Wednesday, January 15

Vijana waeleza namna wanavyokabilina na changamoto kusaka fursa za ajira

Vijana waeleza namna wanavyokabilina na changamoto kusaka fursa za ajira 

  • Wadau kukutana na vikwazo wakisaka mikopo, uwezeshaji

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

SOTE tunafahamu kuwa vijana ndio tegemeo kubwa la taifa na ndio wazalishaji wakubwa katika nchi yoyote ile ulimwenguni.

Miongoni mwa mazingira hayo kuanzishwa kwa baraza la Vijana, uwepo wa sera ya vijana, kuwepo na mikakati mbali mbali inayosimamia vijana, asasi mbali mbali za kiraia nazo zimekua na mchango mkubwa katika kusaidia vijana.

VIJANA WENYEWE WANASEMAJE

Maryam Mussa Salum (22) mkaazi wa Ng’ambwa, anasema changamoto kubwa ni kuwezeshwa, upatikanaji wa mitaji na elimu ya kutoka, kwani bila ya elimu hakuna linaloweza kufanyika.

“Mfano kijana anakwambia ndoto yake ni kufanya biashara, lakini hana elimu wala mtaji, unadhani anaweza kufikia ndoto yake,”anasema.

Anasema baadhi ya miradi inayoanzishwa inatatua changamoto za vijana, kwa kujikwamua na umaskini kwa mfano miradi ya TASAF, ambao wengi imeweza kuwasaidia, kwa kupata sare, mabuku, fedha za kulipia masomo na vitabu.

Juma Hamad Khamis (28) mkaazi wa mjini Chake Chake, anasema hata vijana wawe na mwamko gani, kama changamoto ya elimu na mitaji haijatatuliwa hawawezi kufikia ndoto zao kiuchumi.

“Sisi hapa zaidi ya mara tatu, tushaomba mikopo na kutimiza masharti yote, ila hadi sasa bado mkopo huo hatujautia mkononi, tatizo ni kupunguza masharti ya mikopo kwa vijana.

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab, akivuna tungune katika shamba la vijana wa Mjini Ole huko kangagani.WADAU WA VIJANA WANASEMAJE

Naye Afisa Uwezeshaji Jamii Kiuchumi kutoka TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar anasema, tayari vijana zaidi ya 200 wamewapatiwa elimu, juu ya shughuli za kuwatengezea kipato, elimu jinsia, uongozi na biashara.

Anasema, bado vijana wenyewe hawana uwelewa wa kuzifuatilia fursa ya kufanya kazi, pia hakujakuwa na mazingira wezeshi ya vijana, kuzifikia fursa ikiwemo ujasiri hayapo.

“Hivi sasa kuna mchakato wa kuwashajihisha vijana kujikita katika ujasiriamali, elimu haiko katika mfumo wa kumuwezesha kijana baada ya kumaliza masomo yake kuwa mjasiriamali, wakati vijana wanatakiwa, kuandaliwa mapema anapomaliza tu na kuingia, katika shughuli anazozitaka,”amesema.

Ali Mussa Bakar anasema changamoto kubwa inayowakaza vijana ni uhaba wa mitaji, elimu na utaalamu kutokana na shughuli wanazozifanya vijana.

“Hebu angalia hivi sasa miradi ya UVIKO 19, inatolewa na CRDB lakini kwanza, inachukua muda, kijana anaweza kuomba mwezi wa kwanza akaambiwa subiri, ukingalia shughuli yake ikawa imeshamaliza na kupoteza matumaini,”amesema.

Anaona wakati mwengine hiyo inayotolewa, mtu anaweza kuomba shilingi milioni 10 na akapewa shilingi milioni 2, jambo ambalo halifikii malengo ya kijana husika.

Anasema shughuli za kiuchumi zimegawika sehemu nyingi, wanaofanya biashara, kilimo, ushonaji, uvuvi, changamoto ya elimu na utaalamu ndio kikwazo kwa shughuli wanazozifanya.

Aidha anasema wapo wanaofanya kwa kutumia uzoefu, angalia sasa hivi kuna boti zimetolewa na zina ‘GPS’ jee utaalamu wa kutumia kifaa wanacho, mikopo inatolewa na baadhi ya taasisi.

Khamis Haji Yunus anasema baadhi ya miradi inatatua changamoto za vijana, mfano jina wa Tungule wanasema hata kuajiriwa serikali hawataki, wapo waliopatiwa vyarahani 10 na wanafanya kazi mpaka usiku.

