikosa au kuzifuta maeneo mengine, ni pamoja elimu, afya, maji na umeme, hali inayowafanya baadhi ya akinamama kujifungulia njiani.

Anasema muda wa skuli unapofika kila mzazi anakua na gamu mtoto wake mdogo kumruhusu kwenda skuli, kutokana na mazingira anayopitia barabara kutokua rafiki kwao.

“Watoto wanalazimika kutembe kilomita mbili, kutoka andikoni hadi sisimizini skuli iliko, kipindi cha mvua ndio mtihani kabisa, wazazi wote wanajawa na hofu kutoka na ubovu wa barabara yao,”amesema.

Kwa upande wake Tatu Juma Haji, alisema wanakumbana na changamoto kubwa ya kujifungulia njiani, kutokana na ukosefu wa barabara kijiji kwao, pamoja na umbali wa vituo vya afya vilipo.

“Sisi hapa urahisi bora mtu apitie baharini hadi hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, kwa huku kwetu utazaa njiani, kwani tayari matukio hayo yameshatokea,”amesema.

Nae Tatu Juma Haji mkaazi wa andikoni, anasema changamoto ya kutokuwepo kwa kituo cha afya karibu na kijiji chao, wanalazimika kufuata Mtambile au Wambaa, inapelekea baadhi yao kujifunguliwa njiani, kutokana na umbali wa kufuata huduma hiyo ikizingatiwa barabara sio nzuri.

“Mimi hapa mimba moja nimejifungulia njiani na moja nimejifungulia nyumbani, usiku usafiri unaupata wapi, wenyegari wanatupa masharti kama gari unataka kuinunua wewe, sababu barabara sio rafiki na kituo cha afya kiko mbali,”amesema.

“Urahisi wetu kila kitu bora mtu apitie baharini hadi hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, au mkoani moja kwa moja kwenda kufuata huduma zote za kijamii, boda boda pia ni shida kufika,”amesema.

Anasema changamoto nyengine ni umbali wa skuli kutoka andikoni hadi sisimizini, hali inayowafanya watoto wakati mwengine wanafika vipindi vimeshaanza.

Anasema kipindi cha jua watoto wanawakuta wamelala njiani, kama watoto wanaosoma maandalizi alfajiri ngumu kuwaamsha kila mtu anaogopa na kurudi ndio mtihani.

Kwa upande wake Omar Khamis Shehe, alisema suala la umeme kijijini kwao ni ndoto kubwa, kwani wanalazimika kufika vijiji vya jirani kwa ajili ya kujaza chaji siku zao.

“Sisi hapa kama tunahitaji kujaza chaji simu zetu mpaka tufike kijiji cha jirani tukaombe na ikijaa mtu anarudia nayo, huu ni usumbufu na sisi tunataka kuangalia taarifa za maendeleo ya nchi yetu,”amesema.

WANAFUNZI WANASEMAJE NAO

Mwanafunzi wa darasa la sita (STD 6) Heri Khamis Makame, anasema changamoto kubwa kijiji ni barabara, kipindi cha mvua wanapata shida kwenda kubwa skuli Tumbi, kwani hulazimika kutumia muda mrefu kwenda skuli wakati mwengine wanapofika mwamuli ameshaanza kusomesha.

“Kuna baadhi ya siku tunapelekwa skuli na wazazi wetu, kutokana na kuogopa njiani tunamopita kwani baadhi ya wakati hukumbana na vijana tukiofia kufanyiwa vitendo viovu,”amesema.

Anasema barabara ndio kila kitu kwenye sehemu yoyote, inapokuwepo basi maendeleo mbali mbali yataweza kupatikana tena, ikiwemo kurahisisha usafiri wa wanafunzi kwenda na kurudi skuli

Nae Mwanafunzi Zainab Khamis Kombo, anasema kipindi cha mvua wanalazimika sare safi kuzitia ndani ya mikoba yao na kuvaa nguo zilizokua sio rafiki, ili kuepuka kuchafuka kutokana tope barabarani wakifika skuli wanavua na kuvaa nguo zao safi.

Anasema zipo changamoto nyingi ambazo bado wanataji kutatuliwa, ikiwemo umeme, kituo cha afya, maji, kwani maji kwa sasa wanalazima kwenda mabondeni kuteka

“Wakati mwengine tunaporudi skuli wazazi wanatuonea huruma, baadhi ya vitu wanatusaidia ikiwemo maji sehemu tunayoenda kuteka sio rafiki mbali halafu bondeni ikizingatiwa wakati mwengine maji yanakua na chumvi chuvi kutokana na ukaribu wa bahari,”amesema.

WIZARA YA UJENZI MAWASILIANO NA UCHUKUZI

Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, amesikitishwa na hali ya barabara kijijini hapo ilivyo na kuahidi kwa hatua ya kwanza barabara hiyo itasafishwa, ili iweze kupitika wakati wote na ujenzi wa barabara za ndani, utakapofika basi nayo kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, akizungumza na wananchi wakijiji cha andikoni juu

Amesema barabara ni moja ya kichochote cha maendeleo ya sehemu yoyote, hivyo wananchi wa andikoni hivi karibuni wataweza kuondokana na usumbufu wote waliokua wakiupata.

