Monday, January 27

Wananchi wa Mjini kiuyu wataka wataalamu wa afya katika kituo chao .

Pichani ni kituo cha afya kilicopo kijiji cha Mjini kiuyu Wilaya ya Wete

NA FATMA HAMAD, PMBA

WANANCHI wanaoishi kijiji cha Mjini Kiuyu wilaya ya Wete Pemba,  wavunja ukimya na kutoa kilio chao  kutokana  baada ya kuwekeza nguvu kazi zao na fedha kwa  ajili ya kujenga kituo cha afya, ingawa kimeshindwa kutumika baada ya kukosa watalamu wa afya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi  kijijini hapo mwananchi  Khamis  Omar  alisema kuwa walitisha  mchango wa fedha, vifaa na nguvu kazi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Alisema kuwa kwa wakati huo kila nyumba ilitoa gharama kwa ajili ya ujenzi wa kiyuo hicho ingawa hadi sasa hakija tumika kama malengo yao walivyofikiria.

‘’Kuanzia mwaka 2011,ndipo ambapo kituo chetu hichi kilimalizika ujenzi wake ingawa hadi sasa hakitumiki na kimekaa mithili ya gofu,’’alieleza.

Nae Raya  Hassan  alisema huu ni mwaka wa 12 tokea kujengwa kwa kituo hicho, ambapo kilifunguliwa  kwa  mbio za mwenge,ingawa hadi sasa hakija tumika.

‘’Baada ya kuona tunapata tabu kwa kufuata huduma za afya masafa marefu, ndipo tukamua   kujitolea kujenga ili tuondokane na shida hiyo,’’alieleza.

Kwa upande Bikame  Bakar Darusi   alisema mtoto wake alijifungulia njiani wakati wanafuata huduma za uzazi kituo cha afya kilichopo Vitongoji.

‘’Tulitarajia kuwa fedha tulizozitoa, nguvu kazi na michango mengine juu ya ujenzi wa kituo hichi cha afya shida kama hii isingali tufika kama pengekuwa na watalamu,’’alifafanua.

Mapema Diwani wa wadi hiyo  Nassra Salum Mohamed alisema tayari wameshafuatilia kila sehemu ili kuona kituo hicho kinatoa huduma, lakini imeshindikana.

‘’Ijapokuwa kinajengwa kituo katika eneo la kiuyu Minungwini, lakini ni vvyema kuwangaliwe tena kwa jicho la pili, kwa vile kijiji cha mjini kiuyu ni kijiji cha ndani, na  hakuna  hata miundombinu  ya  barabara,’’ alieleza.

Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal Ali alifahamisha kuwa,kwa sasa hawana mpango wa kupeleka watalamu wa afya katika eneo hilo, kutokana na kuimarishwa kwa kutuo cha afya cha Kiuyu minungwini.

Alisema kuwa kwa sasa  jengo hilo linatumika kwa shughuli malumu kama vile mripuko wa maradhi pamoja na kipindi cha utoaji wa chanjo za watoto.

MWISHO.