Sunday, November 24

Mradi wa heshimu bahari kutekelezwa Zanzibar

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MKURUGENZI Mkaazi kutoka Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani (USAID) Tanzania Craig Hart, amesema shirika hilo linaunga mkono shughuli zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samiia Suluh Hassana pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Husseina Ali Miwnyi, katika kuwapatia maendeleo wananchi wake.

Alisema katika kuunga mkono huko Shirika la USAID, limekua mstari wambele kusaidia huduma mbali mbali ikiwemo afya, elimu na hudumba nyengine.

Mkurugenzi Craig aliyaeleza hayo, wakati akizungumza na Wavuvi, wakulima wa mwani, kamati za uvuvi na wanajamii wa Kiijji cha Chwaka Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema mradi wa Heshimu bahari unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani USAID, umelenga kuimarisha mazingira ya bahari na viumbe vyake, katika maeneo ya hifadhi ili kukuza hifadhi ya bahari na kuongeza uzalishaji katika rasilimali za baharini na mazalio ya samaki.

Aidha aliyataja maeneo ambayo mradi huo unafanya kazi ni Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Tanga, Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es salaam pamoja na Mikoa yote ya Unguja na Pemba, ambao utagharimu Dola za kimarekani milioni 25 hadi kukamilika kwake.

Alisema anapenda kuona sehemu ambayo USAID inafanya kazi kwa karibu na kupitia mradi wa heshimu baharai, ili kusaidia katika sekta ya elimu, afya, shuhuli za kiuchumi.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema ziara hiyo ameweza kujifunza mambo mengi, ikiwemo changamoto za bahari kama vile uvuvi haramu, uvuvi ambao haupo Tanzania pekee bali dunia nzima

“Changamoto hiio sio kwa Tanzania pekee, pia katika nchi mbalimbali zilizoendelea uvuvi haramu upo, ni vyema tukazibiti hali hiyo na kuwa na uvuvi endelevu ambao kila mmoja ataweza kufaidika nao,”alisema.

Katika hatua nyengine mkurugenzi Hart, alisema amevutiwa na mandhari ya Zanzibar ambayo yamezungukwa na bahari, hivyo yanahitaji kulindwa ili wananchi waweze kuendelea kufaidika na rasilimali zilizomo baharini ikiwemo uvuvi na ukulima wa mwani.

“Mimi napenda sana Samaki na hata mke wangu anapenda sana mwani, kama hatutoilinda bahari samaki watakosekana, lakini pia mwani ni muhimu sana na unafaida nyingi mwilini,”alisema.

Naye Mratibu wa mradi wa Heshimu bahari, Sadiki Laiser alisema mradi umejikita katika kuimarisha sera zitakazosaidia serikali, sekta binafsi pamoja na jamii, kwenye kuimarisha, kuhifadhi, matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Alisema mradi huo ni wa muda wa miaka mitano, ambapo sasa unaelekea katika utekelezaji wake kwa awamu ya pili, ili kuboresha ustawi wa kiikolojia na uzalishaji wa maeneo ya viumbe hai wa baharini nchini Tanzania.

Aidha alifahamisha kuwa mradi huo pia unalenga kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi, wakiwemo wakulima wa mwani, wafugaji wa majongoo bahari na wavuvi, ili kuheshimu bahari na rasiliamli hiyo kuwa endelevu.

Wakizungumza katika mkutano huo, wakulima wa mwani wa kijiji Chwaka, walisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nyenzo zitakazowawezesha kufika katika mashamba yao ya mwani hususan kina kirefu cha maji.

Moja ya wakulima wa Mwani Khadija Juma Ame, alisema wanalazimika kuazimana vyombo vya usafiri wakati wanapokwenda kulima mwani, kwani wanakolima ni mbali na lazima wawe na usafiri wa uhakika.

“Hatuna usafiri wa uhakika wa kutufikisha katika mashamba yetu baharini, sisi wengine tumeamua kulima kina kirefu cha maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, tukipatiwa faida za kisasa tutazalisha mwani kwa wingi,”alisema.

Alisema kilimo hicho kinakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, yaliyotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo mkulima huyo, aliliomba shirika la USAID kusadia masoko ya nje ya zao la mwani, ili kuongeza thamani ya mwani zao ambalo ni mkombozi mkubwa wa wananchi hasa wanawake.

MWISHO