Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zena A. Said amesema kuwa APRM Tanzania ni chombo muhimu sana kukitumia kwa wananchi lakini pia kwa Serikali kwakuwa kinatumika kutathmini yale yote yaliofanywa na Serikali kwa lengo la kuimarisha maeneo ambayo yana changamoto na kuongeza nuru katika maeneo ambayo Serikali inafanya vizuri zaidi.
Hayo ameyabainisha mapema leo hii alipokutana na ujumbe kutoka APRM Tanzania ambao walifika Ikulu Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kuelezea dhana nzima ya APRM na mikakati ya kuelekea katika Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora Tanzania.
Mhandisi Zena amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mambo mengi mazuri na makubwa ambayo yanahitajika kuzungumzwa ili wananchi wa Tanzania na dunia ielewe kwa namna gani Tanzania imepiga hatua katika masuala ya Utawala Bora.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano ambao APRM Tanzania inahitaji katika kuhakikisha kuwa taarifa za Zanzibar zinapatikana kwa wepesi na kwa wakati ili zisaidie katika uandishi wa Ripoti hiyo pamoja na kuwataka APRM kuhakikisha wanawafikia wadau muhimu wakiwemo Wabunge na Wawakilishi ambao wanafanya kazi moja kwa moja na wananchi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Bw Lamau A. Mpolo amesema kuwa APRM ipo katika maandalizi ya kuandaa na kuandika Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora nchini, hivyo amewaomba wadau, watendaji wa Serikali na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano endapo wataalamu wa kukusanya taarifa watafika katika maeneo yao.
Bw Mpolo amesisitiza kuwa taarifa za APRM zina umuhimu mkubwa ikiwa ni pamoja na kutumika kama rejea muhimu juu ya masuala ya utawala Bora, mpango wa APRM pia unawagusa wananchi walio wengi ambapo unasaidia sana kutimiza dhana inayoungwa mkono duniani kote ya utawala shirikishi unaowapa wananchi fursa ya kuishauri Serikali yao.
Akizungumza katika kikao hicho Meneja Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania Badria Atai Masoud amesema kuwa licha ya kuwa APRM ina changamoto kubwa ya kutokufahamika vyema na wananchi ila imejipanga vizuri kufanya kampeni kubwa ya uhamasishaji kwa Tanzania nzima ambapo lengo kuu ni kuwafikia wananchi walio wengi na hatimae waweze kushiriki katika utoaji wa maoni katika Tathmini ya Pili ya Utawala Bora Tanzania.
Akitoa neno la Shukrani Mratibu wa eneo la Uchumi Jamii APRM Tanzania Balozi Hemedi Mgaza ameshukuru sana kwa ushirikiano makubwa wanaopata kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaonesha jinsi gani Serikali ilivyojidhatiti katika kuhakikisha kuwa Ripoti ya Pili inafanikiwa lakini pia ameahidi kuyafanyia kazi yale yote maelekezo na miongozo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa APRM Tanzania.