Sunday, November 24

Machungu ya wakulima wa mwani kumezwa na ZSCO

KAIMU Mratibu kampuni ya mwani ya serikali ZASCO Ofisi ya Pemba Khadija Zahran Mohamed, akizungumza na wakulima wa mwani kutoka kijiji cha kukuu kangani na Mwambe, katika ziara ya kutembelea vikundi vya kilimo hicho na kusaidia kutatua changamoto zao zinazowakabili ikiwemo vifaa na mbegu.

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

KAIMU Mratibu wa kampuni ya mwani ya Serikali Zanzibar (ZSCO) ofisi ya Pemba Khadija Zahran Mohamed, amesema kampuni ya mwani ya serikali imekuja kuondosha manyanyaso wanayoyapata wakulima wa zao hilo, wakati wanapokwenda kuuza mwani kwenye makampuni binafsi.

Alisema kuna baadhi ya wakulima walifika kuambiwa mwani wao ni mpeta, sababu sio wakulima wanaosaidiwa vifaa na kampuni hiyo, hali iliyopeleka kushindwa kununuliwa mwani wao.

Hayo aliyaeleza wakati alipokua akizungumza na wakulima wa mwani katika kijiji cha Kukuu Kangani wilaya ya Mkoani, wakati wa ziara ya kutembelea vikundi vya kilimo hicho na kusaidia kutatua changamoto zao zinazowakabili ikiwemo vifaa na mbegu.

Alisema uwepo wa kampuni hiyo itahakikisha mwani wote unanunuliwa na serikali, huku akiwataka wakulima kuendelea kulima kilimo hicho, kwani kiwanda kitakapoanza kazi basi kitanunua mwani kwa mwingi.

“Wapo waliopatiwa vifaa vya kulimia na kubeba mwani, hawa sasa wanapaswa kulima kwa wingi, wale ambao bado tutahakikisha kupitia kampuni hii nao wanapatiwa,”alisema.

Aidha aliwataka wakulima hao kuhakikisha wanashirikiana na serikali, pale itakapoanza kunua mwani, suala la bei linaweza kubadilika, kama ilivobadilika awali kutoka shilingi 700 hadi shilingi 1000 na inaweza kufikia hata shilingi 2000 kwa kilo.

Kwa upoande wake mkulima wa zao hilo Mwadini Hassan Mohamed, alisema kampuni za mwani, zinawanyanyasa baadhi ya wakulima wa mwani, kutokana na kuwepo kwa wakulima wanaowapatia vifaa na mwani hununua kwao.

“Mimi ninamwani ndani moja sina sehemu ya kuuza, nikienda kwenye kampuni wananiambia subiria kwanza, mpaka wauze watu wao wanawapatia kamba tena mtu anauza kilo 50, sisi wenye tani mara unaambiwa mwani wako hauna kiwango,”alisema.

Alisema iwapo kampuni ya mwani ya serikali itakua tayari basi itakuwa ndio kimbilio lao sio kwa kampuni ambazo haziwathamini.

Aidha aliyomba serikali kuwapatia vifaa vya kulimia mwani, ikiwemo kamba za aina zote, pamoja na vihori kwa ajili ya kubeba mwani huo.

Nae Mkulima wa mwani Taifa Shaali Makame, alisema kampuni itakapoanza inapaswa kuongeza bei, kwani iliyopo sasa ya kilo shilingi 1000 ni ndogo kutokana na nguvu kubwa wanayoitumia katika kilimo hicho.

“Changamoto kubwa kwetu kampuni iliyopo inatunyanyasa sisi wengine ambao haijatusaidia vitu vyake, hata tunapokwenda kuuza wanatuambia tunawapa mpeta,”alisema.

Aidha naye Mkali Ali Suleiman, alisema wakulima wa mwani wanahitaji makoti ya mvua, viatu, miwani ya kuzamia chini ya bahari, kwani kuna baadhi ya wakulima wanalima mwani wakina kirefu cha maji.

Hata hivyo aliyomba serikali kuongeza bei ya mwani kutoka shilingi1000 hadi 2500, kutokana na gharama za vifaa kupanda bei na gharama za maisha kuwa ziko juu.

Shehia ya Kukuu Kangani inawakulima wa mwani wasio pungua 300, wengi wao wakiwa na mwani ndani ya majumba yao, baada ya kukosa sehemu za kuuza.

                            MWISHO