RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kuanzisha mpango wa kupunguza kiwango kikubwa cha fedha zinazotumika nje ya nchi na badala yake zitumike ndani ya nchi.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alimpozungumza na uongozi wa mamkala hiyo iliyofika kwa lengo la kuwatambulisha mabalozi wapya wa kuitangaza taasisi hiyo kwenye ngazi ya viongozi wa kuu wa Serikali za SMZ na SMT, Mashirika ya Umma na taasisi nyengine za Serikali juu ya umuhimu wa kuendelea kuitangaza kwa umma.
Dk. Mwinyi alisema kwa miaka mingi Serikali ilikuwa ikikata bima nje ya nchi sasa TIRA imeleta mafaniko makubwa kwa kuokowa fedha nyingi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza mabalozi wapya walioteuliwa na TIRA kuendelea kuitangaza taasisi hiyo kwa viongozi wa umma wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Ahmeid Saidi, Mhe. Wanu Hafidh Ameir na Mhe. Japhet N. Hasunga wote ni Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware kwenye mazungumzo hayo alimueleza Rais Dk. Mwinyi mafaniko yaliyopatikana na TIRA kwenye Sekta ya Bima ikiwemo ongezeko la asilimia 1.68% kwenye pato la Taifa kwa mwaka 2021 kutoka asilimia 0.56% kwa mwaka 2020.
Pia alieleza taasisi hiyo imeendelea kuongeza gawio kwa Serikali kutoka mwezi Julai 2022 hadi Juni 2023 kwa kulipa gawio la Tsh. Bilioni 2.9.
Akizungumzia mafanikio kwenye sekta ya ajira, Kamishna Saqware alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba hadi Septemba 2022 TIRA ilitoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173 ikilinganishwa na 3,208 kipindi kama hicho mwaka 2021.
Mabalozi hao wa TIRA, waliteuliwa mwezi Februari mwaka huu, wakikabidhiwa majukumu ya kutoa ushauri kwa Mamlaka na sekta ya bima kwa ujumla kuhusu maendeleo ya sekta hiyo pia kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya bima katika ngazi mbalimbali ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi, Makatibu Wakuu wa SMT na SMZ, Mashirika ya Umma na taasisi nyengine.
Tangu kuteuliwa kwa mabalozi hao, tayari wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu umuhimu wa bima, kutoa elimu kwa umma wakiwemo viongozi wa Umma, wabunge, wawakilishi, makatibu wakuu, mashirika ya umma na viongozi wa taasisi nyengine kwa kuwa mstari wa mbele kuishauri Serikali kuhusu umuhimu wa ukataji bima wa mali za Serikali.
IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR