Othman Machano, Afisa Elimu Wilaya ya Kaskazini B ambaye ni mwanakamati ya kupinga udhalilishaji akichangia mada wakati mkutano wa kuwasilisha ripoti ulioandaliwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA).
ZANZIBAR.
KAMATI za kupinga vitendo vya Udhalilishaji Zanzibar zimeshauri kuundwa kwa mfumo utakaotoa fursa elimu ya ndoa kuanza kufundishwa katika ngazi mbalimbali kwenye taasisi za elimu ili kutoa nafasi kwa vijana kujifunza misingi ya ndoa na kuielewa kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Wameeleza ukosefu wa mfumo huo unapelekea vijana wengi kuingia kwenye ndoa bila kupata elimu ya kutosha ya ndoa jambo linalosababisha kuongezeka kwa talaka zisizokuwa za lazima.
Ushauri huo umetolewa wakati wa kikao cha kuwasilisha ripoti ya miezi mitatu ya ufuatiliaji na utoaji wa elimu ya kupinga vitendo hivyo katika jamii kilichoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kupitia mradi wa kutumia Jukwaa la Habari Kupambana na vitendo vya udhalilishaji unaotekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la maendeleo ya Denmark (DANIDA).
Walisema hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la migogoro ya familia na kupelekea ndoa nyingi kuvunjika jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa vijana kutambua misingi ya ndoa kabla ya kuoana.
Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kati, Ali Sheha alisema katika Wilaya hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kumeripotiwa kesi saba za kutelekezwa, malezi kesi tatu, kubaka kesi tatu, Shambulio la kuumiza mwili kesi moja ambapo chanzo kikubwa cha kesi hizo ni matokeo ya utelekezaji uliotokana na migogoro ya ndoa.
Kwa upande wake Dodo Rajab Ismail, Afisa Jinsia wilaya Mangaribi A Unguja, alieleza licha ya Ofisi ya Mufti kuchukua juhudi za kuanzisha madarasa maalum ya kutoa elimu ya ndoa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maimamu lakini bado elimu hiyo haitoshi kuwajenga vijana kutambua misingi ya ndoa kutokana na inatolewa kwa muda mfupi na kwa watu maalum.
Alishauri kuundwa kwa mfumo maalum utakaoweka mazingira ya ulazima kwa vijana wote kupata mafunzo ya ndoa kuanzia ngazi ya awali.
“Ili kukabiliana na hili tatizo la ongezeko la talaka, tunahitaji kuwepo madarasa maalum ya kufundisha masomo ya ndoa kwenye skuli na madrasa ili vijana wajifunze kwa undani masuala ya ndoa na sio kupata mafunzo hayo pale tu wanapotaka kuingia kwenye ndoa,” alifahamisha Dodo Rajab Ismail, Afisa Jinsia wilaya Mangaribi A.
Katika hatua nyingine kamati hiyo ambayo inaundwa na maafisa kutoka idara mbalimbali za serikali ngazi ya wilaya wakiwemo Dawati la kijinsia Jeshi la Polisi, Usitawi wa jamii, mkono kwa mkono, mahakama, waratibu wa kupinga ukatili pamoja na viongozi wa dini walisema ipo haja ya jamii kurudi katika malezi ya pamoja waliolelewa wazee hali iliyosababisha vijana kukuwa katika maadili mema.
Jamal Himid Hassan, afisa jeshi la Polisi kituo cha Mwera, Wilaya ya Magharibi A alieleza, “suala la talaka tujiangalie sisi wazazi kwanza tuko sawa.? Lazima tubadilike, wazazi wengi sasa hivi tumekuwa waongo na wanafiki, kila mmoja hakubali kosa la mtoto wake hata kama mtoto kakosea.”
Mapema afisa mradi huo Zaina Salum aliwahimiza wanakamati hizo kuendelea kushirikiana kwa ukaribu katika kufuatilia matukio ya udhalilishaji na kutoa elimu kwa jamii ili vitendo hivyo kumalizika Zanzibar.
“Mradi wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji umeanza mwaka 2018 na unamaliza Sep 2023 hata kama mradi huu unamaliza, harakati hizi hazimalizi na tutaendeleza gurudumu hili ili tutokomeze vitendo hivi Zanzibar na kuwiweka jamii yote salama,” alieleza afisa huyo.
Katika mkutano huo uliwashirikisha wajumbe kutoka Wilaya Tano za Unguja ikiwemo Kusini, Kaskazini A &B, Kati, Magharibi A, ambapo imegundua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii ni pamoja na muhali uliopitiliza, mlolongo wa kesi katika vyombo vya maamuzi, baadhi ya wazazi kuwafanya watoto wao mtaji, na Ushirikano mdogo wa wazazi katika malezi na makuzi ya watoto.