Thursday, January 9

Dk.Mwinyi atoa neno kwenye jukwaa la kimataifa la mageuzi ya mifumo ya chakula barani Afrika, (AGRF) 2023.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema bara la Afrika lina kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa waliyonayo na kuyaendeleza kwa kutumia ubunifu, utekelezaji wa Sera na mikakati iliyojiwekea kwa maendeleo ya uchumi wao na kuimarisha mifumo bora ya chakula ili liendelee kujitegemea na kujitosheleza kwa hali zote.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipozungumza kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam alipotoa neno la shukurani baada ya kumalizika kwa jukwaa la kimataifa la mageuzi ya mifumo ya chakula barani Afrika, (AGRF) 2023.
Rais Dk. Mwinyi amesema Afrika izingatie na kuyafanyikazi matamko ya Agenda 2063 ya Umoja wa bara hilo pamoja na kutekeleza mikakati jumuishi ya uchumi wa bahari kufikia mwaka 2050 ya (AU) ambao bado haujatekelezwa ipasavyo.
Alisema, Mkutano wa kimataifa wa mageuzi ya mifumo ya chakula Afrika AGRF umezingatia zaidi usalama wa chakula kwa kuweka historia ya kuwakutanisha viongozi wakuu wa Afrika mbali na mambo mengine, walijadili namna ya matumizi sahihi ya rasilimali za bara hilo na kubuni mikakati mipya ya kuijenga upya mifumo ya chakula barani humo.
Aliainisha mifumo hiyo, kuanzia uzalishaji mazao, uhifadhi, usarifu na uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha bidhaa za kilimo na uvuvi, miundombinu na mawasiliano, usafirishaji, teknolojia za kisasa na utafiti.
Alisema, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zikiwemo UVIKO19, uhaba wa pembejeo za kilimo, mdororo wa fursa zilizopo katika masoko ya bidhaa zetu. mabadiliko ya tabia nchi, athari za kimazingira, kutetereka kwa uchumi wa dunia, migogoro ya bara la Afrika inayoathiri mifumo yetu ya chakula, Afrika hainabudi kusimama imara kuimarisha ubunifu, teknolojia, mitaji, miundombinu, na uwekezaji wa kilimo na mifumo ya chakula.
“Afrika tumejipanga upya kuzitumia rasilimali zetu za ardhi na bahari katika uzalishaji zaidi wa chakula licha ya athari za mabadiliko ya tabianchi” alifafanua Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema yote hayo yatawezekana ikiwa Afrika itazidisha nguvu ya pamoja, kuwekeza kwenye kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuzingatia usawa wa jamii na jinsia kwa maendeleo ya vijana na wanawake wa bara hilo.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuiletea nchi maendeleo ya uchumi na diplomasia pamoja na heshima kubwa kwa bara la Afrika.
“Mkutano huu ni matokeo chanya ya utekelezaji wa Sera mpya ya diplomasia ya uchumi ya Tanzania”. Alisifu Dk. Mwinyi.
Wakizungumza kwenye mkutano huo Wakuu wa nchi za Afrika, walijadili namna ya kutengeneza na kuzitumia fursa kwa vijana na wanawake katika mpango wa usalama na kujitosheleza kwa chakula na kilimo biashara na kuihakikishia dunia kwamba Afrika sasa imepania kuilisha dunia na kujitosheleza kwa chakula na kumuondoa adui njaa.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Jukwaa hilo la kimataifa la mifumo ya chakula barani Afrika, baada ya lile la mwaka 2012 lililofanyika jijini Arusha chini ya kauli mbiu yake “Kukuza uwekezaji na ubunifu, kwa ukuaji endelevu wa kilimo kwa usalama wa chakula.”
Kongamano la kimataifa la mwaka huu, liliwakutanisha pamoja viongozi wakuu mbalimbali wa bara la Afrika, wadau wa maendeleo, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, taasisi za elimu, mabenki na wafadhili mbalimbali.
IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR