Friday, November 15

MAKALA: Wajawazito wanaojifungulia majumbani wachungulia kaburi.

 

NA FATMA HAMAD, PEMBA

MIMBA yangu ya nne manusura niiage dunia.

Asha Said mama wa watoto 4 ambae sio jina lake halisi anasema,  mimba yake ya pili alijifungulia nyumbani, na alipata tatizo la kutokwa na damu nyingi,na kupelekea   hadi kupoteza fahamu.

‘’Baada tu ya kujifungua siku jifahamu tena, mpaka nilikuja kuzinduka nimewekewa chupa ya maji hospitali ya Micheweni,’’anaeleza.

Mume wa mama huyo ambae hakupenda  jina lake lichapishwe, anasema baada ya kuona hali ya mke wake imesha kuwa mbaya, ndipo usiku huo alipokodi gari na kumpeleka Hospitali.

Hivyo alipatwa na huzuni, hali ambayo ilipelekea kupoteza gharama kubwa ya matibabu, kwa ajili ya kuokoa maisha ya mke, pamoja na mtoto.

‘’Nilipata funzo na sasa ni kimuona tu uchungu umeanza namuwahisha Hospitali haraka, kwani huko akipata matatizo anaweza akawahiwa mapema na watalamu wa afya,’’anaeleza.

Maryam Said mkaazi wa Chake chake ambae anaishi na virusi vya ukimwi kwa muda wa miaka 18  alimuambukiza mtoto wake wa mwanzo mambukizi ya virusi vya ukimwi.

Kwani mimba yake ya kwanza, alijifungulia nyumbani, kwa hofu ya kwenda Hospital kwa kuogopa kunyanyapaliwa.

‘’Hadi leo najilaumu, na najutia nafsiyangu, kwa kitendo cha kutokimbilia hospitali kwa ajili ya kwenda kujifungua nikidhani kwamba nyumbani ni salama,’’anasimulia.

Kwasasa  ameshajifungua watoto  wengine watatu, ambao wako salama na vvu, baada ya kusikiliza na kutekeleza kwa vitendo ushauri wa watalamu wa afya.

Kumbe hata Halima Juma wa Mjini Kiuyu wilaya ya Wete  nae amepitia machungu kwa kule mimba zake tatu kujifungulia nyumbani.

Linalomkimbiza hosptali kwake yeye binafsi moja ni lugha za madaktari, nenda rudi isiyozaa matunda na hata suala la uhaba wa watalamu halimshawishi kujifungulia hospitali.

Khadija Khamis mama wa watoto watano,mkaazi wa  Sizini hadi leo hii bado hajafikiwa na elimu ya kuhudhuria kliniki na ndio maana hufika kwa watalamu baina ya miezi sita hadi saba ya ujauzito wake.

‘’Mimi sipendi kwenda kituo cha afya ikiwa bado mimba ni changa, si pendi ile kila siku nenda na keshokutwa uje tena naona tabu,’’anfafanua.

MTAALAMU WA AFYA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO

Akieleza athari anazozipata mama mjazito anapojifungulia nyumbani Maryam Ali Said Mratibu wa huduma za mama na mtoto Pemba anasema moja  ni kukosekana kwa  huduma za mapema za kimataibabu kwa mama mjamzito.

‘’Inawezekana ikawa mama hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida, analazimika afanyiwe upereshini, lakini mkunga wa jadi hana taluma ya kujua hilo,’’anaeleza.

Anasisitiza kuwa kuhudhuria kituo cha afya kuanzia wiki ya mwanzo ya ujauzito hadi kufikia kujifungua ni lazima kwa mjamzito ili kujikinga na majanga.

‘’Kujifungulia nyumbani ni sawa na kununua mauti, ya mama na mtoto wake, maana hakuna mtalamu, vifa vya kinga ya maradhi na wengine wanaishi mbali na vituo vikuu vya afya,’’anasema.

Fatma Suleiman Daudi msimamizi wa huduma ya mama na mtoto katika Hospital ya Chake chake, anaeleza kuwa     mjamzito akijifungulia nyumbani, anaweza kumuambukiza maradhi mtoto wake na  mkunga.

