Friday, January 10

Ujenzi wa barabara Sisimizi andikoni Wambaa waanza kwa vitendo

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

HATIMAE wananchi wakijiji cha Andikoni shehia ya Chumbageni Wambaa, wameanza kuonja matunda ya serikali ya awamu ya Nane, kufuatia kuanza kwa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita mbili kutoka sisimizini hadi kijiji andikoni.

Ujenzi wa barabara hiyo unakuja kufuatia ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud Agosti 16/2023, kufika kijijini huko kusikiliza changamoto za wananchi hao ikiwemo suala la barabara.

Wakizungumza na Mtandao wa Habari Portal, wananchi wakijiji hicho, wamesema hatua hiyo ilianza ni ishara njema kwao, kwani vilio vyao vitaweza kutatuliwa kimoja kimoja.

Mohamed Haji Mwanakijiji andikoni, alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo itawarahisishia kupeleka mazao yao sokoni, pamoja na kuanza kukifufua kijiji chao kimaendeleo.

“barabara siku zote ndio inayorahisisha maendeleo ya sehemu, sasa maji, umeme, elimu na afya zote zitakuja wakati barabara imeanza na hata maisha yataanza kubadilika kwa wananchi,”alisema.

Alisema mwanzo madereva walikua wakiwatoza gharama kubwa kuwafikisha mizigo yao kijiji kwao, kutokana na ubovu wa barabara ilivyokua.

“Tulikua tunakusanyana tunaenda kuichonga barabara kila muda ukifika, kutokana na baadhi ya madereva kuogopa gari zao kuumia, kizazaaa kinakuja mjamzito anapotaka kujifungua ndio vichwa vinapoumma zaidi,”alisema.

Nae mwanakijiji Ali Kheir Haji, aliishukuru serikali kwa hatua za dharura zilizoanza kuchukuliwa juu ya matengenezo ya barabara hiyo, ambayo ilikua ikiwaumiza kichwa kipindi cha mvua kinapokaribia.

Alisema mvua zinaponyesha baadhi ya wakati wanafunzi wanashindwa kwenda skuli, kutokana na tope kuwa nyingi na kuhofia watoto wao kuchukuliwa na maji kwenye mito.

“Hatuna budi kuwashukuru viongozi wetu kwa kuonesha kwa vitendo uzalendo wao katika ujenzi wabarabara, sasa kila mama mjamzito atalazimika kujifungulia katika kituo cha afya baada ya barabara kukamilika,”alisema.

Kwa upande wake Mwanafunzi Heri Khamis Makame, alisema changamoto kubwa kijiji ilikuwa ni barabara, kipindi cha mvua shida kwenda skuli Tumbi, kwani hulazimika kutumia muda mrefu kwenda skuli hata wakifika masomo yameshaanza.

“Kuna baadhi ya siku tulikua tunapelekwa skuli na wazazi wetu, kutokana na kuogopa njiani tunamopita kwani baadhi ya wakatu hukumbana na vijana tukiofia kufanyiwa vitendo viovu,”alisema.

Nae Mwanafunzi Zainab Khamis Kombo, alisema kipindi cha mvua wanalazimika sare safi kuzitia mkoba yao na kuvaa nguo zilizokua sio rafiki, ili kuepuka kuchafuka kutokana tope barabarani wakifika skuli wanavua na kuvaa nguo zao safi.

Kwa upande wake Sheha wa shehia ya Chumbageni Mgeni Othman Shaame, alisema andikoni ni moja vijiji vilivyokosa huduma zote za kijamii, ikiwemo barabara, umeme, maji safi na salama hata skuli ya maandalizi.

Aidha aliishukuru wizara ya ujenzi kwa kuanza kutekeleza kwa ahadi yake kwa vitendo juu ya ujenzi wa barabara, kwani kipindi cha mvua barabara ilikua shida kupitika na wakati mwengine wanafunzi wadogo wanashindwa kwenda skuli.

Mapema afisa mdhamini Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema wizara hiyo imelazimika kutekeleza kwa vitendo ahadi yake, ili wananchi waweze kunufaika maendeleo yaliopo nchini.

Alisema kwa hatua ya awali wameanza kusafisha barabara hiyo, na tayari eneo la mita 700 limekamilika, huku wananchi wakiridhia baadhi ya vipando vyao kutokulipwa fidia ili barabara ikamilike.

Aidha mdhamini huyo alisema mikakati ya Wizara ni kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo, yenye urefu wa kilomira mbili ili wananchi waweze kunufaika na matunda ya serikali yao.

Hata hivyo alizitaka baadhi ya taasisi zilizotoa ahadi kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo ahadi zao, ikiwemo ZAWA, ZECO, Wizara ya Afya, Wiaara ya Elimu.

Kijiji cha Andikoni shehia ya Chumbageni kina wastan wa nyumba 52 na wakaazi 477, huku shughuli kuu za wananchi wa kijiji hicho uvuvi, kilimo na ufugaji

MWISHO