Wednesday, January 8

Wananchi wahimizwa matumizi sahihi ya vyandarua kumaliza malaria.

NA AMINA AHMED-PEMBA.

WANANCHI wametakiwa kuvitumia kwa usahihi vyanadarua vinavyotolewa na Wizara ya Afya ili lengo la kumaliza malaria Zanzibar liweze kufikiwa.

Ametoa Ombi hilo mkuu wa Idara ya Tiba Massoud Suleiman Abdulla kwa niaba ya Afisa mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali wakati wa mkutano maalumu wa kutoa taarifa kwa wananchi kupitia waandishi wa habari juu ya hali ya malaria na ufuatiliaji wa ugonjwa huo kisiwani humo.

Amesema ili lengo la kumaliza Malaria Zanzibar liweze kufikiwa na kuwa %0 ni vyema wananchi kufuata taratibu zilizowekwa juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vinavyoendelea kutolewa bure kwa mama wajawazito na watoto wanapofika hospitali.

“Serikali inafanya kila jitihada kuona hiyo asilimia 0.4 ya ugonjwa wa Malaria uliopo inamalizika kabisa wadau wa maendeleo pia wanaunga mkono kuona kila mwananchi anankuwa salama dhidi ya ugonjwa huu lakini Baadhi ya wananchi huvitumia vyandarua hivyo kwa lengo ambalo silo kabisa lililokusudiwa”.Ameeleza.

“Wapo wanaovichana na kuzibia miche yao shambani na wao kulala bila vyandarua vilivyokuwa havijapigwa dawa niwaase kuacha hiyo tabia katika kuona tunasaidia serikali kumaliza Malaria yasiwepo kabisa”.Aliendelea kusema.

Aidha Mdhamini huyo amewataka wananchi kufika katika hospitali na vituo vya afya ili kuweza kupima Afya zao mara wanapoziona dalili za Ugonjwa wa malaria na kuacha kutumia dawa kinyume na utaratibu uliowekwa.

Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu kitengo cha Malaria Pemba Makame Muhamed Kombo amesema kitengo hicho kwa sasa kinaendelea na hatua mbali mbali katika kudhibiti ugonjwa huo ikiwemo kupiga dawa, kutoa vyandarua, kutoa elimu na kudhibiti wagonjwa kutoka nje kwa kupima afya wanapoingia kisiwani humo kwa lengo la kumaliza ugonjwa wa malaria.

Aidha Mkuu huyo Amewataka waandishi wa habari kusaidia kufikisha elimu hiyo kwa wananchi ili waweze kujilinda dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Katika kipindi cha Mwezi wa 1 hadi mwezi wa 7 mwaka 2023 jumla ya wananchi 5,755 wamefikiwa na kupewa vyandarua vilivyotiwa dawa katika wilaya ya Wete huku Wilaya ya Mkoani wananchi 4,417 wilaya ya Micheweni ni 5,474 na Wilaya ya Chake chake 5,390 ambao ni mama wajawazito na watoto waliopiga chanjo huku upimaji wa ugonjwa huo majumbani ukifikia Asilimia 96.33 na kubainika kuwa na Asilimia 0.016 ya uathirikaji wa ugonjwa huo kwa waliobanika.

Mwisho.