Monday, November 25

Acheni kukaa Ofisini teremkeni Skuli kuangalia maendeleo ya Wanafunzi

BAKAR MUSSA,PEMBA

WAKAGUZI NA MAOFISA ELIMU kisiwani Pemba wametakiwa kutokukaa Ofisini na badala yake wajikite zaidi katika kukaguwa maendeleo ya wanafunzi kwani pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa lakini imeonekana kuna mapungufu makubwa ya wanafunzi kutojuwa kusoma na kujibu masuala.

Hayo yalielezwa na Mratibu wa Elimu, Utumishi na uendeshaji Wizara ya Elimu Pemba Maalim Harith Bakar Waziri huko katika Skuli ya Limbani Wete wakati akizungumza na walimu , wanafunzi na maofisa Elimu kwenye maadhimisho ya siku ya kujuwa kusoma , kuandika na kuandika Duniani.

Alisema kuwa kuna juhudi mbali mbali zinachukuliwa na Serikali ili kuwajengea mazingira Wanafunzi ya kusomea lakini bado yapo mapungufu ya watoto kutokuwa na uelewa wa kujuwa kusoma na kujibu masuala hasa ya hesabu na Sayansi.

Aliwataka Walimu na Wazazi kuzidisha mashirikiano ya pamoja na kuongeza bidii katika ufundishaji ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuielimisha watoto ambao ndio tegemeo la Taifa la kesho.

“ Kumbukeni kuwa kazi yenu ni ya wito , hivyo hamuna budi kuifanya kwa moyo mkunjufu ili mbali na kupata maslahi hapa Duniani lakini na kesho mbele ya Allah pia tutarajie malipo makubwa”, alisema.

Alifahamisha wapo wadau wa maendeleo wakiwemo Taasisi ya Milele Zanzibar Faundation imekuwa mdau mkubwa anaesaidiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika uboreshaji wa Elimu kwa kujenga mazingira bora ya kujifunzia , ikiwemo utowaji wa mafunzo kwa walimu na vifaa hivyo ni vyema kuonesha bidii kubwa kwa kuongeza bidii katika kazi zenu.

Alisema jukumu la kuwapatia Elimu bora Wanafunzi nila kila mmoja hivyo waoneshe kukerwa na changamoto zilizopo kwa wanafunzi kutojuwa kusoma na kujibu maswali ili hapo baadae waoneshe mabadiliko.

Aidha aliwataka walimu kuwafundisha Wanafunzi wao maadili mema ili apale wanapokutana na Viongozi ama wakubwa wao waoneshe kuwa wamefunzwa na kuelimika na kuwa na utafauti na watu wengine.

Kwa upande wake mkuu wa miradi ya Elimu kutoka Taasisi ya Milele Zanzibar Faundation Aisha Juma akitowa salamu za taasisi hiyo  alieleza kuwa wamekuwa wakisaidiana na Serikali katika kuboresha maendeleo mbali mbali ikiwemo Elimu hivyo aliitaka jamii pamoja na walimu kuongeza uwajibikaji ili kuleta mafanikio mazuri.

Alisema kuwa Milele itaendelea kutowa misaada mbali mbali ya Elimu , lakini jambo kubwa ambalo litawapa faraja ni kuona kunakuwa na mabadiliko ya kielimu kwa Wanafunzi kwa kuelewa mambo ya aina tafauti ya kimasomo.

“ Tunachohitaji ni kuona mabadiliko kwa wanafunzi ili mwaka mwengine tuone wanafunzi wanakuwa wazuri kujibu masuala wanayoulizwa”, alisema.

Nae  Ofisa Elimu Sekondari Mmanga Hamad Mmanga aliwapongeza Milele kwa ushirikiano wao na wizara ya Elimu na kuahidi kusimamia yale mapungufu yaliopo ili kuleta mabadiliko kwa wanafunzi.

Hata hivyo aliwaomba wanafunzi kutembelea vituo vya Skuli HUB vilivyopo katika maeneo yao kujifunza mambo mbali mbali ya kimasomo ikiwemo lugha tafauti tafauti kwa ajili ya kufanya vyema katika masomo yao.

MWISHO.