NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.
MBUNGE wa Jimbo la Mkoani Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, ameagiza kuvunjwa kwa banda bovu lenye vyumba vinne vya kusomea, wanafunzi wa skuli ya msingi Makoongwe ili kujengwa kwa banda jipya la kisasa.
Hayua hiyo imekuja kufuatia banda kongwe linalotumiwa kusomeshewa wanafunzi kupasuka kila sehemu, kutokana na ukongwe wake tokea mwaka 1947 lilipojenga huku likifanyiwa ukarabati.
Kauli hiyo aliitoa katika mkutano wakusikiliza kero za wananchi wa Kisiwa hicho, ikiwa ni ziara ya kutembelea shehia kwa shehia zilizomo ndani ya jimbo la Mkoani.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge huyo, Katibu wa Mbunge jimbo hilo Mariyam Said Khamis, alisema banda hilo watahakikisha linajengwa la kisasa ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao ndani ya mwaka huu.
“Lengo ni kuinua kiwango cha elimu ndani ya jimbo letu, ikiwemo shehia hii ya Makoongwe ili tuweze kutoa wataalamu sisi wenyewe huku huku makoongwe,”alisema.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa banda hilo, kutaondosha mfumo wa kuchanganya madarasa mawili kwa wakati mmoja, hali itakayopelekea urahisi kwa walimu kufundisha madarasani.
Akizungumzia suala la usafiri, aliahidi kuwapatia boti itakayoweza kuwasaidia wananchi kufuata huduma za matibabu hospitali ya Abdalla Mzee, pamoja na kutanuliwa kwa kituo chao cha afya kijijini hapo.
Nae diwani wa wadi ya Michenzani Mashavu Amour, alisema viongozi wa jimbo wamefanya mambo makubwa ndani ya jimbo ikiwemo sekta ya elimu.
Alisema kwa sasa changamoto ya kisiwa cha Makoongwe ni maji, na tayari ZAWA wamesharuhusu kisima cha michenzani maji kupelekwa moja kwa moja makoongwe na sio kugaiwa na michenzani.
Kwa upande wake afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mwalimu Mohamed Nassor Salim, amekiri kupokea taarifa ya kuvunjwa banda hilo bovu, jambo ambalo ni faraja na timu ya wataalamu wa wizara, imetumwa kwenda kuliangali ili hatua zaidi ziweze kufuatwa.
“Tumetuma injinia wa wizara kwenda kulitizama, ikiwa linafanyika ukarabati basi lifanywe na ikiwa halikubali kufanyiwa basi litavunjwa na kujengwa upya,”alisema.
Aliwataka wananchi, wazazi na wadau wa maendeleo kuendeleo kumuunga mkono Rais wa Zanzibar, kwa kushirikiana na kilichofanyika kukilinda, pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi ikiwemo sekta ya elimu.
Aidha aliwataka wananchi kuwapima viongozi wao wa majimbo kwa kuoangalia ubora wa maendeleo wanayoyafanya, kwa kuhakikisha wanawarudisha madarakani kwenye uchaguzi unaofuata.
Akitoa changamoto za Kisiwa cha Makoongwe, Mkubwa Ali Yussuf alisema kilio chao kikubwa ni ubovu wa banda lenye vyumba vinne vya kusomea wanafunzi, kwani walishakatazwa mara tatu kutokulikalia kutokana na ubovu wake.
“Viongozi wa wizara na wataalamu wameshafika zaidi ya mara tatu na kututaka tusilikalie, ni kongwe tokea mwaka 1947 lakini hatuna sehemu nyengine na hivyo wanafunzi wanachanganywa, tunahitaji banda jengine ili ufanisi wakusomesha upatikane,”alisema.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Makoongwe Salim Abdalla Ali, alisema msingi inawanafunzi 571 hali inayowalazimu baadhi ya madarasa mawili kuyachanganya kuwa moja.
Alisema darasa la nne wanawachanganya na kuwa darasa moja lenye wanafunzi 104, darasa jengine la sita wanalichanganya kuwa darasa moja lenye wanafunzi 75, Maandalizi one na two wanawachanganya kuwa darasa moja lenye wanafunzi 86.
“Kutokana na changamoto hii tunalazimika kufanya hivyo ili ufanisi uweze kupatikana, tena huku tumeazima madarasa matano kutoka sekondari ndio yanayotusaidia,”alisema.
Hata hivyo alisema kujengwa kwa madarasa mengine mpya, yatachangia kwa kiasi kikubwa kwani uhitaji wa vyumba vya kusomea makoongwe ni 14, kutokana na kisiwa kinakua siku hadi siku tafauti na miaka ya nyuma.
MWISHO