NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
WANUFAIKA wa mkopo elimu ya juu, kutoka bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar, wamewataka wanufaika wenzao kuhakikisha wanarudisha fedha walizopatiwa wakati walipokua masomoni, ili fedha hizo ziweze kuwasaidia wanafunzi wengine.
Wamesema fedha hizo ziliweza kuwasaidia katika mahitaji mbali mbali wakati alipokua chuni, ikiwemo suala la ulipaji wa masomo kwa muda wote na mahitaji mengine.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika hafla ya kuwatunuku vyeti vya shukurani, kwa urudishaji wa fedha kwa wanufaika 28, hafla iliyofanyika katika banda la bodi hiyo ndani ya maonesho ya elimu ya juu Gombani kisiwani Pemba.
Mmoja ya wanufaika wa mkopo huo Kassim Shimeli, alisema fedha hizo zilimsaidia kuendelea na masomo ngazi ya Masta na sasa ameweza kurudisha tokea mwaka 2014 hadi 2021.
“Nilipata mkopo kutoka bodi hii, zilinisaidia sana katika masomo yangu, ila changamoto kubwa sikupatiwa fedha kwa ajili ya risachi yangu kitu ambachi kilinuumiza sana akilini mwangu,”alisema.
Aidha aliishauri bodi hiyo kuhakikisha wanatoa malipo kwa wakati, kama ilivyo bodi ya Tanzania bara ili kuepusha matatizo kwa wanafunzi wakati wanapokua masomoni.
Naye Hamidi Khamis Ali mnufaika wa mkopo kutoka bodi hiyo, alisema alianza kurudisha mkopo huo mwaka 2019 na kumaliza 2021, mkopo uliweza kumsaidia vizuri kwani bila ya mkopo angeshindwa kuendelea na masomo yake.
“Mimi binafsi kama nisingepata mkopo basi ningeshindwa kuendelea na masomo yangu ya elimu ya juu, ila mkopo umenisaidia kwa kiasi kikubwa sana,”alisema.
Aidha aliwataka wanafunzi wanaopata mkopo kutoka bodi ya mikopo ya elimu ya juu, kuhakikisha mikopo hiyo wanairudisha ili iweze kuwanufaisha wengine.
Mapema mratib wa bodi ya mikopo ya elimu ya juu Zanzibar ofisi ya Pemba Ahmada Omar Juma, alisema bodi hiyo iliundwa mwaka 2011 chini ya sheria Namba 3 sheria ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu Zanzibar mwaka 2011.
Aliyataja majukumu ya bodi hiyo ni kutoa mikopo ya elimu ya juu, kwa wanafunzi waliopata udahili wa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, kusimamia na kufuatilia urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, ili fedha hizo ziweze kutumika kuwasomesha wengine, kutoa nafasi za ufadhili za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nafasi ambazo hutolewa na Rais wa Zanzibar kila mwana.
“Wanaopata mikopo bila ya kurudisha mikopo yao, wanafunzi wengine itakua ngumu kupata fedha za kuwalipia, ndio tukawa tunashajihisha wanufaika kurudisha fedha,”alisema.
Nae afisa kutoka bodi hiyo Abdullazizi Mohamed Iddi, alisema katika maonesho hayo mwamko wa wanafunzi ni mkubwa na zaidi ya 300 wametembelea banda la bodi hiyo.
Alisema wameweza kuwasaidia wanafunzi katika maombi ya mikopo, ikizingatiwa muda wa kuomba mikopo hiyo umekaribia kumalizika huku akiwataka wanafunzi kuhakikisha wanajaza taarifa sahihi wakati wakuomba mikopo yao.
Kwa mujibu wa bejeti wa Wizara ya elimu mwaka 2023/2024, imesema jumala ya TZS 12,426,600,000 bilioni za ruzuku kutoka Serikalini, zilitengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo ya Elimu ya juu, ambapo hadi kufikia April 2023, jumla ya TZS 7.96 bilioni zilipatikana.
Aidha juma ya wanafunzi 4,875 wamepatiwa mikopo ya elimu ya juu wakiwemo, wanafunzi wapya 1,815 na wanafunzi 3,060 wanaoendelea na masomo, wanafunzi nne wapya wamepatiwa nafasi za ufadhili wa masomo nje ya nchi kutoka Serikali ya Ufalme wa Ras al-Khaimah.
MWISHO