Anasema kunakikundi cha uvuvi walipatiwa boti, walipata shilingi milioni 9  na kuwasaidia kuazisha miradi mengine midogo midogo, kama ufugaji wa kuku na kuongeza boti nyengine ya kuvulia na inasaidia katika upatikanaji wa kipato.

Anasema vijana waliamka kuna vikundi zaidi ya 100 wanasubiri kupatia mitaji, huko ‘CRDB’ huku asimilia 45 imetengwa kwa vijana na maeneo mengi vijana wameanzisha vikundi.

MABARAZA YA VIJANA

Makamu Mwenyekiti baraza la Vijana Wilaya ya Chake Chake Zulekha Maulid Kheir, anasema vijana wamekosa elimu ya ujasiriamali, elimu ya kutumia fursa za mikopo (mitaji), soko kwa wale ambao tayari wameanza kujitoa.

“Mfano mradi kikundi unawejengewa kisima, zinazotumika karibu shilingi bilioni 30, lakini vijana wanachokipata baada ya mavuno hakifiki hata shilingi 400,000, kitu ambacho hakiendani ukiangalia kikundi kina vijana 25 hadi 30 wakigawana hawana wanachopata,”amesema.

Miradi mingi imetekelezwa, lakini karibu yote imefeli katika kutatua changamoto za vijana, maana wanashindwa kushirikishwa ipasavyo, na ndio wakati mwengine wanahitajia vitendea kazi vya kilimo wanapewa vya uvuvi.

Nae Mwenyekiti baraza la Vijana Wilaya ya Mkoani Abdallah Saleh Issa, anasema changanmoto kubwa vijana wengi hawana taaluma ya kutosha juu ya kuanzisha biashara na kusimamia, mitaji ni tatizo kwao.

“Tumekua tukifeli katika kuandaa mpango mkakati madhubuti wa kuwasaidia vijana, ili kuweza kufikia ndoto zao lazima tuwe makini hapa katika mikakati na kuwashirikisha moja kwa moja vijana husika,”amesema.

IDARA YA VIJANA PEMBA

Kaimu Mratib Idara ya Maendeleo ya vijana Pemba Seif Edward Kabeyu, anasema sula la ujasiriamali kwa Zanzibar, bado vijana halijawaingia ipasavyo, na wanashindwa kuipokea kuona ujasirialami ni sekta binafsi inayoweza kumpatia fursa kujiajiri.

“Vijana wengi wanajua, ili kuwa na maisha bora ni kuajiriwa serikalini na kusahau kama ujasirimali, unaweza kumtoa kimaisha, kwani wapo vijana ambao wamefanikiwa kutokana na ujasirimali,”amesema.

Changamoto nyengine ni wanaozalisha wanakubwa na uhaba wa mitaji ya asili, wengi wao wanategemea mikopo inayotoka katika taasisi za kifedha, wengine wakilalamika mikopo sio rafiki kwao, ikiwemo kiasi wanachokihitaji hawakipati, wanapotaka mikopo hupatiwa muda umeshapita.

MJUMBE kutoka ubalozi wa Norway Tanzania Vivian Hilde Opsvik, akiangalia zao la tungule kutoka katika kikundi cha Jiandale kilichopo mchangamdogo, wakati wa ukaguzi wa miradi na kuangalia mafanikio yake, kupitia utekelezaji wa mradi wa utengamano wa jamii na amani Zanzibar unaotekelezwa na taasisi za kidini

“Unajua ukweli tuseme vijana wengi wanaofanya shughuli za kiuchumi, benk ya CRDB sio rafiki kwao kutokana na mfumo wa utoaji wa mikopo kuwa na vikwazo vingi, kwa vile inajiendesha kibiashara zaidi,”anaeeleza.

Kwa upande wake Mratib wa baraza la Vijana Pemba Hafidhi Rajab Khamis, anasema changamoto zinazowakanza vijana zimegawika sehemu tatu, kabla ya uzalishaji, mabadiliko ya tabia nchi na ugonjwa wa mazao.

Ukosefu wa taaluma kwa vijana wengine wanalima bila ya kufuata kanunui za kilimo, na baada ya mavuno soko ni tatizo kutokana na mazao wanayo zalisha.

WAKALA WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

KAIMU Mratibu wa wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar Ofisi ya Pemba Haji Mohamed Haji, anasema katika kipindi cha Machi 2021 hadi Mei 2023 shilingi bilioni 7.171 zimetolewa kwa wanufaika 12,277 wanawake 5617 na wanaume 6,660.