“Nitahakikisha hatuchukuwi muda mkubwa tunakuja kusawazisha kila kitu, nyinyi wenyewe mutafuraji serikali inapoahidi basi hutekeleza ahadi zake tena kwa vitendo ndio kama wizara yetu,”amesema.

SHIRIKA LA UMEME ZANZIBAR (ZECO

Mkuu wa Idara ya Ufundi wa Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ Pemba Mohamed Ali Juma, amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 watahakikisha huduma ya umeme, inafikishwa kijijini hapo.

“Huku lazima tuweke tansfoma ili huduma iweze kupatikana kwa urahisi, lazima uvuke kupitia baharini na tutahakikisha huduma itafika, iwapo barabara itakua nzuri,”amesema.

MAMLAKA YA MAJI ZANZIBAR (ZAWA)

Fundi Mkuu wa Mtandao wa Maji Pemba Injinia Juma Omar Khamis, amesema kwa hatua za harakaharaka tayari mewasiliana na taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, kwa ajili ya kuwasaidia kisima na ZAWA kujenga mnara wa tenki la lita 10,000 ili wananchi wanaondokane na shida ya maji.

“Kwa sasa wananchi wanatumia maji ya kisima walivyochimba wenyewe, maji hayo wanatumia kwa kunywa na kufanyia shuhuli mbali mbali za kijamii, ili tukidhi mahitaji yetu ya kila siku,”amesema.

Amewataka wananchi wa kijiji hicho kuwa wastahamilivu na subra, huduma ya maji itatatuliwa kwa vitendo na waweze kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR

Afisa kutoka wizara hiyo Pemba Salum Kuza Sheikhan, amesema changamoto hizo wameanza kuzitatua kidogo kidogo na kuzipa kipaombele zaidi, watahakikisha banda linalojengwa na tutu linamalizwa na wizara husika.

Amesema tayari wanampango wa kuhakikisha wanajenga mabanda mengine kutoka tutu hadi msingi, ili wanafunzi watakaomaliza darasa la sita kijijini hapo ndio waweze kwenda skuli za sekondari.

“Kwa sasa juhudi zimeanza kuonekana katika jengo la tutu hapa kijijini, nguvu za wizara kuliezeka na wanafunzi januari waweze kusoma na kupunguza masafa kwa wanafunzi wa maandalizi kutembea masafa marefu,”amesema.

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Dr.Haji Bakar, amesema watajitahidi wanaongeza huduma matibabu wa wananchi wa kijiji hicho, ikiwemo MMAMA ambayo inawasaidia akinamama wajawazito.

Amesema iwapoa barabara itakua nzuri na yakupitika basi hakuna mazizi anateke jifungulia kijijini, kwa huduma ya MMAMA unapopiga simu tu ikiwa tayari kujifungua gari inakufuata hadi mlangoni kwako.

“Tunatarajia kuongeza watoa huduma wa mama wajawazito na watoto vijijini, ili mama wote wajawazito waweze kupatiwa matibabu kijijini kwao ili kuondosha changamoto zilizojitokeza ya kufuata huduma za afya maeneo ya mbali,”alisema.

VIONGOZI WA SERIKALI WANASEMAJE

Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, amesema kijiji hicho kinahitaji huduma mbali mbali za kijamii, tayari kilio chao kimeshafikishwa katika ngazi za juu na karibuni mafanikio yake yataonekana.

“Nawaombeni tuvumilie viongozi wameshasikia kilio cheni, nawahakikishia kila kitu kitabadilika na kua kama ilivyo vijiji vyengione vyenye huduma muhimu kama munazozihitaji nyinyi,”amesema.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema dhamira ya serikali ya awamu ya nane, ni kuona wananchi wanapata huduma bora, ikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafiri.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, akiondoka kijiji cha andikoni mara baada ya kumaliza kusikilicha changamoto za wananchi wa kijiji hicho.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

Alisema suala la barabara ni muhimu na atahakikisha ujenzi wa barabara ya Wambaa itakapofika na njia zote za ndani zitaweza kutengenezwa, kwa kiwango cha lami ikiwemo kijiji cha andikoni.

“Hivi karibuni wananchi wa andikoni nao wataanza kufurahia matunda ya serikali yao, pale changamoto zao mbali mbali zitakapoanza kutatuliwa na kwa kuanzia tutaanza na barabara ambyo ndio muhimu zaidi,”amesema.

Kunapokuwepoo na miundombinu imara ya barabara, basi huduma zote muhimu kwa wananchi nazo zitaweza kusogea ikiwemo umeme, maji, elimu na huduma za afya, barabara pia itarahisisha wananchi kusafirisha mazao yao na kupeleka sokoni.

NINI KIFANYIKE.

Kijiji cha Andikoni shehia ya Chumbageni kina wastan wa nyumba 52 na wakaazi 477, kwa sasa hakina huduma hata moja muhimu za kijamii, ni wakati wa kila taasisi kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo ahadi zao, ili wananchi wa kijiji hicho nao waweze kunufaika na matunda ya serikali yao.

Utakelezaji wa ahadi hiyo ndio utaweza kubadilisha maisha ya wananchi wa kijiji hicho, ikiwemo kuwafanya watoto waweze kusoma hata muda wa ziada usiku ili kuinua ufaulu wa wananchi wa kijiji hicho.

                      MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari Portal
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355