Wednesday, January 8

Wizara, wadau wajadili muongozo wa jinsia, ukimwi Pemba

NA FATMA HAMAD, PEMBA

AFISA Mdhamini wazara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Pemba Hafidh Ali Mohamed, amesema michango ya wadau mbali mbali katika ripoti ya awali ya mapitio ya muongozo wa jinsia na ukimwi, itasaidia kupatikana kwa mpango sahihi, utakaozingatia usawa wa kijinsia.

Afisa Mdhamini huyo aliyasema hayo, ukumbi wa Samail Gombani, wakati akifungua mkutano wa kupokea ripoti ya awali, ya mapitio ya uchambuzi wa muongozo wa jinsia na virusi vya ukimwi, uliowakutanisha wadau mbali mbali, kisiwani Pemba.

Alisema wizara, ikishirikiana na Tume ya Ukimwi Zanzibar pamoja na wadau wengine, imekuwa ikiweka vipaumbele katika masuala mbali mbali yanayohusu afya ya Jamii.

Alieleza kuwa, kwa hivyo maboresho hayo ya mwongozo huo, utakao zingatia mwitikio wa jinsia na Virusi vya ukimwi, utasaidia makundi yote ndani ya jamii kufikiwa na huduma stahiki.

‘’Kuna maradhi tofauti, ambayo yamekuwa yakiibuka ndani jamii ikiwemo Ukimwi, hivyo ripoti hiyo itasaidia kuweka mpango mkakati, ili kuhakikisha jamii inajikinga nayo, na watu wakawa na afya njema,’’alieleza Mdhamini.

Akiwasilisha tarifa ya matokeo  ya awali, yaliopatikana wakati wa kukusanya maoni ya uchambuzi wa muongozo huo, mshauri mwelekezi Kimwaga Muhidini Ali, alisema ripoti hiyo imetumia mbinu  tofauti,  katika ukusanyaji wa maoni.

‘’Tulihakikisha tunafanya mahojiano na watalamu mbali mbali, kama vile makundi malum, watu wa serikali, kupata maoni yao, ili kuona tunapata mitazamo tofauti ya watu,’’alieleza.

Alieleza kuwa, uwepo wa muongozo huo kutasaidia kujua ni kwa namna  gani mipango mbali mbali  ya nchi, yamezingatia usawa wa kijinsia, hasa katika upatikanaji wa huduma za Virusi vya ukimwi na Ukimwi.

Nao washiriki wa mkutano huo, walisema kuwa muongozo huo utakuwa ni mkombozi wa kupata haki zao, kwa watu wa mahitaji maalumu, hususani kwa watu wenye ulemavu.

MWISHO.