Fedha hizo zimetolwa kwa vikundi, mtu mmoja mmoja na bodaboda ndani ya kisiwa cha Pemba, wengi wa wajasiriamali wakishindwa kufafanua miradi wanayoiyomba na jinsi ya urudishaji wa fedha.

Anaona tatizo kubwa ni ukosefu wa elimu ya ujasiria mali na jinsi ya urudishaji wafedha watakazopewa, hali inayopelekea baadhi ya vikundi kuandikiwa barua.

MWANDISHI wa Habari Raya Ahamda kutoka ZBC TV akipiga picha alizeti zilizolimwa na vijana wa mjini Ole, katika mashamba yao huko Kangagani

SERA INASEMAJE

Sera na Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2005, imeweleza wazi jukumu kubwa la sera hiyo ni kuweka mazingira mazuri ya kupata fursa za kiuchumi.

Aidha Sera imetoa fursa na kuzitaka taasisi nyengine kuhakikisha zinakua na sera rafiki kwa Vijana, waweze kupata mahitaji yao pale wanapoyahitaji na kuzitaja sekta ya kilimo, uvuvi, maji,

MIKAKATI YA WIZARA IKOJE KWA VIJANA

Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, amesema Wizara inatataua changamoto za vijana kupitia sera ya vijana ambayo ndani imeweka njia mbali mbali kutatua changamoto vijana.

Amesema wakati mwengine sera imepitwa na wakati au ina mapungufu lakini kupitia hizo njia wanaweza kurekebisha kidogo kidogo na kufikia matarajio ya vijana.

Mikakati mengine ni kupiti mabaraza ya vijana yameweka kwa ajili ya kwamba vijana wanapata fursa ya kuzungumza shida au changamato zao, baraza la vijana ni sehemu ya chombo cha serikali na inatatua hizo changamoto kupitia nia sahihi.

“Sasa hivi tunamiradi inayoterkelezwa Unguja na Pemba, kituo cha vijana Weni na Mjini Ole, vituo vikimalizika vijana watapata fursa ya kwenda kupata taaluma alau ya kutatua changamoto zao,”anasema.

Upande mwengine, kwa mwaka wa fedha 2021/2022, programu ndogo ya vijana ilitengewe shilingi bilioni 7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ingawa hadi Machi 2022 hakuna fedha iliyopatikana.

Aidha katika bajeti kuu 2022/2023, program ya maendeleo ya vijana ilitengewa shilingi bilioni 6.4, ingawa hadi kufikia mwezi Machi 2023, hakukuwa na fedha iliyoingizwa katika eneo hilo.

Wakati hati yakifanyika hayo, kwa bajeti kuu ya fedha ya mwaka 2023/2024, wizara imetenga tena shilingi milioni 628.598, kwa ajili ya kuongezeka idadi ya ajira kwa vijana.

WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame Khamis, akiangalia kilimo cha zao la Vanila kilivyoshamiri katika mashamba la mkulima Hamad Salim Hamad, huko Gando Wilaya ya Wete wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya Viungo Project, unaotekelezwa na taasisi tatu PDF, CFP na TAMWA kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

NINI KIFANYIKE

Mwenyekiti baraza la Vijana Wilaya ya Mkoani Abdallah Saleh, ansema ni wakati sasa kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia vijana, ili kufikia ndoto zao na sio mfuko huo kuchanganywa na mambo mengine.

Mfuko huo utaweza kumsaidia kijana pale anapohitaji shilingi milioni 10 na wakati wamekua na wazo zuri la mradi, na sio kuambiwa subiria au kupatiwa milioni tatu kitu ambacho hakikidhi haja.

Nae Makamu Mwenyekiti baraza la Vijana Wilaya ya Chake Chake Zulekha Maulid Kheir, anasema ni wakati sasa kwa vijana wa vyuo kutumia fursa ambazo zipo, na kuingia katika shuhuli za uzalishaji, kwa kupatiwa elimu juu ya mbinu mbali mbali za ujasiriamali.

“Tunahitaji kuwepo na sera na sheria zilizorafiki kwa vijana, ambazo zitaweza mkazo zaidi katika kuwasaidia moja kwa moja vijana na sio kuwa na mzunguruko,”amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mratib Idara ya maendeleo ya Vijana Pemba Seif Edward Kabeyu, anasema Tanzania bara kuna mfuko wa vijana ambao unasaidia moja kwa moja, wala haujajumuisha makundi mengi.

Anaona ni wakati sasa na Zanzibar, kuwa na mfuko maalum wa vijana, utakao wasaidia moja kwa moja.

MWISHO

mwandishi wa kamala haya anapatikana kwa mawasiliano:

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari Portal blog
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355