Wednesday, January 15

Chuo cha DMI chapiga hodi Pemba kufundisha usalama wa bahari

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MHANDISI Mkuu wa Meli kutoka chuo cha Bahari (DMI) Deism Danford Mlay, amesema chuo hicho kinakusudia kusogeza huduma zake ikiwemo kufungua tawi ndani ya kisiwa cha Pemba, ili wananchi waweze kunufaika na huduma mbali mbali zinazotolewa ikiwemo usalama la bahari.

Alisema sababu inayopelekea chuo hicho kufungua tawi lao ni kuwasaidia wananchi wa Pemba, pale vijana wanapomaliza masomo yao na kuhangaika katika kuchagua vyuo, ikizingatiwa jeografia ya maisha kwenda Tanzania bara ni ngumu.

Mhandisi mkuu wa Meli aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika maonesho ya vyuo vya elimu ya juu yaliyofanyika katika viwanja vya Gombani nje Wilaya ya Chake Chake.

“Pemba imezungukwa na bahari ikiwa na eneo kubwa la shuhuli za bahari, lakini uwelewa wa masuala ya usalama bahari upo kidogo, sababu kubwa vyuo vinavyotoa elimu viko mbali, hali ya maisha inakua ngumu mwanafunzi wa kawaida kusoma nje ya Zanzibar,”alisema.

Alisema DMI itaanza kufanya upembuzi yakinifu ili kupata eneo la kuendesha kosi, hivyo kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa DMI ipo tayari kushirikisha na wananchi wa Pemba katika kutoa elimu ya usalama na elimu ya meli kwa ujumla.

Aidha alifahamisha kwamba ili uwaeze kufanya vizuri katika sera ya uchumi wa buluu, lazima kutolewe elimu nzuri ya usalama wa bahari na usalama wa chombo, ili kazi iweze kufanyika kwa urahisi, umakini na fanisi kwenye ukanda wa bahari.

“Wananchi wakipatiwa elimu ipaswavyo basi usalama wa bahari, utatunzwa kizazi hadi kizazi ili kuendeleza kwa amani na usalama,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wanafunzi wanaomaliza masomo yao ya kidato cha nne, kuhakikisha wanachagua chuo cha DMI kujifunza fani mbali mbali, ikiwemo uhandisi wa meli, usalama wa bahari, meli na masuala ya Oil na gesi.

Nae Afisa udahili chuo cha bahari Dar es Salaam (DMI) Rehema Athumani Juma, aliwataka wazazi, walezi na wanafunzi kutembelea chuo cha bahari, kwani DMI kinaenda sambamba na sera ya uchumi wa buluu kwa kuhakikisha bahari inakua salama.

Alisema DMI ni chuo kama ilivyo vyuo vyengine na hakina sifa ngumu na kinapokea wanafunzi wa sifa zote, kama zinazotolewa na vyuo vyengine vya serikali na kitoa fani zote zinazohusiana na bahari.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu skuli ya shengejuu sekondari Hamad Hamad Mussa, alisema kutembelea banda la chuo hicho wamepata  elimu ya kutosha, ikiwemo suala la uokozi ikizingatiwa wanafunzi wa Pemba ni wasafiri wa mara kwa mara.

Hata hivyo aliwashauri wananfunzi kuhakikisha wanapomalizia kidato cha nne, kujiunga na chuo cha bahari kupata taaluma mbali mbali zinazohusiana na masuala ya bahari kama ilivyo kwenye vyuo vyengine nchini.

Nae mwanafunzi Sajidi Abdalla Ismail, alisema visiwa vya Unguja na Pemba, vimezungukwa na bahari na wananchi wengi wanatumia bahari kwa shuhuli zao za kijamii, hivyo kujiunga na chuo hicho wataweza kupata ujuzi na elimu ya usalama wa bahari kwa ujumla, ikizingatiwa Zanzibar inasera ya Uchumi wa buluu.

Chuo cha Bahari kilianzishwa mwaka 1978 kama kitengo na 1991 kupitia sheria ya nchi kilipitishwa kua chuo na kuanza kutoa kozi mbali mbali ikiwemo ya ubahari hadi 2000 kutoa kozi daraja la tatu hadi uhandisi na unahodha meli.

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari Portal blog
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355