‘’Kama mama atakua ana mambukizi kama vile  Homa ya Ini au Virusi vya ukimwi bila ya kutumia kifaa chochote, anaweza kusababisha mtoto, mkunga kupata mambukizi,’’ anaeleza.

Mjamzito anaejifungulia nyumbani, anaweza kupata athari kiwemo kukaa kwa muda mrefu na uchungu, jambo ambalo linaweza likapelekea kuchanika haraka kwa fuko lake la uzazi.

‘’Mara nyingi wanapokuja Hospitali inakua mama ameshachoka, hali taabani, mpaka iwe wameshashindwa, hata ukija ukitoa tena izo tiba muda umeshapita,’’ afafanua mtaalamu.

Alifahamisha kuwa unapochanika kwa fuko la uzazi maranyingi mama hutokwa na damu nyingi ambayo inaweza kusababisha hata kifo chake.

‘’Unapochanika kwa fuko la uzazi, hatuwezi kusema kama ndo mwisho, lakini kama hukuwahiwa mapema kupatiwa matibau unaweza ukapoteza maisha,’’anafafanua.

‘’Kuna siku tulimpokea  mama na alikuwa ni ujauzito wake wa tatu, alivyo kuja akapelekwa kwenye chumba cha kujifungulia, kabla ya kumlaza kwa ajili ya kujifungua, tulimuhisi kalala kumbe ameshafariki,’’anasimulia.

Amina Omar Msellem mkaazi wa Chake chake anasema amejifungua mimba saba na zote ni kituo cha afya, wala hajapata changamoto yoyote yeye wala  watoto wake.

Abdala Nassor  Abdala mwananchi wa Chake chake anasema mama anapojifungulia nyumbani, mazingira  ya usafi Pamoja na usalama wa mama kujifungua salama yanakua hayatoshelezi.

Mkewake amejifungua mimba nane na zote alikua anampeleka Hospitali wakati anapoumwa tu na uchungu,’’anafahamisha.

Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja anasema ni vyema kwa wizara ya Afya kuongeza mkakati wa  elimu ili wanawake washawishike kujifulia hospitali.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui anasema wizara imeimarisha miundombinu  ya kutolea huduma Hospitalini, ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Afisa Mdhamin wizara ya Afya Khamis Bilal Ali amewataka wahudumu wa afya kuwa na lugha nzuri kwa wajawazito ili iwe ni sehemu ya ushawishi ya kuhudhuria kliniki.

‘’Wizara kwa upande wake inaendelea kuimarisha miundombinu bora ikiwemo vifaa tiba dawa, lakini ni nafasi kwa watalamu wetu wa Afya nao kutumia lugha laini ili kufanikisha hilo’’,anasema.

 

TAKWIMU

Kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya mama na mtoto Pemba,inaonyesha kuwa  kwa mwaka 2022 mama 2019 walijifungulia nyumbani, kati ya hao  wane [4] walifariki.

Waliojifungulia Hospital ni 16269 kati ya hao, Micheweni ni 985, Mkoani 754, Wete 9445 na Chake chake 5365, ambapo waliofariki kutoakana na uzazi ni 15.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia  Januari hadi Juni mwaka huu, wajawazito waliojifungulia nyumbani ni 1450, kwa upande wa wilaya ya Mkoani walikua ni  270, Chake chake 99, Micheweni 230 na Wete ni 292.

Ingawa wanaojifungulia Hospital kwa Pemba ni 8481, ambapo kwa  wilaya ya Mkoani ni 1562, Chake chake 2601, Wete 2140 na Micheweni 2178, huku vifo vikiwa tisa [9], ambapo Wete na Micheweni kulikuwa na vifo vitatu vitatu.

SERA NA SHERIA.

Sera ya wizara ya Afya ya Zanzibar ya mwaka 1990 ni kuhakikisha inaimarisha huduma za afya ya uzazi ya mama na mtoto, ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vya watoto wachanga.